Juu
na Chini - Mafundi wakiendelea na kazi ya kulaza mabomba ya Maji eneo
la Mbezi Beach jijini Dar es salaam. Mabomba hayo ambayo sasa
yamekamilika kwa urefu wa kilometa 54.8 kati ya 55.9 yatatumika
kusafirisha maji kutoka mtambo wa kuzalisha maji wa Ruvu Chini, Bagamoyo
mkoani Pwani.
( Na. Aron Msigwa - Dar es salaam)
Huduma
ya Usambazaji wa Maji Safi katika jiji la Dar es salaam inatarajiwa
kuimarika kwa kuwafikia wananchi wengi zaidi mwishoni mwa mwezi Februari
mwaka huu kufuatia kukamilika kwa kilometa 54.8 za mradi wa Ujenzi wa
Bomba kubwa la kusambazia Maji kutoka chanzo cha Maji cha Ruvu Chini.
Mradi
huo unajengwa na Kampuni ya JBG Gauff Ingenieure kwa gharama ya
shilingi Bilioni 141 ambazo zimetolewa na Serikali ya Tanzania una jumla
ya urefu wa kilometa 55.9.
Akizungumzia
mradi huo leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Usimamizi na Ufundi
wa DAWASA, Romanus Mwang’ingo amesema kuwa mpaka sasa ujenzi wa bomba
hilo kuelekea matangi ya kuhifadhia maji ya Chuo Kikuu cha Ardhi umefika
eneo la Mbezi Beach jijini Dar es salaam na huku ikiwa imebakiza
kilometa 1.1.
Amesema
ujenzi wa mradi huo kutoka mtambo wa Ruvu Chini ndiyo utakuwa suluhisho
la tatizo la maji katika jiji la Dar es Salaam na maeneo ya mkoa wa
Pwani na kuongeza kuwa utakapokamilika utazalisha lita milioni 270 kwa
siku kutoka lita milioni 182 ambazo zote zitasukumwa kuja jijini Dar es
salaam.
Aidha,
amesema kasi ya mkandarasi ya kulaza bomba hilo inaridhisha licha ya
kuwepo kwa changamoto mbalimbali zinazochelewesha kazi hiyo zikiwemo za
ufinyu wa eneo linapojengwa bomba hilo kuwezesha mitambo kufanya kazi
vizuri katika eneo la mbezi Beach, mvua zinazoendelea kunyesha
,changamoto ya makazi ya watu kuwa ndani ya mradi ambapo kulikuwa na
kesi 17 Mahakamani zikihusisha madai mbalimbali ya wananchi katika
maeneo hayo.
“Ni
kweli zipo changamoto zilizosababisha mradi kukawia kumalizika zikiwemo
za wananchi kufungua kesi 17 Mahakama ya Ardhi, hadi sasa DAWASA
tumeshinda kesi 14 ndiyo maana tumepata haki ya kutumia njia hii
kukamilisha upanuzi wa mradi” Amesema Mwang’ingo.
Ameongeza
kuwa lengo la mradi huu nikuongeza uzalishaji wa maji na kuboresha
huduma kwa wakazi wa maeneo ya uwekezaji (EPZ) Bagamoyo, Chasimba, Buma,
Zinga, Kerege na Mpiji mkoa wa Pwani.
Maeneo
mengine yatakayonufaika na mradi huo kwa Mkoa wa Dar es Salaam ni
Bunju, Wazo, Salasala, Madale na Kinzudi Mbezi Juu, Goba, Kawe, Makongo,
Mwenge, Msasani, Mikocheni, Mlalakua, Masaki, Sinza, Kijitonyama,
Manzese, Konondoni, Magomeni, Kigogo na Vingunguti.
Kwa
upande wake Meneja Mradi wa Kampuni inajenga bomba hilo nchini
Muhandisi Eric Omuruli akizungumzia mradi huo amesema kuwa yeye kama
Meneja mradi atahakikisha anashughulikia changamoto zilizopo ili
kukamilisha kwa wakati.
Amesema
kuwa licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali katika eneo la mradi
hasa eneo la Mbezi Beach jijini Dar es salaam kampuni ya JBG Gauff
Ingenieure inafanya kila linalowezekana ili mradi huo ukamilike mwishoni
mwa mwezi Februari mwaka huu.
“Tumejipanga
kufanya kazi hadi usiku kupunguza muda,kazi iliyobaki ni ndogo,
tunawahakikishia DAWASA tutaimaliza kazi hii mwishoni mwa mwezi huu”
Amesisitiza.
Mkurugenzi wa Usimamizi na Ufundi wa DAWASA, Romanus Mwang’ingo (katikati) akitoa ufafanuzi kuhusu maendeleo ya Mradi wa ujenzi wa bomba hilo la kusafirishia Maji kutoka Ruvu Chini kuelekea matangi ya kuhifadhia maji ya Chuo Kikuu cha Ardhi ambao umefika eneo la Mbezi Beach jijini Dar es salaam
0 comments:
Post a Comment