Adverts

Tuesday, March 22, 2016

Raia wa Marekani waandamana kumpinga Donald Trump


Kwa mara nyingine tena mgombea wa kiti cha Republican kwenye uchaguzi wa urais nchini Marekani, Donald Trump amekumbana na vikwazo wakati akijiandaa kwenda kwenye mkutano katika jimbo la Phoenix.

Waandamanaji walifunga barabara katika jimbo la Arizona wakati Trump akijiandaa kwenda kufanya mkutano katika eneo la Phoenix na kumzuia asipite.

Mgombea huyo kiti cha Republican kwenye uchaguzi huo alihutubia wafuasi wake katika eneo la Fountain Hills.

Waandamanaji hao walisababisha msongamano wa magari huku wakibeba mabango ya kumpinga Trump.

Mikutano ya mgombea huyo ilikumbwa tena na fujo hivi karibuni akitakiwa aache ubaguzi anaonyesha kwenye kampeni zake.

Mkutano wa Chicago wiki moja iliyopita ulilazimika kuahirishwa baada ya kutokea kwa maandamano makubwa ya kumpinga.

Mamia ya waandamanaji walikuwa wamekusanyika katika jimbo la Illinois na mapigano kuzuka kati ya wafuasi na waandamanaji katika jukwaa ambalo Trump alipanga kutoa hotuba yake.

Wiki iliyopita Shirika la Utafiti la Kimataifa Economist Intelligence Unit ( EIU) lilisema ikiwa Trump atakuwa rais wa Marekani ushindi wake utakuwa ni miongoni mwa hatari 10 kuu zinazokabili dunia.
Shirika hilo lilisema huenda ikawa ni chanzo cha kuvurugika kwa uchumi wa dunia pamoja na kuongeza hatari za kisiasa na ki usalama dhidi ya Marekani.

Shirika hilo lilisema ushindi wa Trump utakuwa hatari zaidi kwa dunia kushinda hata Uingereza kuondoka kutoka Umoja wa Ulaya (EU) au hata makabiliano ya kivita katika Bahari ya South China Sea.

Kuyumba kwa uchumi wa China au Urusi kuingilia kivita Ukraine na Syria na kusababisha vita baridi vipya ni miongoni mwa mambo ambayo yanachukuliwa kuwa hatari zaidi ya ushindi wa Trump.

“Mpaka sasa Trump ametoa maelezo machache kuhusu sera zake na huwa anabadilisha sana msimamo wake,” EIU walisema kwenye ripoti yao ya utathmini wa hatari zinazokabili dunia.

Utathmini huo huangazia pia athari za jambo fulani na uwezekano wa jambo hilo kutokea.

Vigogo 
Miongoni mwa masuala yanayowatia wasiwasi vigogo wa Republican ni msimamo mkali wa Trump dhidi ya wageni nchini Marekan na kuahidi kujenga ukuta katika mpaka wa kati ya Marekani na Mexico.

Pia, aliahidi kuwarejesha makwao wahamiaji milioni 11, ambao hawajapata hifadhi na kuwazuia raia wa kigeni waislamu kuingia Marekani.

Mitt Romney aliyegombea urais mwaka 2012 kwa tiketi ya Republican amemtaja Trump kuwa tapeli na bondia anayecheza na akili za wapigakura huku mgombea urais wa chama hicho mwaka 2008 John McCain ambaye ni seneta wa jimbo la Arizona akisema sera za kigeni ni hatari.

Kundi la vigogo wa Republican linalopinga azma ya Trump lina muda mchache kumzuia mfanyabiashara huyo tajiri kushinda tiketi ya Republican.

Mgombea huyo anapewa nafasi kubwa ya kuchaguliwa kuwania kiti cha urais kupitia chama chake cha Republic.

Awali kwenye uchaguzi uliopita na yeye alijitutumua kuchukua fomu ili achuane na Rais wa sasa Barack Obama lakini aliangushwa vibaya.

Licha ya kushindwa kuteuliwa kwenye chama chake mwaka huu ameamua kujitutumua kwa mara nyingine tena.

0 comments:

Post a Comment