Adverts

Friday, February 19, 2016

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu Atangaza Oparesheni Kamata Bodaboda Nchi Nzima


MKUU wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu amewaagiza makamanda wa Polisi kote nchini, kuendesha oparesheni kali ya kuwachukulia hatua za kisheria, waendesha bodaboda wasiotii sheria za usalama barabarani.

Ametaja makosa yatakayosababisha waendesha bodaboda hao kukamatwa kuwa ni pamoja na kubeba abiria zaidi ya mmoja, kupita katika taa nyekundu na kutovaa kofia ngumu.

IGP Mangu alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na maofisa wakuu wa Polisi, wakiwemo makamanda wa Polisi wa mikoa, vikosi na makao makuu katika kikao kazi kilichofanyika Dar es Salaam hivi karibuni ambacho kilifunguliwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga.

Alisema waendesha bodaboda wamekuwa wakikaidi kufuata sheria za usalama barabarani, lakini sasa mwisho wao umefika na kuwataka makamanda wa Polisi wa mikoa kote nchini, kutekeleza maelekezo hayo, ili kuleta nidhamu kwa bodaboda katika kufuata sheria za usalama barabarani.

IGP Mangu alisema suala la kufuata sheria za usalama barabarani kwa bodaboda halina mjadala na kila Kamanda ahakikishe kuwa wote wasiofuata sheria na kukaidi, wanakamatwa bila kuoneana muhali kwa kuwa wamekuwa wakisababisha ajali zinazoweza kuzuilika.

“Pamoja na kuendelea kudhibiti uhalifu wa aina zote, natoa maelekezo kwa kila mkoa kuhakikisha unaendesha oparesheni kali dhidi ya bodaboda, ili kupunguza ajali zinazosababishwa na bodaboda.
 “Wengi wao hawataki kufuata sheria na kanuni za usalama barabarani, tusiwaonee muhali maana maisha ya watu ni muhimu sana na jambo la msingi ni kusimamia sheria tu,” alisema IGP Mangu.

Awali akifungua kikaokazi hicho Waziri Kitwanga alilitaka Jeshi la Polisi kuendelea na mapambano yake dhidi ya uhalifu na wahalifu, ili usalama wa raia na mali zao uendelee kuimarika na Watanzania waendelee na shughuli zao za kujiletea maendeleo bila hofu ya kutendewa uhalifu.

0 comments:

Post a Comment