WAFANYABIASHARA
wa Rwanda wamepongeza hatua zinazochukuliwa na Rais John Magufuli
katika Bandari ya Dar es Salaam, kwa kuimarisha ufanisi wa bandari,
kukuza biashara baina ya Tanzania na nchi jirani.
Aidha
wamesema tangu Rais Magufuli aanze kuchukua hatua hizo, mizigo yao
imekuwa salama zaidi na wamefanikiwa kuipata kwa urahisi tofauti na
zamani ambapo mingi ilikuwa ikipotea.
Hayo
yalielezwa jana na Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Augustine Mahiga wakati
akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).
Akizungumza
baada ya kutua nchini akitokea Kigali, Rwanda, Balozi Mahiga alisema
pia Rais wa nchi hiyo, Paul Kagame amemhakikishia kuwa ataendelea
kushawishi wafanyabiashara wake kutumia Bandari ya Dar es Salaam, ili
kukuza uhusiano wa kibiashara uliopo.
“Nilipata
bahati ya kuzungumza na wafanyabiashara wa kule... wamepongeza sana
hatua zinazochukuliwa na Rais Magufuli pale bandarini kwa sababu
wanasema sasa hivi itawasaidia sana kuhakikisha usalama wa mizigo yao,” alisema Blozi Mahiga.
Alisema
wafanyabiashara hao pia wameomba mkutano wa pamoja na wenzao wa
Tanzania, ili kujadili masuala mbalimbali, ikiwemo fursa za uwekezaji
ndani ya Rwanda na Tanzania.
Alisema
Rais Kagame anaunga mkono ujenzi wa reli itakayotumika kusafarisha
mizigo kwa kuwa ni njia mojawapo ya kukuza uchumi wa nchi hizo mbili
rafiki.
Akizungumzia
safari yake hiyo, Balozi Mahiga alisema, alienda nchini humo
kujadiliana masuala mbalimbali aliyoagizwa na Rais Magufuli kwa Rais wa
nchi hiyo, ambapo walijadili masuala matatu, ikiwemo machafuko
yanayoendelea Burundi.
Alisema
kuhusu machafuko ya Burundi, Rais Kagame alikanusha tuhuma zinazotolewa
na nchi hiyo pamoja na jumuiya za kimataifa kuwa anahusika katika
kuchochea machafuko hayo.
Kwa
mujibu wa Balozi Mahiga, maandamano ya nchi nzima yaliyofanyika wiki
iliyopita nchini Burundi ya kuishutumu Rwanda kuhusika na machafuko
nchini mwao, yalishitua nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC),
kutokana na baadhi ya maneno ya chuki yaliyokuwa yakitolewa na wananchi
hao dhidi ya nchi hiyo.
Alisema hali hiyo, ilihofiwa kwamba ingeweza kuvunja mazungumzo ya kutafuta suluhu yanayoendelea. “Nilimuuliza
Rais Kagame kuhusu hili suala, akasema hatachukua hatua yoyote licha ya
kwamba wananchi wake wamemlazimisha kufanya kitu."
Lakini alisema atashiriki katika majadiliano ya kutafuta suluhu ya Burundi.
“Sisi tulikuwa tunahofia kuwa huenda akachukua hatua ambazo zingeweza
kuleta matatizo na hata mazungumzo yanayoendelea kuvunjika, lakini
ameniambia hatachukua hatua yoyote inayoweza kusababisha kuvunjika kwa
uhusiano,” alisema Balozi Mahiga.
Hata
hivyo, alisema Rais Kagame alilalamikia nchi yake kushutumiwa kwa kutoa
mafunzo ya kijeshi kwa wakimbizi wa Burundi, ili kuipindua Serikali ya
nchi hiyo na kutaka Jumuiya za Kimataifa, kuwaondoa wakimbizi zaidi ya
70,000 na kuwahamishia nchi nyingine za jirani.
“Aliniambia
kuwa kuendelea kuwa na hawa wakimbizi katika nchi yake, kunaweza
kumletea matatizo makubwa, kwa sababu amekuwa akilaumiwa sana. Hivyo
kuliko lawama, ni bora hizi Jumuiya za Kimataifa zikawaondoa wakimbizi,” alisema.
Alisema
kwa mujibu wa Rais Kagame, Rwanda itaendelea kushiriki katika mijadala
mbalimbali ya kutafuta suluhu ya Burundi na itahakikisha Burundi inakuwa
salama.
Jambo
lingine walilozungumza na Rais Kagame ni mkutano wa marais wa Nchi za
Jumuiya ya Afrika Mashariki, unaotarajiwa kufanyika mwisho wa mwezi
nchini Tanzania, ambapo pia alikuwa katika hatua ya mwisho katika
kukamilisha ajenda na watakaoshiriki mkutano huo.
0 comments:
Post a Comment