Rais wa Uganda Yoweri Museveni
amesema uchaguzi uliofanyika nchini humo Alhamisi wiki iliyopita ulikuwa
wa haki na akasema wanaoutilia shaka “hawaielewi Uganda.”
Aidha, ametetea hatua ya maafisa wa usalama kumzuilia mgombea mkuu wa upinzani Dkt Kizza Besigye wa chama cha FDC.
Tume ya Uchaguzi ilisema Jumapili kwamba
Bw Museveni alipata ushindi wa asilimia 60.75 dhidi ya mpinzani wake wa karibu Dkt Besigye aliyepata asilimia 37.35.
Upinzani umedai kuwepo wizi wa kura na waangalizi wa kimataifa wamesema pia kwamba hakukuwa na nafasi sawa ya ushindani.
Waangalizi hao wamelalamikia kukamatwa na
kuzuiliwa kwa Dkt Besigye, kucheleweshwa kwa kufunguliwa kwa vituo vya kupigia kura na
kuzimwa kwa mitandao ya kijamii.
Mkuu wa waangalizi wa Jumuiya
ya Madola, Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo, alisema
matatizo mengi katika utaratibu wa uchaguzi yalitia dosari uaminifu na
uhaki wa shughuli nzima
Akizungumza na mwandishi wa BBC Zuhura Yunus, katika mahojiano maalum
Nyumbani kwake Rwakitura Magharibi mwa Uganda Museveni, Bw Museveni
alisema waangalizi hao hawaelewi vyema taifa la Uganda.
"Maafisa wa usalama walikuwa wengi kulinda usalama. Kwa sababu
walikuwa wanataka kufanya fujo. Wajua wapinzani wa hapa sio kama wa
Ulaya. Hawajaiva kisiasa. Usipokuwa mwangalifu wanaweza kuleta fujo
kabisa. Na sisi hatuwezi kukubali hivyo,” amesema.
Kuhusu
kukamatwa na baadaye kuzuiliwa kwa Dkt Besigye nyumbani kwake, Rais
Museveni alisema kiongozi huyo alikuwa amepanga kujitangazia matokeo
yake jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
"Walikuwa wanataka
kufanya fujo. Kwanza walikuwa wanataka kutangaza matokeo yao, wenyewe ya
uongo. Pili walitaka kufanya fujo za kuharibu mali,” amesema.
"Tulitaka
kuwawahi hawa wafanya fujo na ndio sababu polisi iliwazuia. Sasa
uchaguzi umekwisha, mipango yao tumeivunja, basi tunawaacha. Hatuna
shida nyingine nao.”
Bw Museveni ambaye sasa ana umri wa miaka 71
anatarajiwa kufikisha umri wa kustaafu wa miaka 75 akikaribia kumaliza
muhula wa sasa.
Amesema hana mipango ya kufanyia marekebisho katiba ili kuendelea kuongoza taifa hilo.
"Hakuna mpango wowote. Hatujazungumzia hilo. Lilikuja kwenye baraza la mawaziri tukasema hapana, hakuna haja ya kuongeza.”
Chanzao: BBC Swahili
0 comments:
Post a Comment