Mahakama ya rufani jana imeanza kusikiliza kesi ya viongozi wawili
waandamizi wa polisi, Kamishna mstaafu, Suleiman Kova na Kamishna
Msaidizi Mwandamizi, Godfrey Nzowa wanaogombea nyumba ya Serikali.
Katika
rufani hiyo, Nzowa anapinga uamuzi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha,
kumpa haki ya kumiliki nyumba ya Serikali, Kova ambaye ni mlalamikiwa wa
kwanza katika kesi hiyo. Mlalamikiwa wa pili ni Wakala wa Majengo ya
Serikali (TBA).
Nzowa anapinga nyumba ambayo anaishi hadi sasa,
iliyokuwa na namba 203 na baadaye kubadilisha kuwa namba 140 kuuziwa
Kova kwa kuwa wakati tangazo la kuuzwa nyumba za Serikali linatolewa
yeye ndiye alikuwa akiishi katika nyumba hiyo.
Hata hivyo, TBA ilimuuzia Kova ambaye alikuwa amehamishiwa mkoani Kigoma.
Tangazo
la kuuzwa nyumba hiyo, lilitolewa Mei Mosi, 2002, wakati Nzowa akiwa
katika nyumba hiyo baada ya kuhamia Arusha Januari 8, 2002.
Nzowa
ambaye ni Mkuu wa Kikosi cha Kuzuia Dawa za kulevya nchini na Kova
ambaye amestaafu karibuni akiwa Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar
es Salaam, waliwasili mahakamani jana saa tatu asubuhi.
Wa kwanza kufika alikuwa Kova akiwa anasindikizwa na watu kadhaa na baadaye Nzowa alifika akiwa ameongozana na familia yake.
Wakiwa
mahakamani kila mmoja alikaa eneo lake, akifuatilia mabishano ya
kisheria ya mawakili na baada ya shauri hilo kuahirishwa saa 6.25 mchana
walitoka nje ya chumba cha Mahakama, kila mmoja akishauriana na wakili
wake.
Pingamizi la rufani
Kabla ya kuanza kusikilizwa rufani
hiyo jana mbele ya majaji Mbarouk Salum, Benard Luanda na Mussa Kipenga,
mawakili wa wajibu rufani katika kesi hiyo, wanaowatetea Kova na TBA,
waliwasilisha pingamizi la kusikilizwa rufani hiyo kwa maelezo kuwa
liliwasilishwa nje ya muda na lina upungufu wa kisheria.
Mawakili
Dilip Kesaria na Pascal Qamala wanaomtetea Kamishna Kova na mawakili wa
Serikali, Harun Matagane na Sylvester Mwakitalu wanaowakilisha TBA
walieleza kuwa ni muhimu Mahakama ikaheshimu taratibu zake na
kuhakikisha nyaraka zinazowasilishwa mbele yake zipo sahihi.
Wakili
Kesaria alisema notisi ya kukata rufani ilitolewa Oktoba 3, 2013,
lakini rufani iliwasilishwa rasmi mahakamani Januari 2, 2015 nje ya muda
wa kisheria.
Mawakili hao wa walalamikiwa walieleza mkanganyiko
wa nyaraka zilizowasilishwa mahakamani na waliiomba mahakama kuitupa
rufani hiyo kwa kuwa ina upungufu ya kisheria.
Hata hivyo,
mawakili Mpaya Kamara na Neema Mtayangulwa walipinga hoja hiyo wakisema
hakuna dosari za kisheria katika uwasilishaji wa rufani hiyo.
Kamara alisema rufani na notisi vimefikishwa mahakamani ndani ya muda na ndiyo sababu Msajili wa Mahakama alivipokea.
Alisema
kama kulikuwa na upungufu katika nyaraka, wanaopaswa kulaumiwa siyo
wao, bali maofisa wa Mahakama waliopokea nyaraka za rufani na akatoa
vielelezo vya kesi kadhaa ambazo ziliendelea mahakamani licha ya kuwapo
dosari ndogo.
Kamala aliwaomba majaji kutupa hoja za wajibu
rufani na kama ikifikia uamuzi wa kulipa gharama za pingamizi hilo, basi
wajibu maombi wa pili ambao ni TBA ndiyo wanaopaswa kufanya hivyo.
Baada ya pande zote kuwasilisha hoja hizo, Jaji Mbarouk aliahirisha shauri hilo hadi hapo watakapomaliza kuzipitia.
0 comments:
Post a Comment