KAMPUNI
ya Simu Tanzania (TTCL) imekanusha taarifa zinazosambaa mitandaoni kuwa
mfumo wa mawasiliano wa kampuni hiyo umeingiliwa na wadukuzi.
Taarifa
iliyotolewa leo kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam na Meneja
Uhusiano wa kampuni hiyo, Nicodemus Thomas Mushi alisema taarifa
zinazotolewa si za kweli hivyo kuwataka wateja wao wazipuuze.
“Tunapenda
kuwathibithia Wateja wetu wote wa ndani na nje ya nchi, wadau wetu na
Umma kwa ujumla kwamba, taarifa hizi si sahihi, na kwamba mifumo yetu ya
Mawasiliano ya TTCL ipo salama, huduma zetu zote zipo thabiti na mpaka
sasa tunapotoa taarifa hii, hakuna uhalifu wowote uliofanyika kwa sisi
wenyewe kama Kampuni wala kwa mteja wetu yeyote,” alisema Thomas Mushi na kuongeza;
"Aidha,
tunapenda kuwathibitishia kuwa, taarifa za Wateja wetu wote ikiwemo
Serikali , Idara, Wakala na Taasisi za Umma, Taasisi za fedha,
Mashirika, Makampuni na Watu binafsi zipo salama kabisa. Ukweli huu
unathibitishwa na Wateja wao pia kwani hadi sasa, hakuna hata mmoja
aliyeleta taarifa za kukosa huduma ama kupata athari zozote kutokana na
tetesi hizo."
Hata
hivyo, alisema pamoja na taarifa hizo, Wataalamu wa kampuni hiyo
wanaendelea kuwa macho kwa muda wote, ili kuhakikisha kuwa, wanafanyia
kazi kila taarifa ama tishio la kiusalama linaloweza kujitokeza katika
mfumo wao.
“TTCL
inaendelea kuwaomba Umma na Wateja wetu wote kuendelea na majukumu yao
kama kawaida bila wasiwasi wowote. TCCL inawaleta Karibu.” Alisema Thomas Mushi.
Kwa
upande wake Meneja wa Kitengo cha Usalama Mifumo ya Mawasiliano ya
TTCL, Lina Rujweka alisema kitengo chao baada ya tetesi hizo kimefanya
uchunguzi wa kina na hakuna ashirio lolote la mifumo yao kuingiliwa
(kudukuliwa) kama ilivyoelezwa.
Alisema
kitengo hicho kina wataalam ambao muda wote wapo kazini kufuatilia
ufanisi wa mfumo wa mawasiliano wa kampuni yao hivyo kuwaondoa hofu
wateja wao.
“...
Baada ya taarifa hizo Kitengo cha Usalama wa Mifumo ya Mawasiliano ya
Kampuni ya TTCL kiliingia kazini ili kubaini ukweli wa taarifa hizo na
kufanya majaribio ya kitaalamu ili kuthibitisha usalama wa mifumo yetu.
Baada ya utafiti wa kina na majaribio ya kitaalamu, tunapenda
kuwathibithia Wateja wetu wote wa ndani na nje ya nchi, wadau wetu na
Umma kwa ujumla kwamba, taarifa hizi si sahihi...” alisema.
0 comments:
Post a Comment