Adverts

Friday, February 19, 2016

Waziri Wa Fedha Na Mipango Akutana Na Wabunge Kutoka Nchini Sweden


Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango akizungumzia vipaumbele vya Serikali wakati wa mkutano na Wabunge kutoka nchini Sweden jana jijini Dar es salaam kwa ziara ya kikazi nchini.
***
Waziriwa Fedha na Mipango,Mhe. Dkt. Philip Mpango amekutana na Wabunge wa Sweden katika ukumbi wa Wizara hiyo, kuzungumzia ushirikiano baina Tanzania na Sweden.

Katika mazungumzo yake na wabunge hao ambao wamewasili nchini kwa  ziara ya kikazi, Dkt. Mpango amesema Serikali ya Awamu ya Tano ipo makini na inafanyakazi kwa ufanisi ili kuhakikisha Watanzania wanapata huduma stahiki kutokana na rasilimali zilizopo nchini.

Amesema Serikali imejipanga kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato ya ndani ili kuiwezesha nchi kujiendesha yenyewe na kuacha kutegemea misaada ya wahisani.

Aidha, amefafanua kuwa Tanzania imejipanga kuongeza vyanzo vya ukusanyaji mapato pamoja na kuboresha  vyanzo vilivyopo na kuhakikishakila Mwananchi anayestahili kulipa kodi stahiki analipa kwa wakati.

“Ni aibu kwa nchi yenye rasilimali za kutosha Wananchi wake kuishi katika hali ya umasikini, tunachotakiwa ni kuboresha kilimo kwa sababu wananchi wengi ndicho wanachotegemea”, alisema.

Akizungumzia vipaumbele vya Serikali katika mkutano huo, Dkt. Mpango alisema mkazo umewekwa zaidi katika kufanya mapinduzi ya viwanda, ambapo nchi inaanza kuboresha viwanda vilivyopo hususani vile ambavyo hutumia rasilimali zinazopatikana nchini kama zile zinazotokana na kilimo.

Aliongeza kuwa katika kuboresha viwanda pia Serikali ipo katika hatua za kuboresha soko la ndani na nje ya nchi kwa bidhaa zinazozalishwa na viwanda hivyo.

Dkt. Mpango alisema sambamba na kufanya mapinduzi ya viwanda, Tanzania imejipanga kuboresha miundombinu ambapo mpaka sasa kuna miradi mbalimbali ya maendeleo imeanzishwa kama mradi wa umeme vijijini.

Alisema katika suala la umeme, nchi imeazimia kujikita katika uzalishaji wa kutumia vyanzo vingine kama gesi asilia, jua na upepo kuliko kutegemea maji pekee.


 
Kuhusu sekta ya usafirishaji, Dkt. Mpango amesema Serikali imejipanga kuboresha bandari zote nchini na kuzifanya ziwe za kisasa ili kuhamasisha biashara za ndani na nje ya nchi kupitia bandari hizo.

Hata hivyo, Dkt. Mpango alikiri kuwa uboreshaji wa reli ya kati ni changamoto kwani reli hiyo haiwezi kuboreshwa kwa kutumia fedha za bajeti ya Serikali pekee, hivyo Serikali inajitahidi kutafuta njia za kufanikisha ujenzi huo.

Katika mkutano huo, Dkt. Mpango alizungumzia suala la huduma za kijamii alisema, nchi imejipanga kutoa elimu inayoendana na soko la ajira na Serikali imeanza kutoa elimu ya msingi na sekondari bila malipo ili kuwawezesha wananchi wengi kupata elimu.

Akizungumzia suala la uchumi, Dkt. Mpango alisema hali ya uchumi kwa sasa ni nzuri kwani pato la ndani la Taifa limefika asilimia 7 katika miaka ya hivi karibuni.

Dkt. Mpango alisema ili kufanikisha vipaumbele hivyo, ni lazima maadili na nidhamu ya kazi vifuatwe na watendaji pamoja na watumishi wa umma katika utekelezaji wa majukumu yao.

Aliongeza kuwa Serikali ipo msatari wa mbele kupambana na rushwa na haitosita kuhakikisha watu wote wanaohusika na rushwa wanachukuliwa hatua za kisheria.

Kwa upande  Wabunge kutoka nchini Sweden, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje, Kenneth Forslund, wameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa jitihada mbalimbali zinazochukuliwa katika ukusanyaji wa  mapato ya ndani na kutoa huduma za kijamii.

Tanzania na Sweden zimekuwa na ushirikiano wa muda mrefu ambao umeifaidisha Tanzania katika shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo kuendeleza miradi ya afya na umeme hususani vijijini, elimu pamoja na kusaidia kukamilisha bajeti ya kila mwaka.

Imetollewa na Msemaji
Wizara ya Fedha na Mipango
Kitengo cha Habari
19.2.2016

0 comments:

Post a Comment