Adverts

Wednesday, March 16, 2016

Waziri Kitwanga Afanya Mazungumzo Na Wakuu Wa Vyombo Vya Ulinzi Na Usalama Zanzibar....Akanusha Wazanzibar Kukimbilia Nchi Jirani Kwa Kuogopa Vurugu


WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga amewataka wananchi wa visiwani Zanzibar kujitokeza kwa wingi Machi 20, 2016 ili waweze kupiga kura kwa amani na utulivu bila kubughudhiwa na mtu yeyote.
 
Kitwanga amesema kuwa ulinzi umeimarishwa na kuwataka wananchi visiwani humo kujitokeza kwa wingi kuja kumchagua kiongozi wanaompenda siku ya uchaguzi huo na watarejea nyumbani kwao salama mara baada ya kumaliza kupiga kura.
 
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza mazungumzo na Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi Makao Makuu ya Polisi Zanzibar na baadaye kuzungumza na Wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama, Waziri Kitwanga alisisitiza kuwa, vyombo vya ulinzi na usalama vimejiandaa vizuri na wananchi waondoe shaka kwani hawatakubali vurugu ya aina yoyote itokee.
 
“Jitokezeni kupiga kura siku ya uchaguzi kwani ni haki yenu, nawahakikishia usalama upo na wa hali ya juu, asijitokeze mtu yeyote akawatisha kutokuja kupiga kura, tumejipanga vizuri na lengo letu kubwa kabisa ni kuwalinda wananchi,” alisema Kitwanga.
 
Hata hivyo Waziri Kitwanga alisema hakuna mwananchi yeyote anayehama kwakuogopa vurugu siku ya uchaguzi bali watu wanasafiri kwasababu mbalimbali ikiwemo hiki ni kipindi cha maandalizi ya Sikukuu ya Pasaka, baadhi ya wananchi wanaenda kula sikukuu maeneo mbalimbali nchini na wengine wanasafiri kutokana na majukumu mbalimbali na sio wamekuwa wakimbizi wakikimbia sehemu zao kama inavyoenezwa.
 
“Acheni kusikia habari za mitaani amani ipo, jitokezi kupiga kura na hii habari mnayosikia eti watu wameanza kuyakimbia makazi yao ni uzushi tu, hakuna kitu kama hicho, wananchi wanaendelea na shughuli zako kama kawaida na vyombo vya ulinzi vimejipanga kwa ajili ya kulinda usalama wa raia na mali zao,” alisema Kitwanga.
 
Waziri Kitwanga aliwasili Zanzibar jana kwa ajili ya ziara ya kikazi ya kuimarisha usalama  zaidi visiwani humo pamoja na kujua mikakati iliyowekwa na vyombo vya ulinzi na usalama kuhusu usimamizi wa uchaguzi huo.

0 comments:

Post a Comment