Mvua
kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia juzi imeleta athari kubwa katika
Kijiji cha Chenene Kata ya Haneti Tarafa ya Itiso, Wilaya ya Chamwino
mkoani Dodoma na kukosesha makazi zaidi ya kaya 40.
Akizungumza
jana, Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Farida Mgomi alisema nyumba nyingi
zilizobomoka ni zile zilizojengwa kwa matofali ya udongo. Mgomi alisema
athari hiyo inaweza kuongezeka kutokana na nyumba kujaa maji na
zinaposhindwa kuhimili hudondoka.
“Nyumba nyingi zilijaa maji, kwa hiyo hata chakula, magodoro, nguo vyote vimeharibika,” alisema.
Mgomi alisema tathmini ya awali tayari imefanyika. Na hakuna mtu aliyefariki dunia kufuatia maafa hayo.
“Waathirika
wote ambao nyumba zao zimeanguka tayari wamepata sehemu za kujihifadhi
kwa msaada mkubwa majirani na kutoka viongozi wa Serikali ngazi ya
Kijiji, Kata, Tarafa na Wilaya,” alisema mkuu wa wilaya.
Alisema
Kamati ya Maafa ya Wilaya tayari imechukua na inaendelea kuchukua hatua
za haraka,kuona namna ya kusaidia familia zilizoathiriwa na maafa hayo
kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Pia alisema hata baadhi ya mashamba (mazao) yamesombwa na maji.
“Baadhi
ya wananchi wamepoteza mali zao hifadhi za chakula katika kaya zao,
mabati, vyombo vya ndani na mali nyingine za namna hiyo,” alisema.
Naye Ofisa Tarafa wa Itiso, Remidius Emmanuel alisema mvua hiyo imeacha kaya zikiwa hazina makazi.
“Kaya zaidi ya 40 zimeathirika, nyumba nyingi zilizodondoka ni zile zilizojengwa kwa matofali ya udongo,” alisema Emmanuel na kuongeza kuwa nyumba nyingi zilibomoka kutokana na kujaa maji kutoka milimani.
Pia
ujenzi wa barabara ya Kondoa hadi Babati umeonesha kuathiri miundombinu
kwani madaraja yaliyojengwa ni madogo yanashindwa kuhimili wingi wa
maji kutoka milimani
“Katika
eneo la Chenene ujenzi wa barabara unaonekana kuleta athari kwa makazi
ya wananchi kwani madaraja ni madogo, maji yanapofika kwenye barabara
yanakosa mwelekeo na kurudi kwenye makazi ya watu hali hiyo ikapelekea
nyumba kubomoka,” alisema Ofisa Tarafa huyo.
“Nimetembelea maeneo yote yaliyokumbwa na maafa hayo. Nimekutana na kuzungumza na waathirika wote,” aliongeza.
0 comments:
Post a Comment