Adverts

Saturday, October 1, 2016

Mbarawa ataka ujenzi Flyover ya TAZARA uharakishwe

Serikali imeitaka Kampuni ya kikandarasi ya Sumitomo Mitsui inayojenga mradi wa ujenzi wa barabara ya juu (Flyover) katika makutano ya barabara ya Nyerere na Mandela eneo la Tazara kumaliza ujenzi huo kwa wakati

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ndiye aliyetoa agizo hilo na kusema kuwa mradi huo ni muhimu ili kusaidia kupunguza tatizo la msongamano.

Akizungumza mara baada kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo jijini Dar es salaam, Profesa Mbarawa amesema kuwa kukamilika kwa mradi huo kutajenga historia nchini kutokana na kuwa ni wa mwanzo kujengwa.

“Nimefurahi kuona mradi huu upo katika hatua nzuri, naomba mkamilishe mradi huu unakamilika kwa ubora na kwa wakati ili tatizo la msongamano lililopo katika maeneo haya kupungua au kuisha kabisa”, amesema Waziri Mbarawa.

Aidha, Waziri Mbarawa amewataka wananchi wa maeneo hayo kutoa ushirikiano kwa Mkandarasi huyo ili kurahisisha kazi za ujenzi huo kukamilika kwa wakati na kupata matokeo chanya.

“Nawaomba watanzania wenzangu kuwa wavumilivu na usumbufu wowote utakaojitokeza katika kipindi hiki chote, kwani ukamilifu wa mradi huu utasaidia kupunguza tatizo la msongamano katika barabara hizi”, amefafanua Waziri Mbarawa.

Katika hatua nyingine, Profesa Mbarawa amekagua daraja la watembea kwa miguu eneo la Buguruni Sheli na kuwataka wananchi wa maeneo hayo kulitunza daraja hilo ambalo uwepo wake umesaidia kupunguza ajali katika maeneo hayo.

“Ni matumaini yangu sasa wakazi wa maeneo haya mtavuka kwa amani kupitia daraja hili, na ajali zilizokuwa zikitokea maramara hazitakuwepo tena”’, amesema Profesa Mbarawa.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Eng. Patrick Mfugale amemuahidi Waziri huyo kumaliza kwa wakati ujenzi huo na kumhaakikishia Waziri kuwa ujenzi wa barabara hiyo utakuwa na viwango vilivyo bora.

Mradi wa Tazara Flyover ni msaada kutoka Serikali ya Japan ambao umegharimu shilingi bilioni 93.4 na unatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba mwaka 2018

0 comments:

Post a Comment