Adverts

Friday, October 7, 2016

Serikali Yachachamaa....Walimu Waliomfanyia Ukatili Mwanafunzi Watimuliwa Chuoni, Mkuu wa Shule Apoteza Kibarua

 
Walimu  wanne wa Chuo Kikuu cha Elimu Dar es Salaam (Duce) na cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere waliohusika kumpiga vibaya mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Mbeya wamefukuzwa chuo huku Jeshi la Polisi mkoani Mbeya likiwashikilia kwa mahojiano walimu wengine watano wa shule hiyo kutokana na tukio hilo.

Aidha, serikali imemvua madaraka Mkuu wa shule hiyo, Magreth Haule kwa kutochukua hatua baada ya kitendo hicho kufanyika shuleni hapo Septemba 28, mwaka huu.

Hatua hizo zimechukuliwa baada ya jana katika mitandao ya kijamii kusambaa kipande cha video kikionesha walimu zaidi ya watatu wakiwa eneo la ofisi wakimshambulia kwa kumpiga makofi, mateke na fimbo sehemu mbalimbali za mwili hasa kichwani mwanafunzi Sebastian Chinguku.

Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako ametangaza kuwafukuza chuo walimu wanafunzi hao walioshiriki kitendo cha kumpiga mwanafunzi huyo wa kidato cha tatu wa Shule ya kutwa ya Sekondari ya Mbeya.

Walimu hao ni Frank Msigwa (anayedaiwa kumpiga zaidi mwanafunzi huyo kwa makofi kichwani), John Deo na Sante Gwamaka wote wa Duce na Evans Sanga wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.

Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana, Profesa Ndalichako alisema kitendo hicho ni cha kikatili, jinai na kuwa walimu hao wanafunzi hawafai kuendelea na taaluma hiyo ya ualimu na kuwa hatua zaidi za kisheria zinaendelea kuchukuliwa dhidi yao.

Profesa Ndalichako alisema kwa mujibu wa taratibu za vyuo vikuu kitendo kilichofanywa na walimu wanafunzi hao ni kosa la jinai na kuwa hakiwezi kufumbiwa macho.

Alitoa onyo kali kwa wanafunzi wanaokwenda kwenye mafunzo kwa vitendo na kwenda kinyume cha taaluma yao kuwa wanapoteza sifa hivyo amewataka kuzingatia maadili ya fani na taaluma wanazosomea.

Mkoani Mbeya, Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Dhahiri Kidavashari alisema wanawashikilia walimu wa shule hiyo watano kwa mahojiano kuhusu tukio hilo. Hata hivyo, alisema si kwamba walimu hao wanaohojiwa ndio waliohusika na tukio hilo bali wameanza na wale waliopo ili kupata taarifa zaidi.

“Hatuwezi kusema sasa hivi kama wale walimu ndio walioonekana katika kipande cha video kinachosambaa mitandaoni kwa kuwa hili ni suala la mahojiano, tunaamini hawa tulionao wanaweza wakatupa mwanga,” alisema.

Akieleza sababu ya adhabu hiyo, Kamanda alisema katika mahojiano ya awali imebainika kuwa mwalimu wa Kiingereza alitoa kazi, lakini baadhi ya wanafunzi hawakufanya baadaye mwalimu huyo aliwapa adhabu ya kupiga magoti, lakini mwanafunzi huyo alionekana kupinga kwa kueleza ana tatizo la goti hatoweza kufanya adhabu hiyo na mwalimu aliamua kumpeleka ofisini na kumpiga kwa kumchangia.

“Mwalimu aliwaadhibu wanafunzi darasani na alipotaka kumuadhibu mwanafunzi huyo mbele ya darasa, alionesha kupinga kupigwa mbele ya wanafunzi wenzake ndipo alipoamua kumpeleka ofisini na kutokea tukio linalosambaa,” aliongeza Kidavashari.

Katika taarifa yake, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, alisema Septemba 28 mwaka huu, mwanafunzi Chinguku wa kidato cha tatu wa Shule ya Sekondari Mbeya, mkazi wa Uyole, alipigwa na walimu watatu.

“Nimeelekeza vyombo vya dola Dar es Salaam wawatafute chuoni kwao hao walimu kuhusiana na shambulio hilo kwa mwanafunzi huyo,” ilisema Mwigulu.

Naye Waziri katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene ameagiza mamlaka za nidhamu kumvua madaraka Mkuu wa Shule hiyo, Haule kwa kushindwa kuchukua hatua na kutoa taarifa mara baada ya tukio hilo kufanywa na walimu hao shuleni hapo.

"Kwa kuwa waliotenda kosa hili wametoweka tangu Septemba 29, 2016 na hawajulikani walipo, nimesikitishwa kwa kitendo cha mwalimu mkuu wa shule hiyo, Magreth Haule kutochukua hatua. Hii inaonesha kulikuwa na dalili za kutaka kulificha tukio hili baya.

“Na kwa sababu hiyo, pamoja na kwamba wanaendelea kuhojiwa na Polisi, naagiza mamlaka yake ya nidhamu kumvua madaraka mkuu huyo wa shule," alisema Simbachawene katika taarifa yake kwa umma jana.
 Katika hatua nyingine, Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba amelaani kitendo kilichofanywa na walimu hao na kukieleza kuwa ni cha mwituni na cha kinyama kwa kuwa hakuna adhabu kama hiyo katika utumishi wa ualimu.

"Nami nimeona hiyo video katika mitandao ya kijamii, kuna sheria za adhabu za viboko lakini si hii walioifanya hao walimu vijana maana walikuwa wakipiga makofi, ngumi, mateke, ngwara. Hizi hazipo kwenye ualimu, lazima wafuate sheria zinazosimamia utumishi wa walimu," alisema Mukoba.

Alishauri vyuo vya ualimu viweke mkazo katika kufundisha walimu vijana namna ya kuwa zaidi ya walimu, kuwa na uvumilivu, subira na kuzingatia sheria. Wafunzwe kisaikolojia kukubali kuwa hawaishii kuwa walimu bali wanaingia kwenye kundi la malezi.

Alisema kwa tukio hilo, ni lazima sheria ichukue mkondo wake ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia hizo hasa walimu vijana kwa kuwa kitaaluma ni tukio la kinyama lisilokubalika.

“Hata kama mwanafunzi ana makosa, amevuta bangi, huwezi kumuadhibu vile, maana pale hujui nani kavuta bangi nani mzima,” alisema Mukoba.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla alisema serikali inalifuatilia kwa karibu tukio la kupigwa kama mwizi mwanafunzi huyo wa shule hiyo ya jijini Mbeya na kusema tayari baadhi ya walimu akiwemo mkuu wa shule, wanashikiliwa na Polisi.

Makalla alibainisha hayo jana kwenye Maadhimisho ya Siku ya Fimbo Nyeupe Duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani Mbeya na kusisitiza kuwa walimu waliohusika na tukio la kumpiga mwanafunzi wao kama mwizi wanasakwa na lazima watapatikana.

Alisema Septemba 26, mwaka huu, mwalimu aliyekuwa katika mafunzo kwa vitendo katika shule ya Sekondari ya Mbeya Day aliyemtaja kwa jina la Frank Msigwa alitoa kazi kwa wanafunzi darasani na Septemba 28 alipokuwa akisahihisha kazi zilizofanyika alibaini baadhi ya wanafunzi hawakufanya.

Makalla alifafanua kuwa miongoni mwa wanafunzi aliobaini hawakufanya kazi yake ni pamoja na Chinguku na ndipo aliwatoa nje ya darasa na kuwapa adhabu ya kupiga 'push up' lakini mwanafunzi huyo akagoma akidai kuwa na matatizo ya kiafya katika mbavu zake.

Alisema baada ya kugomea adhabu hiyo mwalimu aliwaamuru wapige magoti lakini pia mwanafunzi huyo aligoma akisema ana matatizo ya goti katika moja ya miguu yake ndipo mwalimu alilazimika kutoa adhabu ya kuwachapa viboko viwili kila mmoja na aliwapiga wote isipokuwa Chunguku ambaye kama alivyofanya kwenye adhabu za kwanza hii pia alikataa.

Alisema baada ya hapo mwalimu huyo alilazimika kwenda kuwaita wenzake wawili ambao nao walikuwa kwenye mafunzo ya ualimu kwa vitendo shuleni hapo na wakambeba mwanafunzi huyo hadi ofisini kwao ambako huko ndiko walianza kumchapa kwa kumchangia kama inavyooneshwa kwenye kipande cha video kilichosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

Kwa mujibu wa Makalla, walimu waliotenda kitendo hicho walitoroka na hawajulikani walipo. Alisema serikali inaendelea kuwasaka huku walimu wengine wakihojiwa Polisi.
 
Click hapa kuona video
 

0 comments:

Post a Comment