Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ametoa siku 18 kwa uongozi wa Manispaa ya Ilala kuvunja jengo la ghorofa 16 lililopo katika Mtaa wa Indira Gandhi kabla halijaleta maafa.
Akizungumza
jana katika jengo hilo, Lukuvi alisema anashangaa hadi sasa kazi ya
kuvunja jengo hilo haijaanza licha ya manispaa kuelekezwa kulivunja.
Uamuzi
wa Serikali kulivunja ulikuja baada kuporomoka kwa jengo katika mtaa
huo lililosababisha vifo vya watu 37 na wengine 18 kujeruhiwa mwaka
2013.
“Ni aibu, manispaa mnataka jengo hilo liporomoke na kuua watu tena! Tutachekwa kwa uzembe kama ikitokea tena ajali,” alisema.
Lukuvi alisema kuanzia Februari Mosi uvunjaji wa jengo hilo unatakiwa kuanza vinginevyo wahusika wajiandae kuchukuliwa hatua.
“Nataka nikipita hapa siku yoyote kuanzia mwezi ujao nikute mkandarasi anabomoa jengo hili vinginevyo hatutaelewana,” alisema.
“Hili
ni eneo hatarishi hata tuliosimama hapa hatari yoyote inaweza kutukuta
lakini Manispaa ya Ilala haioni kwamba hapa kuna tatizo,” alisema.
Waziri alisema uvunjaji wa jengo hilo utakapoanza, wananchi wanaoishi jirani watatakiwa kuhama kwa muda kwa tahadhari.
“Mkuu
wa Wilaya ya Ilala, wakianza kuvunja jengo hilo tafadhali waondoeni
wakazi wote kwa sababu eneo hili litakuwa hatarishi,” alisema.
Jengo hilo linamilikiwa kwa pamoja kati ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na Ali Raza Investment.
Mkurugenzi
wa Manispaa ya Ilala, Isaya Mngulumi alisema kilichochelewesha ni
makandarasi walioshinda zabuni hiyo kujitoa katika hatua za mwisho
wakitoa sababu mbalimbali.
Alisema hivi sasa amepatikana mkandarasi Patty Interplan ambaye yuko katika hatua za mwisho za kupewa kazi hiyo.
“Tutaanza kazi kama ulivyoelekeza,” alisema Mngulumi.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Raymond Mushi, alisema atatoa ushirikiano kwa manispaa hiyo ili kuhakikisha jengo hilo linabomolewa.
0 comments:
Post a Comment