AGIZO la Rais John Magufuli la kuibadilisha jengo la maofisa wa
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto lililopo
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, limetelekezwa baada ya jana maofisa hao
kuondoa vifaa vyao.
Tangu jana asubuhi maofisa wa wizara hiyo Kitengo cha Afya ya Uzazi
na Watoto wakiongozwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Mpoki Ulisubisya
walikuwa wakiondoa vifaa na kupakia kwenye magari.
“Ikifika jioni vifaa vyote vitakuwa vimeondolea ndani na katika eneo
hili,” alisema Ulisubisya na kueleza kuwa ofisi hizo zitahamia wizarani
Barabara ya Sokoine jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya kukagua uondokaji wa maofisa hayo, Waziri Ummy
Mwalimu alisema agizo la Rais limetekelezwa na kusisitiza kuwa hakuna
mgonjwa atakayelala chini.
Alisema pamoja na kuwa kazi ya kulipangia matumizi jengo hilo ni ya
uongozi wa Muhimbili, uongozi wake utasimamia kuhakikisha jengo hilo
lenye ghorofa tatu linatumika kama wodi katika kupunguza msongamono
katika wodi ya wazazi.
Mwalimu alisema baada ya kuhamishwa maofisa hao, kinachofuata ni
kufanya ukarabati wa kuongeza vyoo na mabafu ili yaendane na viwango vya
wodi inavyotakiwa na baadaye kuwekwa vitanda takribani 300.
Akitoa maelezo kwa Waziri, Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili, Profesa Lawrence Museru alisema katika kutatua tatizo hilo
kwa muda wameamua kutumia ghorofa ya chini, ambayo ilikuwa ikitumika
kama kliniki ya wajawazito na watoto chini ya siku 30 na kuweka vitanda
kwa ajili ya wagonjwa 50.
“Mpaka leo (jana) tulikuwa na wagonjwa 50 waliokuwa wamelala chini,
hivyo tumeamua kutumia eneo lililokuwa likitumiwa kama kliniki kuwa wodi
kwasababu ya kuwa na vyoo na mabafu. Baada ya maofisa wa wizara
kuondoka, eneo la chini la jengo la ghorofa tatu litatumika kama
kliniki,” alisema Profesa Museru.
Naye Asha Twalib aliyekuwapo hospitalini hapo kumuona mgonjwa wake,
alipongeza juhudi za Rais Magufuli katika kuboresha sekta ya afya
nchini.
Rais Magufuli ambaye alisimamishwa na akina mama hospitalini hapo na
kutembelea wodi ya wazazi wiki iliyopita, alitoa siku mbili kwa maofisa
70 wa wizara Kitengo cha afya ya Uzazi na Mtoto kuhama katika jengo hilo
na kuhamishia wazazi ili kila mzazi apate kitanda cha kulala.
“Nimeshatoa agizo lile jengo la ofisi la uzazi ndani ya siku mbili
wahame...wakiweza wakakae na Waziri (Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto).
“Ndani ya siku mbili hizo hizo, pawe na
vitanda na wale akinamama (wajawazito wanaolala watano kitanda kimoja),
wahamishiwe kule,” alisema Rais Magufuli alipozungumza na Taifa juzi
kupitia kwa wazee wa Dar es Salaam kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee
akitimiza siku 100 tangu aingie Ikulu ya Magogoni.
0 comments:
Post a Comment