Rais John Magufuli jana alitumia dakika 55 kuzungumza na wazee wa Dar es
Salaam, akigusa kila sekta wakati akizungumzia mambo aliyoyafanya
katika siku 100 na anayotarajia kufanya.
Katika hotuba hiyo ambayo aliendelea kuzungumzia jinsi nchi inavyotafunwa, kiongozi huyo wa Serikali ya Awamu ya Tano aliweka msimamo wake kuhusu mgogoro wa kisiasa Zanzibar, akisema hataingilia.
Pia alidokeza kuhusu
uteuzi wa wakuu wa mikoa na wilaya, akimhakikishia Mkuu wa Wilaya ya
Kinondoni, Paul Makonda kuendelea au kupandishwa cheo.
Mambo
mengine aliyozungumzia ni mafanikio na changamoto ya elimu bure, ujenzi
wa barabara na madaraja, utendaji wa mawaziri, miradi ya umeme, huduma
kwenye Hospitali ya Muhimbili, vyombo vya habari, na kuwataka wananchi
wajitathmini wamefanya nini katika siku 100 za kwanza za utawala wake.
Dk
Magufuli aliyekuwa ameambatana na Makamu wa Rais, Samia Suluhu, Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa, Naibu Spika Dk Tulia Ackson, alikuwa akizungumza
na baraza la wazee wa Dar es Salaam kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee,
ikiwa ni siku yake ya 102 tangu alipoapishwa Novemba 5, 2015 kuwa Rais.
Mkutano
huo ulihudhuriwa na watu zaidi 3,000, wakiwamo mawaziri, viongozi wa
CCM na viongozi wa dini, walioongozwa na Sheikh wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Alhaj Mussa Salum na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima,
Josephat Gwajima.
Rais Magufuli aliyeingia katika ukumbi huo saa
8:30 mchana, alianza kuzungumza saa 9:36 alasiri na kumaliza saa 10:32
jioni, akisisitiza wananchi wamuombee aweze kutekeleza majukumu yake,
ikiwa ni pamoja na kutumbua majipu.
Uchaguzi Zanzibar
Rais ambaye amekuwa kimya
kwa muda mrefu kuhusu mgogoro wa kisiasa Zanzibar, hatimaye jana aliweka
bayana msimamo wake akisema hataingilia kwa kuwa anaheshimu utawala wa
sheria.
“Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ni huru kwa mujibu
wa Kat iba ya Zanzibar kifungu kati ya 112 au 115. Lakini kama ilivyo
kawaida Tume huru ya uchaguzi duniani haiwezi kuingiliwa na rais yoyote.
Ni kama ilivyo ZEC na (Tume ya Taifa ya Uchaguzi) NEC ndivyo ilivyo,”
alisema Rais.
Alisema uamuzi wa ZEC kufuta uchaguzi Zanzibar na
kisha kutangaza tarehe ya marudio, hauwezi kuingiliwa na mtu yeyote,
akisisitiza kuwa wanaotaka tafsiri ya kisheria juu ya uamuzi wa ZEC,
waende mahakamani.
“Mahakama ipo hutaki kwenda halafu unasema Magufuli ingilia! Nenda
mahakamani ukapewe tafsiri ya haki. Siingilii na nitaendelea kukaa
kimya. Jukumu langu ni kuhakikisha usalama wa Zanzibar, Pemba na
Tanzania unaimarika,” alisema.
“Ukifanya “fyokofyoko” katika eneo lolote nchini, utashughulikiwa na vyombo vya ulinzi na usalama.”
Mgogoro
wa kisiasa Zanzibar uliibuka baada ya ZEC kufuta matokeo ya uchaguzi wa
rais, wawakilishi na madiwani kwa maelezo kuwa sheria na kanuni
zilikiukwa na baadaye kutangaza Machi 20 kuwa siku ya kupiga kura upya.
Wakati
mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha akitangaza kufuta matokeo siku
ambayo alitakiwa amtangaze mshindi wa kiti cha urais, tayari matokeo ya
majimbo 31 yalikuwa yameshatangazwa huku majimbo tisa yakiwa
yameshahakikiwa. Pia washindi wa viti vya uwakilishi na udiwani
walishatangazwa na kupewe hati za ushindi.
Chama kikuu cha
upinzani Zanzibar, kimepinga ZEC kufuta matokeo kikisema ni kukiuka
katiba kwa kuwa ushindi unapingwa mahakamani tu na kimejitoa kwenye
uchaguzi wa marudio huku kikimtaka Rais Magufuli aingilie katika kutatua
mgogoro huo mezani.
“Sitaingia suala la Zanzibar,” alisema Magufuli.
Akizungumzia
mabadiliko ambayo Serikali yake inayafanya, Rais alisema yana
changamoto zake ambazo zinaweza kuwagusa baadhi ya watu, lakini akasema
watakaoguswa ni wachache kwa faida ya wengi.
“Tanzania haitakiwi
kuwa na wanafunzi wanaokaa chini, watu kukosa maji, Muhimbili watu
kulala watano kitandani. Tanzania hii ina neema ila lazima tutambue wapo
watu wachache waliotufikisha hapa,” alisema.
Alisema mabilioni ya fedha za Watanzania yanatumika hovyo.
“Ifike
mahali Watanzania tujiulize tumemkosea nini Mungu? kwa nini asitusamehe
kwa makosa tuliyoyafanya. Serikali imejitoa sadaka kwa ajili ya
Watanzania,” alisema.
“Ndani ya Serikali tumejipanga, anayetaka
kutukwamisha tutambomoa kwa faida ya Watanzania, hasa wanyonge.
Haiwezekani kila mahali unapokwenda ukute wananchi wanalia wakati nchi
ina rasilimali za kila aina.”
Ufisadi
Katika hotuba yake ambayo
mara kwa mara alikuwa ikikatishwa na shangwe za wananchi, Dk Magufuli
alianza kuzungumzia ufisadi, akisema katika siku 100 ambazo amekaa
madarakani, wamejifunza mengi na kukumbana na changamoto lukuki.
“Wapo
watu katika nchi hii kwao fedha sio tatizo, fedha hizo hawajazipata kwa
uhalali wamezipata kutoka kwa masikini wanaohangaika . Kila tulipokuwa
tunagusa kuna maajabu,” alisema
Alisema alimtuma Majaliwa kwenda
bandarini na Katibu Mkuu wa Tamisemi kwenda wilayani Bariadi na
wakakumbana na madudu.
“Akiwa Bariadi alikuta barabara ya
kilomita moja imejengwa kwa Sh2 bilioni tena ni barabara ya halmashauri
ya wilaya. Mimi nimekaa Serikalini sijawahi kujenga barabara kuu ya
kilomita moja kwa Sh2 bilioni, ila hii ya halmashauri imejengwa kwa
kiasi hicho?” alihoji.
“Barabara ya kilomita nne na nusu ya
Halmashauri ya Bariadi imejengwa kwa Sh9.2 bilioni, wakati mkuu wa mkoa,
wilaya, mkurugenzi na mhandisi yupo.
“Ninapozungumza kutumbua majibu,
Watanzania mtuunge mkono tuyatumbue kwelikweli.”
Alisema kiwango hicho cha fedha kingeweza kutengeneza kilomita 22 hadi 23 za lami.
Wizi
bandarini
Akizungumzia wizi wa mafuta bandarini alieleza kushangazwa na
kitendo cha mita za mafuta kutofanya kazi kwa miaka mitano.
“Waziri Mkuu alikwenda bandarini na kukuta flow meter ya kupimia mafuta yanayoingia nchini haifanyi kazi kwa miaka mitano,” alisema.
“Mafuta
yanaingia nchini yanagawiwa kwa watu na ndiyo maana mnaona kutoka Dar
es Salaam kwenda Kibaha kila mahali kuna sheli (vituo vya mafuta).”
Kutokana
na wizi huo wa mafuta, juzi Majaliwa alimsimamisha kazi mtendaji mkuu
wa Wakala wa Vipimo (WMA) na meneja wake wa kitengo cha bandari kupisha
uchunguzi.
Alisema fedha ambazo zingepatikana kama mafuta hayo
yangepimwa na kulipiwa kodi zingeweza kutumika kununua dawa hospitali,
kusomesha wanafunzi bure na kujenga barabara.
“ Hiyo ndiyo Tanzania tuliyoikuta sisi. Mifano ni mingi ya kila aina,”alisema.
Madudu muhimbili
Alisema alitembelea Muhimbili na kusimamishwa na
akinamama waliomtaka aende wodi ya wanawake, lakini wasaidizi wake
wakamzuia.
“Walinizuia ila nilikataa. Niliwambia naenda hukohuko na niliyoyakuta ni maajabu,” alisema.
Alisema
katika wodi namba 36, alikuta maji kutoka chooni yanavuja huku akina
mama wakiwa wamelala chini, watano kwenye godoro moja.
“Ukiwa
unaenda Muhimbili jirani kuna jengo la ghorofa tatu, linatumika kama
ofisi ya uzazi na watoto. kuna wafanyakazi 70. Ukisogea mbele zaidi kuna
jengo lilianza kujengwa tangu utawala wa Serikali ya Awamu ya Pili
mpaka leo halijaisha,” alisema.
“(Rais wa Serikali ya Awamu ya
Pili, Ali Hassan) Mwinyi hakulimaliza, akaja (wa Awamu ya Tatu,
Benjamin) Mkapa hakulimaliza, akaja (wa Awamu ya Nne, Jakaya) Kikwete hakulimaliza na sasa nipo mimi bado halijaisha.”
Alisema
inashangaza kuona viongozi wa hospitali hiyo wakishindwa kumfukuza
mkandarasi anayejenga jengo hilo ambaye ni Masasi Construction
Engineering .
Alisema alipokuwa Waziri wa Ujenzi alifukuza
makandarasi 3,000, lakini akashangazwa kuona jengo la ghorofa nne
likijengwa zaidi ya miaka 20.
“Nadhani jengo hili limeweka rekodi duniani,” alisema.
Alisema
jengo hilo likimalizika linaweza kuchukua watu 342, lakini hivi sasa
lina watu 100, waliopo eneo la chini la ghorofa hilo, halina umeme wala
maji.
Alisema Muhimbili kuna jengo la Taasisi ya Tiba ya Mifupa
ya Muhimbili (Moi), kuna jengo la ghorofa sita lililoanza kujengwa miaka
minne iliyopita, lakini mpaka leo halijamalizika kutokana na mvutano
kati ya Moi na mkandarasi anayetaka kulipwa Sh9 bilioni.
“Wamechukua
wagonjwa wachache na kuwaweka ghorofa ya kwanza hadi ya tatu. Lina
jenereta ila haijafungwa. Hiyo ndiyo Tanzania,” alisema.
Alisema
ameshatoa maagizo kwamba ndani ya siku mbili wafanyakazi hao 70
waondolewe kwenye jengo hilo linalotumika kama ofisi na badala yake
viwekwe vitanda vya wagonjwa.
“Sasa Waziri wa Afya na Katibu Mkuu
watajua watawatafutia wapi pa kuwapeleka. Wanaweza kuwapeleka pale
wizara ya Afya wakakae nao huko. Ndani ya siku mbili hizohizo ofisi hiyo
ijae vitanda na akina mama waliokuwa wanalala chini wahamishiwe kwenye
jengo hilo,” alisema.
Alisema ili Tanzania isiwe ombaomba lazima viongozi wajifunze kutokukubali kulea makosa.
“Kama
ni majipu tutayatumbua kwelikweli. Likienda kichwani tutalitumbua,
likienda kifuani tutalitumbua, likienda mgongoni tutalitumbua ili mradi
majipu yaishe na Tanzania iende mbele,” alisema.
Tanzania bila mapato haiwezekani
Alisema Tanzania haiwezi kuendelea bila kuwa na mapato yake.
“Wafanyabiashara
wamekuwa wakikwepa kulipa kodi. Mara ya kwanza tulipoanza kuchukua
hatua tulipata zaidi ya Sh1 trilioni, mwezi uliofuata tulipata Sh1.592
trilioni na Januari tulikusanya Sh1.063 trilioni,” alisema.
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano inataka kuona fedha hizo zikiwahudumia wananchi masikini.
“Zipo
kejeli nyingi, wanasema ni nguvu ya soda. Hata kama ni soda ukiweka
gongo utalewa. Hii ni soda ‘special’ ambayo tumedhamiria kufanya kazi
kwa ajili ya Watanzania. Haiwezekani nchi tajiri kama Tanzania tuwe
ombaomba, inatakiwa iwe inaombwa misaada,” alisema.
Aliwataka Watanzania kujenga utamaduni wa kulipa kodi na kudai risiti kwa kila manunuzi wanayoyafanya.
Kukwama
kwa mradi wa umeme
Kuhusu mradi wa umeme wa gesi wa Kinyerezi 2
uliokwama tangu mwaka 2012, alisema wafadhili kutoka Japan walitoa dola
292 za Marekani na Serikali ya Tanzania ilitakiwa kuchangia asilimia 15
ya fedha hizo.
Alisema mradi huo utaingiza zaidi ya megawati 240 za umeme.
“Fedha
hizo tumezitoa na kampuni kutoka Japan imeshaanza kazi na mwezi ujao
tunakwenda kuweka jiwe la msingi. Mradi wa ujenzi wa barabara ya juu Dar
es Salaam mkandarasi ameshaanza kazi na fedha za awali ameshalipwa,”
alisema.
Alisema upembuzi yakinifu wa mradi wa barabara ya njia
sita kutoka Dar es Salaam kwenda Chalinze, umeshamalizika na kuna
kandarasi zaidi ya 12 wameshaomba zabuni.
“Katika kipindi
hikihiki cha awamu ya tano itajengwa ili tuwe na barabara ya njia sita
kupunguza msongamano wa magari,” alisema.
Rais pia alidokeza
kuhusu mradi wa ujenzi wa daraja la urefu wa kilomita saba litakalopita
baharini kutoka ufukwe wa Coco hadi Hospitali ya Aga Khan, akisema
Serikali imeshapata zaidi ya Sh260 bilioni.
“Kuhusu barabara ya
Mbagala rangi tatu kuja mjini (Posta), nilikuwa nazungumza na ubalozi wa
Japan wapo katika utaratibu wa kutangaza tenda,” alisema.
Pia alizungumzia ujenzi wa barabara za juu zitakayojengwa kwenye makutano ya Ubungo.
Alisema makutano hayo yatakuwa na ghorofa tatu ambazo zitakuwa na barabara zinazokutana eneo hilo ili kuondoa tatizo la foleni.
“Benki
ya Dunia imekubali kutoka Sh67 bilioni kujenga interchange (mzunguko wa
juu wa barabara) ya ghorofa tatu pale Ubungo, nina uhakika watani zangu
wazaramu watakwenda pale kufunga ndoa,” alisema.
Kuifufua ATCL
Alisema Serikali ina mpango wa kufufua Shirika la Ndege (ATCL), ambalo
hivi sasa lina ndege moja lakini limeajiri wafanyakazi 200.
Alisema
kwa sasa wanakusanya fedha za kutosha ili kuweza kununua ndege aina ya
Airbus yenye uwezo wa kuchukua kuanzia abiria 120 na kuendelea, akisema
bei yake ni takriban Sh140 bilioni.
“Mkijipanga mnaweza kuwa mnanunua ndege moja kila mwezi,”alisema.
Elimu bure
Akizungumzia changamoto ya elimu bure alisema wanafunzi
walioanza darasa la kwanza nchini mwaka huu ni 1,337,000, jambo ambalo
alisema linaonyesha kuwa wananchi walikuwa wakishindwa kuwapeleka watoto
wao shule kwa sababu ya kukithiri kwa michango.
Alisema
changamoto zilizojitokeza baada ya Serikali kuanza kutoa elimu bure
watazimaliza, ikiwa ni pamoja na kutenga fedha nyingi zaidi kwa ajili ya
kuzipeleka katika shule.
Aliwashukuru wananchi ambao wameanza
kujitokeza kuchangia ujenzi wa madarasa na kumsifu Mkuu wa Wilaya ya
Kinondoni kwa kuendesha harambee ya kuchangia ujenzi wa shule.
Awashukia
wakuu wa mikoa na wilaya
Dk Magufuli pia alizungumzia utendaji wa wakuu
wa wilaya na mikoa na wakurugenzi wao, akiwataka kutathmini hali ilivyo
kwenye shule na ofisi zao.
“Kama unajua kujipima vizuri,
ujitambue kuwa hutoshi kuwa kiongozi. Sijateua wakuu wa mikoa, wakuu
wilaya na wakurugenzi ili niendelee kuwachambua vizuri (waliopo) ni nani
anatosha na nani hatoshi,” alisema..
“Kutosha kwao ni lazima
wajipange watatatua vipi kero za wananchi. Lazima ifike mahali viongozi
tujue jukumu letu. Unapopewa jukumu la uongozi wewe ni mwakilishi wa
wanyonge.”
Huku akiwataka Watanzania wa kada zote nao kujipima
walichoifanyia nchi ndani ya siku 100, alisema haingii akilini kiongozi
kusimama na kusema chakula hakuna wakati mvua inanyesha kila mkoa
nchini.
“Kiongozi umeshindwa hata kuhamasisha watu walime. Natoa
wito kwa viongozi wenzangu. Katika mkoa, wilaya au tarafa itakayokuwa
haina chakula kwa mwaka huu ambao mvua inanyesha, ajitambue hafai
kuongoza katika nchi,” alisema.
Alisema aliahidi
kuwalipa wazee waliolitumikia taifa lakini jambo hilo haliwezekani kama
kutakuwa na vijana wanaoshinda mitaani bila kufanya kazi.
“Najua
mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, wakuu wa mikoa wenzako watakuuliza
nitateua lini wakuu wa mikoa na wilaya. Kwanza tarehe ya kuteua
hawataijua na ninaendelea kuwachambua,” alisema Magufuli.
“Lakini
angalau Makonda umeshajihakikishia walau utakuwepo ila na wewe usiende
kulala, endelea kufanya juhudi. “Ukipanda cheo watu wasikuonee wivu.”
Alisema
Makonda amejijengea heshima kubwa kwa kuhamasisha watu wa kada
mbalimbali kumaliza changamoto za kuongezeka wa wanafunzi, uhaba wa
madarasa na madawati.
Kuhusu changamoto za elimu bure, Rais
alisema asilimia 80 ya viongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano wanaishi
Dar es Salaam, akiwamo yeye, waziri mkuu, mawaziri, makatibu wakuu na
naibu spika.
“Wao wakitoa milioni moja moja zinafika milioni 82
na zitabaki milioni 18, lakini kuna Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na mimi.
Tuigawane hii na kila mmoja achangie Sh6 milioni itimie Sh100 milioni
na tutaileta kwenye uongozi wa mkoa wa Dar es Salaam,” alisema.
Alisema
kwa mamlaka aliyonayo ataongeza Sh2 bilioni na kumtaka mkuu wa mkoa wa
Dar es Salaam kutozitumia vibaya, akitaka zigawanywe kwa kila wilaya ili
zijengwe shule za kutosha kufidia wanafunzi wanaokaa chini.
Afagilia
vyombo vya habari
Kiongozi huyo wa Serikali ya Awamu ya Tano pia
alizungumzia vyombo vya habari ambavyo alisema vimefanya kazi kubwa na
kuisaidia Serikali.
“Hata sisi huwa tunafuatilia. Mfano katika
gazeti la Jamhuri waliweka michoro fulani mpaka sisi (Serikali),
tukajiuliza wamejuaje tunachotaka kukifanya?” alisema.
Tazama hotuba ya Rais hapa
Tazama hotuba ya Rais hapa
0 comments:
Post a Comment