Mwenyekiti
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe,
amepingana na sera ya Rais John Magufuli ya kuwatumbua majipu
watumishi wa umma wazembe na wabadhilifu wa mali za umma.
Mbowe
amedai kuwa Serikali Magufuli imekuwa ikiwatimua watumishi mbalimbali
wa umma bila kuwapa nafasi ya kuwasikiliza kupitia kampeni ya kupambana
na ufisadi, inayotambulishwa kwa kaulimbiu ya ‘utumbuaji majipu’.
Akizungumza
jana katika ibada maalumu ya shukrani kwa kumaliza uchaguzi mkuu
salama, iliyofanyika kwenye Usharika wa Nshara wa Dayosisi ya Kaskazini
ya KKKT na kuhudhuriwa na Mkuu wa KKKT, Askofu Dk. Frederick Shoo, na
maaskofu wastaafu Dk. Erasto Kweka na Dk. Martin Shao, Mbowe alisema
(wapinzani) hawaridhishwi na hatua ya serikali ya Rais Magufuli
kuendeleza timuatimua na kuwasimamisha kazi watumishi wa umma 160 tangu
aingie madarakani bila kuwapa nafasi ya kuwasikiliza.
Mbowe
ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema
wapinzani wako tayari kuipongeza serikali wakati wowote inapofanya mambo
mazuri kwa manufaa ya taifa, lakini kwa sharti kwamba mara zote iwe
inahakikisha sheria za nchi zinasimamiwa, mali na rasilimali za umma
zinalindwa na kila kitu kinafanyika kwa kuzingatia taratibu zilizopo.
"Kutokana
na hali ya sintofahamu kutamalaki katika taifa kwa sasa, hakuna
mtumishi wa umma aliye na amani kutokana na mfumo unaoitwa kutumbua
majipu. Tunasikia watumishi wa umma wakifukuzwa kazi bila kusikilizwa.
“Mpaka
sasa kuna watumishi 160 wamefukuzwa na wengine kusimmishwa. Lakini pia
zaidi ya taasisi na idara za serikali zipatazo 20 hazina uongozi…hii si
sahihi,” alisema.
Katika
ibada hiyo, Mbowe alikuwa ameongozana na wabunge 16 na makada wengine
mbalimbali wa Chadema, alitoa sadaka ya Sh. milioni 279 kwa ajili ya
kusaidia ukarabati na upanuzi wa jengo la Bethel lililoko Hai.
"Sisi
tunamshukuru Mungu leo kwa kuwa tuko salama ndiyo maana tunatoa sadaka.
Sadaka yetu tunaielekeza kwenye upanuzi na ukarabati wa jengo hili la
Betheli la Usharika wa Nshara. Kwa hiyo, nawaomba sana viongozi wa dini
na Watanzania kuliombea taifa kutokana na hali inayoendelea," alisema Mbowe.
Kiongozi
huyo ambaye pia ni Mbunge wa Hai, alisema wabunge 42 wa Chadema
wamemuunga mkono kwa kuchangia kanisa hilo Sh. milioni 131.5; mwanasiasa
mkongwe na mfanyabiashara, Philemon Ndesamburo alimchangia Sh. milioni
50; marafiki zake wa Arusha Sh. milioni 49.9; Mwenyekiti mstaafu wa
Chadema, Edwin Mtei Sh. milioni mbili; makada wengine wa Chadema Sh.
milioni 15 na Kamati ya Maandalizi Sh. milioni 41.
Katika
hatua nyingine, Mbowe alitumia nafasi hiyo pia kuzungumzia mgogoro wa
uchaguzi wa kumpata Meya wa Jiji la Dar es Salaam kwa kuitupia lawama
CCM kwa madai kuwa ndio wanaokwamisha kwa maslahi yao.
Alisema
jambo hilo pia linasikitisha kwa sababu sasa ni miezi minne imepita
huku haki ya wananchi wa Jiji la Dar es Salaam kuwa na Meya wao
ikiendelea kuminywa kutokana na CCM kutoheshimu demokrasia na kutaka
waendelee kuongoza licha ya wananchi kufanya uamuzi wao kupitia sanduku
la kura katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana.
Chadema
na Chama cha Wananchi (CUF) vinavyoshirikiana kupitia Umoja wa Katiba
ya Wananchi (Ukawa), ndivyo vyenye idadi kubwa ya madiwani kulinganisha
na CCM, hivyo kwa mujibu wa Mbowe, CCM wamebaini kuwa hawawezi kushinda
na sasa wanajitahidi kadri wawezavyo kukwamisha uchaguzi huo.
0 comments:
Post a Comment