Serikali
imesema itachukua hatua kali kwa kampuni ya Halotel kama itashindwa
kutekeleza makubaliano ya mkataba wa kusambaza huduma za simu na mtandao
katika ofisi za Serikali katika kila Wilaya nchini kote.
Kauli
hiyo imetolewa na Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame
Mbarawa wilayani Maswa wakati akizungumza na watendaji wa sekta ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mkoani Simiyu na kusisitiza kutoa
ushirikiano unaostahili kwa kampuni hiyo.
“Makubaliano
yetu kati ya Serikali na Halotel ni kuunganisha ofisi za Umma kwa
mtandao zikiwemo shule tatu katika kila Wilaya, Hospitali, Mahakama na
Ofisi za Polisi ili kuwezesha mkakati wa mawasiliano vijijini
kutekelezeka”, amesema Prof. Mbarawa.
Waziri
Prof. Mbarawa ameeleza kuwa ifikapo mwaka 2017 kila eneo hapa nchini
litakuwa na huduma ya mawasiliano ya mtandao na kuwezesha wananchi wote
kunufaika na huduma hizo.
Katika
hatua nyingine Prof. Mbarawa amekagua Ujenzi wa Barabara ya
Lamadi-Bariadi KM 71.8 na Bariadi-Maswa KM 49.7 na kuwapongeza
makandarasi wanaojenga barabara hizo kwa kazi nzuri wanayofanya.
“Nawapongeza
kwa kazi nzuri mnayoifanya, hakikisheni kazi yenu inauwiana na thamani
ya fedha na kuhakikisheni wafanyakazi wazawa wanapewa kipaumbele katika
kazi wanazoziweza na kupewa mikataba stahiki ya kazi wanazozifanya”, amesititiza Prof. Mbarawa.
Aidha,
Waziri Prof. Mbarawa amemuagiza mkandarasi anaejenga barabara ya
Maswa-Mwigumbi KM 50.3 kuhakikisha nyumba zinazojengwa kwa ajili ya
mkandarasi zinajengwa kwa ubora ili zitumike kwa muda mrefu.
“Nakuagiza
Meneja wa TANROADS, hakikisha nyumba hizi baada ya mradi wa barabara
kukamilika unazikabidhi kwa jeshi la polisi ili waweze kuzitumia kwa
ajili ya makazi na ofisi”, amesema Prof. Mbarawa.
Kwa
upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Bw. Eraston Mbwilo amemwomba Waziri
Prof. Mbarawa kuelekeza nguvu za ujenzi wa ofisi na nyumba za watumishi
katika mkoa huo.
Katika
hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya ya Maswa Bi. Rosemary Kirigini amemuomba
Waziri Prof. Mbarawa kuwawezesha Wakala wa Majengo nchini (TBA)
kukamilisha mradi wa Ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo unaojengwa
sasa kwa miaka mitano ili kuipunguzia Wilaya hiyo adha ya kutumia jengo
chakavu ambalo si salama hasa kipindi cha mvua.
Waziri
Prof. Mbarawa pia amekagua Kiwanja wa Ndege kilichopo Mkoa wa Shinyanga
na ofisi za Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) kiwanjani hapo na kusisitiza
kuwa Serikali iko katika hatua za kuboresha uwanja huo kuwa wa kisasa
ili kuvutia mashirika mengi ya ndege kutumiwa kiwanja hicho.
Waziri
Prof. Mbarawa yupo kwenye ziara ya kukagua miradi ya ujenzi kwenye
sekta za barabara, nyumba, viwanja vya ndege na mkongo wa taifa wa
mawasiliano katika mikoa ya kanda ya ziwa ambapo ametembelea Wilaya za
Busega, Bariadi na Maswa mkoani Simiyu.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (aliyevaa koti
la bluu), akisikiliza maelezo ya mkandarasi kuhusu ujenzi wa mtambo
(hauonekani pichani) wa kusaga kokoto kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya
Maswa-Mwigumbi Km 50.3.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa, akiongea na
vibarua wanaofanya kazi kwenye mradi wa barabara ya Maswa-Mwigumbi Km
50.3, mkoani Simiyu.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akiongea na
wafanyakazi wa sekta za Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuhusiana na
mkakati wa Wizara wa kuongeza mapato mkoani Simiyu.
0 comments:
Post a Comment