Makamu
wa Rais wa Kampuni ya Total Afrika Mashariki Bw. Javier Rielo
amemuhakikishia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe
Magufuli, kuwa kampuni hiyo itaanza ujenzi wa mradi wa bomba la
kusafirisha Mafuta kutoka nchini Uganda hadi bandari ya Tanga hapa
Tanzania haraka iwezekanavyo, kwa kuwa fedha za kutekeleza mradi huo
zipo.
Bw. Javier Rielo ametoa ahadi hiyo leo tarehe 14 Machi, 2016 alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais Magufuli Ikulu Jijini Dar es salaam.
Mradi
huo utahusisha ujenzi wa bomba lenye urefu wa kilometa 1,410 ambalo
litasafirisha mafuta ghafi kutoka ziwa Albert nchini Uganda hadi Bandari
ya Tanga na utarajiwa kuzalisha ajira za moja kwa moja 1,500 na ajira
zisizo za moja kwa moja 20,000.
Katika
Mazungumzo hayo Bw. Javier amemueleza Rais Magufuli kuwa Kampuni yake
inatarajia kutumia dola za kimarekani karibu bilioni 4 ambazo tayari
zimeshaandaliwa.
Pamoja
na kuukaribisha uwekezaji huo mkubwa kwa Tanzania, Rais Dkt. John Pombe
Magufuli ameitaka kampuni hiyo kuharakisha mchakato wa kuanza kwa
mradi, na ameshauri muda wa miaka mitatu uliopangwa kuukamilisha mradi
huo upunguzwe, ili manufaa yake yaanze kupatikana mapema.
Kwa
upande wake Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo, amesema
Wizara yake ipo tayari kuhakikisha mradi huo unafanikiwa, na itatoa
ushirikiano wa kutosha kuharakisha utekelezaji wake.
Prof.
Mhongo amebainisha kuwa licha ya kwamba hali ya kijiografia, hali ya
hewa na bandari ya Tanga vinatoa mazingira bora ya kufanikiwa kwa mradi
huo, Tanzania pia inatarajia kunufaika na bomba hilo, kwa kuwa kuna
tafiti mbili za mafuta zinazoendelea katika ziwa Tanganyika na katikati
mwa Tanzania, ambazo zikikamilika kwa mafanikio inatarajiwa bomba hilo
litasaidia kusafirisha mafuta yake.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
14 Machi, 2016
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
akisalimiana na mmoja wa wajumbe walioambatana na Makamu wa Rais wa
Kampuni ya Total Afrika Mashariki, Javier Rielo Ikulu jijini Dar es
Salaam.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza
na Makamu wa Rais wa Kampuni ya Total Afrika Mashariki, Javier Rielo
Ikulu jijini Dar es Salaam
0 comments:
Post a Comment