Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano nchini Tanzania imewapiga marufuku wafanyakazi wake
''Kuchati'' katika mitandao ya kijamii kwa kutumia simu katika muda wa
saa za kazi.
Waziri wa Wizara hiyo Makame Mbarawa amekemea tabia
ya baadhi ya wafanyakazi, kutumia muda mwingi maofisini kuperuzi katika
mitandao ya kijamii pamoja na kupiga porojo, hali inayosababisha kushuka
kwa uzalishaji na maendeleo.
Ameongeza kuwa watakaobainika
kufanya hivyo watachukuliwa hatua za kisheria bila ya kuonewa haya, na
pia kuwataka wafanyakazi wa wizara yake kuwa na bidii ya kazi na weledi.
Lakini hata hivyo, marufuku hiyo itaweza kufanikiwa?, kutokana na
ukubwa wa matumizi ya mtandao, huku walengwa wakiona wananufaika nayo.
Kutokana
na kukua kwa teknolojia ya habari na mawasiliano duniani, watu wengi
hususan vijana wamekuwa wakitumia muda mwingi katika mitandao ya
kijamii, kupitia simu za mikononi na kompyuta, kwa lengo la kupata
taarifa mbalimbali za ulimwengu na pia kujifunza.
Nchini Tanzania
matumizi ya huduma ya mawasiliano imekuwa kwa kasi katika siku za hivi
karibuni, hususan kupitia mitandao ya WhatsApp, Facebook, Twitter na
blogi mbalimbali.
Chanzo: BBC Swahili
0 comments:
Post a Comment