Uamuzi wa Edward Lowassa kujiondoa CCM na kujiunga Chadema, bado unakitesa chama hicho tawala baada ya mikoa kuanza kuwashughulikia viongozi waliomuunga mkono wakati wa Uchaguzi Mkuu, huku baadhi wakisema wako tayari kupambana na wanaowatuhumu kusaliti chama.
Lowassa
alijiengua CCM Julai mwaka jana baada ya jina lake kuondolewa kwenye
mbio za urais kwa tiketi ya chama hicho, na baadaye kufuatwa na
mawaziri, wabunge, wenyeviti wa mikoa na madiwani na hivyo kufanya
Uchaguzi Mkuu kuwa na ushindani mkubwa.
Baada ya kumalizika kwa
uchaguzi huo, viongozi na wanachama wa CCM walioonekana kuwa karibu na
waziri huyo mkuu wa zamani, walituhumiwa kukihujumu chama kwa kumpigia
kampeni Lowassa wakati wa usiku, huku mchana wakijionyesha kuwa wanaunga
mkono wagombea wa CCM.
Tuhuma hizo ziliongezewa nguvu na
mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete takriban wiki mbili zilizopita
alipotangazakuwa waliosaliti chama hicho watatumbuliwa bila ya aibu, na
tayari mkoa wa Manyara umeshatangaza kuwatimua uanachama viongozi 21
wanaotuhumiwa kushabikia upinzani.
Viongozi wa mikoa wamekanusha tuhuma zinazoelekezwa kwao kuwa
walisaidia upinzani wakati wa uchaguzi wa mwaka jana.
Miongoni
mwa wanaotuhumiwa ni mwenyekiti wa Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu
ambaye aliangushwa kwenye kura za maoni ndani ya chama hicho na
Frederick Mwakalebela, ambaye pia alishindwa na Mchungaji Peter Msigwa
kwenye kinyang’anyiro cha ubunge wa Jimbo la Iringa Mjini.
Mwenyekiti huyo anatuhumiwa kubadili timu yake ya kampeni na kuifanya iwe ya kumpigia debe mgombea huyo wa Chadema.
Lakini
Msambatavangu, ambaye pia anadaiwa kutoa gari zake zitumike kwenye
kampeni za wapinzani, alisema yupo tayari kuhojiwa ili ajibu tuhuma
dhidi yake ambazo tayari zimewasilishwa kwenye chama hicho.
Alisema anasubiri ahojiwe ili aeleze ukweli kuhusu suala hilo.
Mwakalebela alifungua kesi Mahakama Kuu akidai kuwa taratibu zilikiukwa wakati wa kuhesabu kura.
Mwingine
anayezungumzwa ni mwenyekiti wa CCM wa Simiyu, Dk Titus Kamani, ambaye
alikuwa Waziri wa Uvuvi na Maendeleo ya Mifugo katika Serikali
iliyopita, ambaye amezielezea tuhuma dhidi yake kuwa ni majungu ya
wasiompenda ambao wanataka avuliwe uongozi.
Dk Kamani anadaiwa
kuwawezesha kwa hali na mali baadhi ya wagombea wa upinzani, kama kutoa
vyombo vya matangazo na gari lake wakati wa kampeni.
Ilidaiwa kuwa kutokana na msaada huo, wagombea wa upinzani walishinda katika kata ya Lamadi na Mkula.
“Matokeo ya uchaguzi yanaonyesha wazi kuwa wanaCCM kwa ujumla walikuwa na umoja,” alisema Dk Kamani.
“Majimbo
mawili kati ya saba kwenye mkoa huu yalikuwa yanashikiliwa na upinzani,
lakini tumefanikiwa kuyakomboa. Hata kata nyingi zilikuwa ngome ya
upinzani, lakini tumezikomboa. Sasa kama zilizopotea hizo mbili, mimi
nahusika vipi?”
Tuhuma kama hizo zilielekezwa kwa Profesa Juma
Kapuya, ambaye licha ya kupitishwa na CCM kugombea ubunge wa Jimbo la
Kaliua, anatuhumiwa kujinadi yeye na Magufuli, lakini akatumia usiku
kumuombea kura Lowassa aliyegombea urais kwa tiketi ya Chadema.
Profesa
Kapuya, ambaye aliangushwa kwenye jimbo hilo na Magdalena Sakaya wa
CUF, alisema anaijua vyema CCM, hivyo asingeweza kufanya usaliti na
kuendelea kubaki ndani ya chama hicho.
“Mungu pekee ndiye
anayejua jinsi nilivyojituma kumuombea kura Dk Magufuli aliyekuwa
mgombea wetu ambaye ameshinda na kuwa Rais. Sijui wanaonituhumu
wanaanzia wapi,” alisema Profesa Kapuya.
Alisema hakukuwa na
muda wa kufanya usaliti kwa sababu alikuwa anaachana na kamati ya
kampeni usiku mara baada ya kumaliza vikao vya tathmini ya mikutano ya
hadhara.
“Mtu kama mimi nitawezaje kufanya usaliti kama huo.
(Nikifanya) Basi hapo shule itakuwa haijanisaidia,” alisema Profesa
Kapuya ambaye amebobea kwenye elimu ya mimea.
“Pia ninaijua vyema CCM. Huwezi kuwa msaliti ukabaki kuwa salama huku ukiendelea kubaki hivyo. Ningejitoa mwenyewe.”
Tayari
viongozi 21 wa Manyara wametimuliwa kwa tuhuma hizo.Kati ya
waliotimuliwa, watatu ni kutoka Babati Mjini na wengine 18 wa ngazi ya
kata.
Inadaiwa
kuwa viongozi waliotimuliwa walikuwa wanamshabikia Lowassa na
kusababisha CCM kupoteza jimbo na kata tano kati ya nane za Babati
Mjini, kwa mujibu wa katibu wa CCM wa Manyara, Ndeng’aso Ndekubali.
0 comments:
Post a Comment