Adverts

Wednesday, March 16, 2016

Majaliwa Amtumbua JIPU Mhandisi wa Maji Nyumbani Kwa Rais Magufuli


Rungu la kuwatumbua majipu watumishi wa umma wasiowajibika limetua kwa Mhandisi wa Maji Wilaya ya Chato, Peter Ngolemi baada ya Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa kuagiza kusimamishwa na kuamuru Takukuru kumchunguza kutokana na kumdanganya. 

Ngolemi, anadaiwa kumdanganya Majaliwa kuhusu mradi wa maji katika Kijiji cha Kalebezo ambao umesababisha wananchi kutembea umbali mrefu kutafuta huduma hiyo.
 
Mradi huo umesimama tangu mwaka 2011, kutokana na kukosa usimamizi baada ya mashine mbili kutofanya kazi. Licha ya kumsimamisha, Waziri Mkuu aliagiza Takukuru kumchunguza na kumchukulia hatua za kisheria. 

“Hatuwezi kuwa na kiongozi muongo, naondoka naye. Mtumishi huyu atakaa pembeni Takukuru wamchunguze,” alisema.

Kabla ya kuchukua uamuzi huo, Majaliwa alimwita jukwaani na kumtaka ajibu madai ya wananchi kukosa maji muda mrefu.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu, kuna mashine mbili na hili suala lipo kwa Mamlaka ya Maji Bukoba, lakini zile pampu mbili zipo,” alijibu Ngolemi huku akitetemeka na wananchi wakimzomea.

Hatua hiyo ilisababisha Majaliwa kusema: “Huwezi kumdanganya Waziri Mkuu anayetegemewa na wananchi wengi, nimepita pale wananchi wana mabango wanadai mashine ziling’olewa na kupelekwa Morogoro, halafu leo unaniambia zipo!

“Sasa naondoka na wewe, kaa pembeni kuanzia sasa hakuna kazi, Takukuru mchunguze na kumchukulia hatua.”

Baada ya agizo hilo, maofisa wa usalama walimchukua mhandisi huyo na kuondoka naye kwenye Uwanja wa Chato.

Katika hatua nyingine, Majaliwa ameagiza kufutwa kwa umiliki wa mashamba makubwa 11 yakiwamo ya Kanisa Katoliki Jimbo la Rulenge yenye ukubwa wa ekari 7,700 kwenye vijiji vya Kasharazi na Rwakalemera, Wilaya ya Ngara mkoani Kagera, kutokana na kutokuwa na hati na kutelekezwa kwa muda mrefu.

Pia, Majaliwa ameagiza kusimamishwa kazi kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, Colnel Ngudungi na kutaka arejeshwe wilayani hapa kujibu tuhuma za kuhusika na upotevu wa fedha za mauzo ya mbao kwenye Msitu wa Rumasi.

Ngudungi alihamishwa kwenda Sekretarieti ya Mkoa wa Shinyanga Agosti 2015, kwa kile kilichoelezwa kuwa anakwenda kwa kazi maalumu.

Majaliwa ambaye alikuwa njiani kuelekea Geita akitokea Kagera, alitoa maagizo hayo jana alipozungumza na wakazi wa vijiji vya Kasulo na Rwakalemera, baada ya kusimamishwa na wananchi wakiwa na mabango wakiomba kurejeshewa ardhi ya kijiji huku baadhi yao wakidai wanatishiwa kwa bunduki wanaposogelea mashamba hayo.

Waliendelea kuwa uongozi wa kijiji umekithiri kwa ubadhirifu kwani licha ya Msitu wa Rumasi kuuzwa na mapato kutoonekana, kijiji kina minada ya ng’ombe ambayo sheria inataka asilimia 20 ya mapato ibaki eneo hilo.

Awali, Waziri mkuu alimuita kwenye mkutano huo Ofisa Ardhi na Maliasili wa Wilaya, Betty Munuo ili aeleze chanzo cha mgogoro wa ardhi katika vijiji hivyo.

Akitoa ufafanuzi huo, Munuo ambaye amehamishiwa wilayani hapo Agosti mwaka jana, alisema malalamiko hayo ameyarithi kwa mtangulizi wake na amefanya uchambuzi wa majina ya wamiliki wote wa mashamba na kwamba, uongozi wa wilaya ulikuwa unapanga kuwapatia notisi ya kujieleza.

Munuo alisema kati ya wamiliki 18 wa mashamba makubwa, saba ndiyo wenye hati huku matatu pekee ndiyo yameendelezwa.

Kwa mujibu wa Munuo, mashamba yaliyoendelezwa yanatumika kwa kilimo, ufugaji na shule na kwamba Shamba namba 606 lenye ukubwa wa ekari 161 linamilikiwa na Kanisa Katoliki Dayosisi ya Rulenge, Dario Zakaria shamba ana ekari 282 na Masista wa Mtakatifu Fransisco wanamiliki ekari 759.

“Mashamba manne ndiyo yenye hati lakini yametelekezwa, yaliyotelekezwa yote yapo Kijiji cha Rwakalemera nayo ni ya Abdallah Sadalla (ekari 521); Mahsen Saidi (458); Mshengezi Nyambele (3,88) na Mushengezi Nyambele (497).

Majaliwa aliwataja wamiliki wa mashamba yasiyo na hati kuwa ni Joseph Rugumyamheto (505) lipo Rwakalemera, Nicholaus Kidenke, Gwasa Angas Sababili (236) lipo Kasharazi na Makumi Rufyega (500) lipo Rwakalemera.

Wamiliki wengine ambao mashamba yao yapo kijiji cha Rwakalemera na ukubwa wake kwenye mabano ni Paulo Shikiri (250), Frank Derila (750), Godfrey Kitanga (800), Phillemon Mpanju (200), Issa Sama (500), Hekizayo Mtalitinya (225) na Joel Nkinga (1,250).

Majaliwa aliagiza kurejeshwa mara moja aliyekuwa Ofisa Ardhi wa Wilaya hiyo, Enock Mponzi ambaye amehamishiwa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya mkoani Mara ili aende kusaidia uchunguzi.

0 comments:

Post a Comment