Idara ya Uhamiaji nchini imefanya mabadiliko ya maofisa waandamizi kwa
kuwahamisha vituo vya kazi kuanzia ofisi ya makao makuu, mikoa, wilaya
na mpakani.
Pangapangua hiyo ni utekelezaji wa agizo la Waziri
wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga alilolitoa kwenye kikao chake na
viongozi wakuu wa idara hiyo kilichofanyika Februari 23.
Siku
hiyo, Waziri Kitwanga aliagiza kufanyika kwa mabadiliko hayo
kutokana na kukithiri kwa vitendo vya upitishaji dawa za kulevya na
wanyama hai kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na
Kilimanjaro (KIA) na kwenye mpaka wa Tunduma, Mtukula, Halolili na
Kasumulo.
Pia,
aliagiza kuhamishwa kwa wakuu wa upelelezi wote wa wilaya za Dar es
Salaam na maofisa wa uhamiaji waliokaa kwenye kituo kimoja kwa zaidi ya
miaka mitatu, huku akisema huo ni mwanzo wa mabadiliko makubwa kwenye
idara hiyo.
Akitangaza mabadiliko hayo jana, Naibu Kamishna wa
Uhamiaji, Abbas Irovya (pichani), alisema upanguaji huo unalenga
kuimarisha utendaji, ufanisi na dira katika idara hiyo.
“Pamoja
na orodha hii ya maofisa waandamizi wanaohama vituo vyao vya sasa kwenda
vituo vingine, Idara ya Uhamiaji inaendelea na utaratibu wa
kuwabadilisha vituo vya kazi maofisa zaidi ya 200 kutoka sehemu
mbalimbali nchini ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga,” alisema.
Irovya,
ambaye alitangaza mabadiliko hayo kwa niaba ya Kaimu Kamishna Jenerali
wa Uhamiaji, alisema amewahamisha Ofisa Uhamiaji, Faustine Nyaki,
aliyekuwa mkoani Iringa, kwenda Mwanza kuwa ofisa uhamiaji wa mkoa.
Wengine
waliohamishwa ni Remigius Pesambili (Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Mwanza),
anayekwenda kuwa mfawidhi wa ofisi ya Uhamiaji ya Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Rose Mhagama (Ofisa Uhamiaji Mkoa wa
Geita) anayehamia Njombe.
Assa Mwansansu aliyekuwa Mfawidhi wa
Kitengo cha Hati za Ukazi, anahamia Pwani kuwa ofisa uhamiaji wa mkoa,
Safina Muhindu (Ofisa Uhamiaji wa Wilaya ya Ilala), anahamia Morogoro
kuwa ofisa wa mkoa na Wilfred Marwa (Naibu Ofi sa Uhamiaji wa Tanga),
anayehamia Geita kuwa ofisa uhamiaji wa mkoa.
Alisema Evarist
Mlay (aliyekuwa Ofisa Uhamiaji wa Wilaya ya Kinondoni) anahamia Wilaya
ya Same, wakati Frank Mwakifuna (aliyekuwa Ofisa Uhamiaji Same),
anahamia Kinondoni, huku Pilly Mdanku (ofisa wa hati za kusafiria wa
Makao Makuu), anakuwa Ofisa Uhamiaji wa Wilaya ya Ilala na George Goda
(kitengo cha Hati za Ukazi Makao Makuu) anahamia Temeke kuwa ofisa
uhamiaji wa wilaya.
Mwingine aliyehamishwa ni jafari Kisesa,
ambaye alikuwa ofisa Uhamiaji wa Wilaya ya Temeke, anahamia Tanga kuwa
naibu ofisa wa uhamiaji wa mkoa.
Pia, Julieth Sagamiko (Kitengo
cha Hati za Kusafiria cha Makao Makuu) amehamishiwa Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kuwa mfawidhi wa kituo na nafasi yake
itashikwa na Fredrick Eustace Kiondo, huku Naibu Ofisa Uhamiaji Mkoa wa
Kagera, Hosea Kagimbo akihamishiwa Holili kuwa mfawidhi wa kituo.
Pia,
alisema Kaimu Kamishna, Jenerali wa Uhamiaji, Victoria Lembeli
amewabadilisha vituo vya kazi maofisa hao 14, huku baadhi ya maofisa
wakistaafu utumishi wa umma akiwamo aliyekuwa mfawidhi wa kituo cha
Holili, Kaimu Kamishna, Alphonce Tishe.
0 comments:
Post a Comment