Mkurugenzi
Mtendaji wa zamani wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), David Mattaka
na wenzake wawili wamepandishwa kizimbani wakikabiliwa na mashtaka sita
yakiwamo ya matumizi mabaya ya madaraka, kughushi na kuisababishia
hasara Serikali kupitia ukodishaji wa ndege.
Wakili
Mkuu wa Serikali, Timon Vitalis akishirikiana na mawakili wa Takukuru,
Joseph Kiula na Stanley Luoga waliwataja washtakiwa wengine
wanaokabiliwa na kesi hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage
kuwa ni Ofisa Mtendaji Mkuu Mstaafu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi
ya Umma (PPRA), Ramadhan Mlinga na Mwanasheria wa mamlaka hiyo, Bertha
Soka.
Wakili
Vitalis alidai kuwa Oktoba 9, 2007 katika ofisi za ATCL zilizopo
wilayani Ilala, Mattaka alitumia vibaya madaraka kwa kutia saini mkataba
wa ukodishaji wa ndege A320-214 iliyotengenezwa kwa namba 630 baina ya
Wallis Trading Inc na ATCL.
Alidai alifanya hivyo bila ya kuzingatia Sheria ya Manunuzi ya Umma na taratibu za zabuni kwenye mchakato huo.
Pia,
alidai Oktoba 27, 2007 alitumia vibaya madaraka yake kwa kutia saini
cheti cha kuruhusu mchakato wa ukodishaji wa ndege hiyo bila ya kufuata
ushauri wa kiufundi aliopewa na kuisababishia Serikali hasara ya dola
772,402.08 za Marekani zilizolipwa kwa kampuni ya Aeromantenimiento,S. A
kama gharama za huduma ya matengenezo.
Kuhusu
Mattaka, wakili huyo alidai Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kumpa
dhamana na kwamba, anaweza kuomba kudhaminiwa kupitia Mahakama Kuu.
Washtakiwa
Mlinga na Bertha wanadaiwa kuwa Machi 19, 2008 katika ofisi za PPRA
walighushi muhtasari wa kikao cha siku ukionyesha mamlaka hiyo ilijadili
maombi ya ATCL juu ya kuidhinishwa kwa mkataba huo.
Washtakiwa hao walikubaliwa dhamana kwa kuwa shtaka linalowakabili linadhaminika. Kesi hiyo iliahirishwa hadi Machi 29.
0 comments:
Post a Comment