Mkuu
wa Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Chande Nalicho ameagiza kushushwa
vyeo wakuu wa shule zote za msingi na sekondari katika wilaya hiyo,
ambao shule zao zimefanya vibaya katika matokeo ya mtihani wa kumaliza
elimu ya msingi na sekondari mwaka 2015/2016.
Aidha
amewataka wenyeviti na wajumbe wa bodi za shule kujipima uhalali wao
kama wana sifa ya kuendelea kuwemo katika nyadhifa zao, kutokana na
matokeo mabaya yaliyopata shule wanazozisimamia ambayo yameitia aibu
wilaya hiyo.
Alisema
wenyeviti na wajumbe wa bodi ni lazima waachie ngazi kwani shule zao
zimefanya vibaya na imeonekana sababu mojawapo ya kufanya vibaya kwa
shule hizo ni walimu kutowajibika.
Alisema wameshindwa kuwafuatilia na kushindwa kushirikiana na wazazi kutatua changamoto mbalimbali zinazozikabili shule zao.
Nalicho
alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na wakuu wa shule nne za
sekondari, wajumbe na wenyeviti wa bodi za shule hizo zilizofanya vibaya
katika matokeo ya kumaliza elimu ya sekondari mwaka uliopita.
Alikutana
nao katika kikao maalumu cha kazi na baadhi ya watumishi wa kata ya
Lusewa kilicholenga kutafuta majawabu juu ya kero zinazowakabili wakazi
wa kata hiyo.
Shule zilizofanya vibaya katika matokeo hayo ni Lusewa, Msisima, Kwizombe na Matepwende.
Aliwataka
walimu na wakuu wa shule hizo kuongeza juhudi katika kuwasaidia watoto
madarasani ili waweze kufanya vizuri katika masomo yao.
“Sitakubali
mwaka ujao kuona shule zenu zinaendelea kushika mkia, ninyi ndiyo
chanzo cha wilaya yetu kushika nafasi ya pili kutoka mwisho katika
matokeo ya mitihani ya mwaka jana. Nataka muongeze juhudi katika kazi
zenu, tumieni muda mwingi kuwafundisha hawa watoto madarasani, badala ya
kutumia muda wenu kwa ajili ya kufanya anasa,” alisema Nalicho.
Alisema
suala la elimu ni muhimu katika maisha ya binadamu kwani hakuna
anayeweza kufanikiwa katika maisha yake kama hajakwenda shule.
Aliwasisitiza
kuwa muda umefika kwa wakazi wa kata hiyo kuona aibu na matokeo hayo,
badala yake wahimize watoto wao kupenda shule kwa kuwa elimu ndiyo
urithi bora kwa mtoto.
0 comments:
Post a Comment