Na Fatma Salum na Sheila Simba, MAELEZO
Spika
wa zamani wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Pius Msekwa
amewaasa watanzania kuacha kufuata mkumbo wa kisiasa badala yake watii
mamlaka ili kuepuka kuvunja sheria na kuleta madhara kwao binafsi na
taifa kwa ujumla.
Msekwa
aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumzia masuala
mbalimbali kuhusu mwenendo wa siasa za hapa nchini na utendaji kazi wa
Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. John Pombe
Magufuli. Alieleza kuwa watu wengi wana hulka ya kufuata mkumbo kwenye
mambo fulani bila ya kuchunguza na kufahamu ukweli wake kabla ya
kushabikia.
“Ni
hulka ya watanzania kushabikia mambo wasiyoyafahamu ilimradi tu
yanawafurahisha masikioni au machoni mwao kwani hata huko mitaani
wanakimbilia ngoma bila ya kujua inatokea wapi au inaelekea wapi, hivyo
nawasihi wajaribu kuwa makini na mbinu za siasa zinazotumiwa na baadhi
ya vyama kwa kuwa nyingine zina madhara ndani yake.” Alisema Msekwa.
Akifafanua
mwenendo wa siasa za hapa nchini, Mzee Msekwa alisema kuwa bado
wanasiasa wengi hawafuati kanuni za ushindani wa kisiasa katika kutafuta
madaraka badala yake wanatumia mbinu ambazo zinavunja sheria za nchi na
hatimaye wanapambana na mamlaka.
“Ushindani
wa kisiasa ni jambo la kawaida na linalokubalika ingawa ushindani huo
ni lazima ufuate sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ili kufikia
lengo, hivyo kubuni vitu ambavyo vinachochea utovu wa nidhamu na
uvunjifu wa amani sio jambo zuri, ' alisisitiza.
Aidha,
Msekwa alieleza kuwa utendaji wa Mhe. John Magufuli ni wa kuridhisha na
wa aina yake kwa kuwa amekusudia kuleta mabadiliko chanya kwa
watanzania na kuondoa mfumo wa utendaji kazi kwa mazoea jambo ambalo
limesaidia kurudisha nidhamu kwa watumishi wa Serikali.
Akizungumzia
uzoefu wake katika masuala ya kuongoza Bunge, alieleza kuwa tofauti ya
Bunge la zamani ni kwamba lilikuwa na nidhamu kubwa na linaheshimika
lakini Bunge la sasa halina utii na hicho ndio chanzo cha malumbano
yanayojitokeza mara kwa mara katika vikao vya Bunge.
Aliongeza
kuwa tangu awali wapinzani kazi yao ni kuipinga Serikali iliyo
madarakani lakini kwenye Bunge la uongozi wake walikuwa wakipinga kwa
kutumia hoja na kufuata kanuni bila ya kudharau mamlaka ya Spika wala
Serikali iliyoko madarakani.
“Kanuni
zinatoa nafasi kwa mbunge asiyeridhika na maamuzi ya Spika kushitaki
kwenye Kamati ya Kanuni za Bunge, na kamati hiyo itasikiliza na kutoa
uamuzi kama mahakama inavyosikiliza lakini wabunge wa sasa hawataki
kutumia utaratibu bali hutumia mbinu za tofauti ili waweze kupata sifa
ambazo hazina tija kwa wananchi waliowachagua,” alisema.
Msekwa
pia amewaasa vyama vya upinzani kutumia mbinu nzuri katika kutafuta
madaraka bila ya kuvunja sheria au kuhatarisha amani ya nchi kwani
waliowachagua wanategemea zaidi matokeo ya kazi waliyoahidi kuwatumikia
kuliko malumbano yasiyo na tija kwa ustawi wao na taifa.
0 comments:
Post a Comment