Adverts

Showing posts with label Siaisa. Show all posts
Showing posts with label Siaisa. Show all posts

Friday, October 7, 2016

Waziri Mkuu Akutana na Madudu Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA)

 
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Bunge), Bw. Uledi Mussa afuatilie malipo ya kiwanja kilichouzwa na CDA kwa sh. milioni 240 lakini fedha iliyoingia ofisini ni sh. milioni 6 tu.

“Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, ninataka ufuatilie mauzo ya kiwanja namba 26 block AA eneo la Kikuyu East ambacho kimeuzwa kwa sh. milioni 240 lakini fedha iliyoingia CDA ni sh. milioni 6 tu. Nataka kujua nani ameingiza milioni 6 na nani kachukua hizo sh. milioni 234,” alisema.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana mchana Alhamisi, Oktoba 6, 2016 wakati akizungumza na watumishi na viongozi wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) kwenye ukumbi wa Hazina ndogo mjini Dodoma.

Bila kutoa ufafanuzi zaidi, Waziri Mkuu alisema eneo hilo lilipaswa kuwa na kituo cha mafuta na akataka apatiwe taarifa mapema iwezekanavyo.

Pia alimwagiza Katibu Mkuu huyo afuatilie mkataba wa upangishaji wa jengo la CDA ambalo wamepangishwa taasisi ya Tunakopesha Limited kwa madai kuwa mhusika alipewa bure na sasa anataka kulipangisha tena ili apate cha juu.

Waziri Mkuu aliwaonya watumishi hao pamoja na viongozi wao waache tabia ya kushirikiana na madalali kuuza viwanja na akawataka wachape kazi wakijielekeza na kasi ya Serikali ya kuhamia Dodoma.

“Tabia ya watumishi kushirikiana na madalali kuuza ardhi sasa basi. Hata hivyo, nimefarijika kukuta mmeanza kuweka mfumo wa kielektoniki katika baadhi ya huduma. Ni lazima mauzo ya viwanja sasa hivi yafanyike kwa njia ya kieletroniki, madalali hawana nafasi,” alisisitiza.

Aliutaka uongozi wa CDA uongeze kasi ya upimaji viwanja kwa sababu mahitaji ni makubwa lakini akaonya kuwa wakati zoezi hilo likifanyika, wananchi walionunua viwanja na bado hawajamalizia kuvilipia, wasinyang’anywe kwa kigezo cha kutaka kuwauzia wengine.

“Mimi nataka idadi ya viwanja vilivyopimwa iongezeke. Lakini pia msitumie fursa hii kuwanyang’anya watu wenye umiliki halali eti kwa sababu Serikali inataka idadi ya viwanja vilivyopimwa iongezeke,” alisema.

“Kama mtu amepewa offer au hati yake asinyang’anywe hata kama amelipia nusu asinyang’anywe. Ahimizwe kumalizia hilo deni na ninyi kazi yenu ni kupima viwanja vingine,” alisisitiza.

“Natambua mnayo benki ya viwanja, lakini inabidi muongeze idadi ya viwanja vingi zaidi. Tumeita wawekezaji waje kujenga nyumba za kuishi watumishi, mahoteli na viwanda na maeneo yote haya inabidi yatengwe rasmi,” alisema.

Alisema jumla ya viwanja 70,000 vimepimwa tangu CDA ianzishwe mwaka 1973. Amesema kama wataendelea na kasi hiyo wakati mahitaji yameongezeka, itawachukua zaidi ya miaka 40 kukamilisha mahitaji ya viwanja 100,000 ambavyo vinatarajiwa kuanza kupimwa hivi karibuni.

Mapema, akitoa taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mkuu wa CDA, Eng. Paskasi Muragili alisema usanifu wa upimaji viwanja 20,000 umekamilika na kwamba wana lengo la kupima viwanja vingine 100,000 ifikapo Juni 2017.

Waziri Mkuu alitembelea Ofisi ya CDA na kukagua mfumo wa utunzaji mafaili wa zamani pamoja na uhamishaji wa taarifa za wenye viwanja kwenye mfumo wa kompyuta. Pia alikagua mifumo ya uuzaji viwanja kwa njia ya mtandao ambayo hata hivyo bado haijakamilika.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu alipokea mchango wa zaidi ya sh. milioni moja kutoka kwa Mkuu wa Wilaya wa Kongwa, Bw. Deogratius Ndejembi zikiwa ni kwa ajili ya wakazi wa mkoa wa Kagera walioathirika kwa tetemeko la ardhi lilitokea Septemba 10, mwaka huu.

Pia Waziri Mkuu alipokea mchango mwingine wa zaidi ya sh. milioni tano kutoka kwa makundi mbalimbali ya wafanyabiasha wa Manispaa ya Dodoma wakiwemo wamiliki wa hoteli, nyumba za kulala wageni, waendesha bodaboda na madereva wa daladala.

Akipokea msaada huo, Waziri Mkuu aliwashukuru wafanyabiashara hao na kuwahakikishia kwamba fedha hizo zitapelekwa mkoani Kagera na kuwafikia walengwa kama ilivyokusudiwa.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU

Zitto Kabwe Awamwagia Sifa UKAWA ......Atia Neno Kuhusu Mgogoro wa CUF


Kiongozi Mkuu wa Chama Cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ameisifia nguvu ya vyama vya siasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwa kile walichokifanya hasa katika uchaguzi wa mwaka jana.
 
Akizungumza jana katika mahojiano maalum na kituo cha runinga cha Clouds TV, Zitto alisema kuwa chama chake hakiwezi kubeza nguvu kubwa iliyooneshwa na umoja huo na kwamba uliweka historia katika chaguzi zote zilizowahi kufanyika nchini.
 
“Ukawa umeweka historia Kubwa zaidi katika chaguzi za nchi yetu japo kuwa kuna madhaifu ila hatuwezi kupuuza nguvu ile,” alisema Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini.
 
Hata hivyo, pamoja na kusifu nguvu ya muungano huo wa hivyo vya siasa ambavyo ni Chadema, Chama Cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na NLD, Zitto alisisitiza kuwa chama chake hakitajiunga na umoja huo kutokana na maazimio na miiko waliyoiweka katika Azimio la Tabora la chama chake.
 
“Hatukuweza kujiunga na Ukawa kwasababu tuliweka kanuni zetu wazi  tulizozitangaza katika azimio la Tabora,” Zitto anakaririwa.
 
Katika hatua nyingine, Zitto alizungumzia mgogoro wa uenyekiti wa CUF unaoendelea ndani ya chama hicho na kutoa rai kwa vyama vingine vya siasa kutowafarakanisha.
 
Alisema kuwa CUF inapaswa kuachiwa suala hilo walimalize wenyewe katika vikao vyao vya ndani ya chama na sio vinginevyo. 

Aliongeza kuwa kutokana na mgogoro unaoendelea ndani ya CUF, hivi sasa ajenda yao kubwa [kupinga kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa Oktoba]imewekwa kando bali sasa wanatafuta uhalali wa kiongozi wa chama hicho.
 
“Rai yangu tusichochee kabisa mgogoro huu bali ni tuwe kama madaraja ya kufanikisha mgogoro huu kumalizimika kwa amani,” alisema.
 
Hata hivyo, mapema wiki hii Baraza Kuu la Uongozi wa CUF lilifungua shauri mahakamani kuhusu mgogoro wa uongozi ndani ya chama hicho, wakimshataki Msajili vya Vyama vya Siasa nchini pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

 Katika shauri hilo, wanapinga uamuzi wa Msajili kuandika barua ya kumtambua Profesa Ibrahim Lipumba kuwa Mwenyekiti halali wa chama hicho huku wakidai kuwa alijiuzulu na taarifa za kujiuzulu kwake waliziwasilisha kwa Msajili.
 
Baraza hilo limedai katika shauri hilo kuwa katiba na sheria ya vyama vya siasa haimpi mamlaka Msajili kuingilia maamuzi ya ndani ya vyama vya siasa. Shauri hilo bado halijaanza kusikilizwa.

Sunday, October 2, 2016

ACT-Wazalendo waitisha mkutano wa kidemokrasia Kupigania Upatikanaji wa Katiba Mpya


Chama cha ACT- Wazalendo kimepanga kuwasha moto mjadala wa Katiba mpya katika mkutano wake kidemokrasia kilioitisha jijini Dar es Salaam Oktoba 8. 
Mkutano huo unalenga kufufua mchakato wa Katiba Mpya kwa kuzingatia michakato ya katiba za nchi nyingine za Afrika, alisema Katibu wa itikadi na uenezi wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu alipozungumza na waandishi jijini Dar es Salaam  jana. 
Alisema katika kupata uzoefu, ACT Wazalendo imemualika Adabu Namwamba, ambaye ni kiongozi wa Chama cha Labour cha Kenya kilichofanikiwa kubadilisha katiba yake baada ya mchakato mrefu. 
 Aliwataja wageni wengine kuwa ni mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania, Deus Kibamba ambaye naye atatoa mada kuhusu suala hilo. 
Mchakato wa kuandika Katiba mpya nchini umekwama katika hatua ya kupiga Kura ya Maoni baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kushindwa kukamilisha uandikishaji wapigakura kwa muda uliotakiwa. 
Mchakato huo uligubikwa na vikwazo kadhaa, ikiwa ni pamoja na vyama vinne vya upinzani na baadhi ya wajumbe kususia kwa maelezo kuwa Bunge liliacha Rasimu ya Katiba iliyokuwa na maoni ya wananchi na kuingiza sera za CCM. 
Katika mkutano huo, kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe atawasilisha mada kuhusu hali ya nchi kwa mtazamo wa chama hicho. 
“Kiongozi wetu atawasilisha uchambuzi mpana wa kina zaidi kuhusu hali ya nchi yetu kiuchumi, kisiasa na kijamii tangu Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani,” alisema. 
Pia, mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Anna Mghwira, ambaye aligombea urais mwaka jana, ataeleza uzoefu wake katika uchaguzi, wakati mshauri wa chama hicho, Profesa Kitila Mkumbo atachambua mwelekeo wa chama hadi mwaka 2020. 
“Chama kinatoa wito kwa wananchi wanaotaka kushiriki katika mkutano huo kuwasiliana na ofisi ili kujiandikisha,” alisema.

Maazimio 8 ya UKAWA kukabiliana na Prof. Lipumba na Msajili wa vyama


Umoja wa Katiba ya Wananchi umedhamiria kwenda mahakamani kumshtaki Prof. Lipumba na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kutokana na mgogoro unaoendelea ndani ya Chama cha Wananchi (CUF).


Katika kikao walichofanya jana, UKAWA walipitisha maazimio kukabiliana na mgogoro unaoendelea ndani ya CUF. Maazimio hayo ni pamoja na;-
  1.  Hatumtambui Prof. Lipumba kama mwanachama wa CUF na Mwenyekiti mwenza wa UKAWA
  2.  UKAWA wanautambua uongozi wa Julius Mtatiro na Maalim Seif
  3.  Wanachama wa vyama vinavyounda UKAWA wasitoe ushirikiano kwa Prof. Lipumba na washirika wake
  4.  Wenyeviti wa mitaa, vijiji, Madiwani, Wabunge wasitoe ushirikiano kwa Prof. Lipumba na washirika wake
  5.  Wabunge wote wanaomuunga mkono Prof. Lipumba  watatimuliwa ndani ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
  6.  Ushirikiano wa kisiasa Tanganyika na Zanzibar utashughulikiwa na UKAWA
  7.   Mawakili wa UKAWA watamfunguliwa mashtaka Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kwa matumizi mabaya ya madaraka na
  8.  Mawakili wa UKAWA watamfungulia mashtaka Prof. Lipumba.
Kwa upande wake Prof. Lipumba aliwataka wanachama wa CUF kuwa wamoja na kusema kuwa yeye hajali kuhusu UKAWA kikubwa anachoangala ni kuijenga upya CUF.

Majina ya Wakurugenzi wa CUF ambao uteuzi wao umetenguliwa na Prof. Lipumba


Kila kukicha mgogoro ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) unazidi kuchukua sura mpya. Jana viongozi wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi wamekutana kujadili mgogoro wa CUF sababu ni moja ya vyama vinavyounda UKAWA.

Viongozi wa UKAWA jana wametangaza kuwa hawamtambui Prof. Lipumba kama mwenyekiti wa CUF na kuwa wao watashirikiana na viongozi halali wa CUF, na kutilia maanani maazimio yaliy0pitishwa katika vikao halali vya CUF.
 Aidha, mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe amewataka viongozi wa chama hicho nchini kote kumpuuza na kutompa ushirikiano Prof. Lipumba kwani ni msaliti.

Kwa upande wake yeye, Prof. Lipumba ameendelea kutekekelza majukumu yake kama Mwenyekiti wa CUF ambapo jana ametangaza kutengua uteuzi wa Wakurugenzi na Manaibu Wakurugenzi wa Idara mbalimbali za Chama cha Wananchi (CUF).

Wakurugenzi na Manaibu Wakurugenzi ambao uteuzi wao umetenguliwa ni pamoja na;-
  1.  Joran Bashange – Mkurugenzi wa Uchumi na Fedha
  2.  Ismail Jussa- Mkurugenzi wa Mambo ya Nje
  3.  Mustafa Wandwi- Mkurugenzi wa Kamati ya Ulinzi na Usalama
  4.  Kurufumu Mchuchuli- Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Sheria
  5.  Shaweji Mketo- Naibu Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi na
  6.   Abdalla Mtolea- Naibu Mkurugenzi wa Mambo ya Nje
Aidha Prof. Lipumba amesema kuwa hajali kama viongozi wa UKAWA wanamtaka au hawamtaki kwani yeye anachojali ni kuijenga CUF.

Thursday, September 1, 2016

Mapokezi ya Waziri Mkuu Mjini Dodoma Yaahirishwa Hadi Vikao vya Bunge Viishe

SERIKALI Mkoa wa Dodoma imesema Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa atahamia rasmi mkoani humo mara baada ya kumalizika kwa vikao vya Bunge vinavyoanza wiki ijayo, Septemba 6.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana alisema baada ya kufika Dodoma, ataanza kuratibu utaratibu wa wizara mbalimbali kuhamia katika Makao Makuu hayo ya nchi.

Pamoja na hayo Jeshi la Polisi limejipanga kuongeza vituo vya Polisi ili kuimarisha ulinzi wakati serikali itakapohamia na hakuna mwananchi atakayenyang’anywa ardhi yake kwa sababu yoyote ile.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana, Rugimbana alisema kama mkoa walishauri ujio huo ufanyike mara baada ya kikao cha Bunge na Waziri Mkuu ameridhia suala hilo.

Alisema Waziri Mkuu atakuwa Mratibu wa wizara zote kuhamia Dodoma na kazi hiyo ataianza rasmi mara baada ya kuwasili mkoani humo.

Alisema maandalizi yanaendelea vizuri na ukarabati wa nyumba ya Waziri Mkuu umefikia asilimia 90.

Alisema Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Christine Mndeme aliyekutana na makundi mbalimbali kwa ajili ya mapokezi ya Waziri Mkuu.

“Awali tulisema atakuja Septemba Mosi lakini baada ya kushauriana tumeona aje mara baada ya vikao vya Bunge kwani pilikapilika nyingi zitakuwa zimepungua, kama serikali ikiamua kuja leo tutaipokea kwani maandalizi ya serikali kuja Dodoma yamekamilika kwa asilimia 70,” alisema.

UVCCM yaivaa rasmi Chadema kwa kushindwa kufanya Maandamano ya UKUTA

Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), umewavaa viongozi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa kile walichodai kuendesha siasa za maigizo baada ya kushindwa kuzindua Operesheni UKUTA, Septemba 1.

Kupitia taaria yake kwa vyombo vya habari, Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, amesema kuwa Chadema walijua kuwa hawana ubavu wa kufanya maandamano na mikutano nchi nzima Septemba 1 na kwamba walichofanya ni kuwatia hofu wananchi.

“UVCCM tulijua, tulielewa na kutambua bayana kwamba Chadema walikuwa wanafanya maigizo katika siasa, hawana ubavu wala jeuri ya kuandamana kwa madai ya kipuuzi na ambayo sio ya msingi kwa mustakabali wa nchi yetu,” alisema Shaka.

Aidha, Shaka alikanusha sababu zilizotolewa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kuahirisha maandamano hayo kuwa wameombwa na viongozi wa dini ili waweze kukaa na pande zote kujaribu kutafuta suluhu kwa amani.

“UVCCM inatamka bayana kuwa hakuna majadiliano, mazungumzo wala mijadala itakayojadiliwa kati ya Serikali ya CCM na Chadema. Tunaomba Serikali ya Rais John Magufuli iendelee na mikakati yake ya kisera,” Shaka ameongeza.

Kaimu Katibu Mkuu huyo wa UVCCM alisisitiza kuwa Chadema hawana ubavu wa kufanya maandamano na mikuano nchi nzima Oktoba 1 kama walivyosema, baada ya kushindwa kufanya hivyo Septemba 1.

Shaka amesema wanachokifanya hivi sasa Chadema kinatokana na kushindwa kubuni mikakati ya kufanya siasa ili chama chao kiimarike na kukubarika.

Juzi, Chadema walitangaza kuahirisha uzinduzi wa oparesheni UKUTA nchi nzima, iliyokuwa imepangwa kufanyika jana (Septemba 1) kwa maandamano na mikutano nchi nzima.

UVCCM pia walitangaza kuahirisha maandamano yao ya nchi nzima waliyokuwa wamepanga kuyafanya Agosti 31 kwa lengo la kumpongeza Rais Magufuli kwa kazi aliyoifanya ndani ya kipindi kifupi.

Maandamano ya pande zote mbili yalipigwa marufuku na Jeshi la Polisi nchini.

Rais Magufuli amuapisha Bw. Doto M. James kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli,  tarehe 01 Septemba, 2016 amemuapisha Bw. Doto M. James kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
 
Bw. Doto M. James aliteuliwa kushika wadhifa huo jana tarehe 31 Agosti, 2016 na amechukua nafasi iliyoachwa wazi na Dkt. Servacius Likwelile ambaye atapangiwa kazi nyingine.
 
Kabla ya uteuzi huo, Bw. Doto M. James alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango (Sera).
 
Hafla ya kuapishwa kwa Bw. Doto M. James imehudhuriwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa.
 
Aidha, Bw. Doto M. James amekula kiapo cha Uadilifu kwa Viongozi wa Umma, zoezi ambalo limeongozwa na Kamishna wa Maadili Jaji Mstaafu Salome Kaganda.

 Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es salaam
01 Septemba, 2016

Cheyo: Rais Magufuli ni Rais aliyesubiriwa tangu kuanza kwa uhuru


Na: Lilian Lundo-Maelezo
Mwenyekiti wa Chama cha UDP John Cheyo amesema kuwa Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli ni Rais aliyesubiriwa kwa muda mrefu tangu kuanza kwa Uhuru.

Cheyo ameyasema hayo alipokuwa akielezea juu ya utendaji wa Rais Magufuli tangu ameingia madarakani Novemba, 2015.

“Utendaji wa Rais Magufuli umewashtusha watu wengi kwani hawakutegemea kwa muda mfupi aliokuwa madarakani kama angeweza kuchukua hatua kubwa kama vile kupambana na mafisadi, jambo ambalo limekuwa likiongelewa na viongozi waliopita lakini kulikuwa hakuna matunda ya moja kwa moja,” alifafanua Cheyo.

Ameendelea kwa kusema kuwa Rais Magufuli amekuwa na adhima ya kupambana na Mafisadi na kutatua kero za Taifa tangu akiwa kwenye kampeni huku akisimamia kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu.

Vile vile Cheyo amesema kuwa kero ambazo amekuwa akizitatua Rais Magufuli zikiwemo ufisadi, uchumi tegemezi, mapato madogo na ukosefu wa vifaa mahospitalini ni kero ambazo zimekuwa zikipigiwa kelele na kambi ya upinzani kwa muda mrefu.

Hivyo kuingia kwa Rais Magufuli madarakani kumeleta utatuzi mkubwa kwa kero hizo ambazo zimekosa utatuzi kwa muda mrefu kutokana na viongozi waliopita kutozichukulia uzito mfano Rais Magufuli alivyoweza kutatua tatizo la vitanda hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa kipindi kifupi ambapo hivi sasa hakuna mgonjwa anayelala nchini katika hospitali hiyo.

Akielezea suala la ufisadi nchini, Cheyo amesema kuwa ufisadi ni ugonjwa wa muda mrefu ambao umepoteza fedha nyingi za nchi kutokana na mikataba mibovu iliyokuwa ikisainiwa na viongozi wa juu.

Aidha amempongeza Mhe. Rais kwa kuanzisha Mahakama ya Mafisadi na kuona tatizo hilo lishughulikiwe kisheria na kwa njia maalum ili kukomesha ufisadi nchini.

Cheyo amewataka watanzania kugeuza mawazo yao na kuchukia rushwa kwa kukataa kupokea na kutoa rushwa kwani rushwa ni adui wa haki na inarudisha nyuma maendeleo ya nchi.

Msajili amlima Barua Maalim Seif kuhusu sakata la Lipumba


Ofisi ya Msajili wa Vyama vya siasa nchini imemuandikia barua Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad kufuatia mvutano wa kusimamishwa uanachama aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya Profesa Lipumba kumuandikia barua Msajili wa vyama vya siasa nchini, Jaji Francis Mutungi akilalamikia kusimamishwa uanachama bila kufuata utaratibu huku akitaka kurejeshwa kwenye nafasi yake ya uenyekiti.

Ofisi hiyo imeutaka uongozi wa CUF kueleza kwa kina hatua ilizopitia hadi kufikia uamuzi huo kwa mujibu wa katiba ya chama hicho, na kwamba iwasilishe barua hiyo kufikia kesho majira ya saa 9:30 alasiri.

Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano cha Ofisi ya Msajili wa Vyama Vya Siasa, Monica Laurent amesema kuwa ofisi hiyo ilipokea barua ya Profesa Lipumba Agosti 29 mwaka huu ikiwa na malalamiko na kwamba wametaka uongozi wa CUF kutolea majibu.

“Tumeitaka CUF kutoa majibu kuhusu malalamiko ya Profesa Lipumba, ndipo sisi tutakapotoa majibu,” amesema Monica.

Lipumba ambaye alijiuzulu nafasi yake ya Uenyekiti mwaka jana akipinga uamuzi wa chama chake kumuunga mkono Edward Lowassa kugombea urais, amerejea na kudai kutengua barua yake ya kujiuzulu.

Baraza Kuu la CUF lililoketi visiwani Zanzibar hivi karibuni lilimsimamisha uanachama Profesa Lipumba pamoja na viongozi wengine 10 akiwemo Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya aliyekuwa Naibu Katibu mkuu (Bara).

Hata hivyo, Profesa Lipumba amepinga uamuzi huo akieleza kuwa kikao cha baraza hilo kililiwa batili.

Wednesday, August 31, 2016

Rais Magufuli apongezwa kwa kupambana na rushwa na kujenga mazingira bora zaidi kwa uwekezaji nchini

 
Mwenyekiti wa Taasisi inayoshughulikia masuala ya Afrika (Africa Matters Limited) Mhe. (Baroness) Lynda Chalker wa Wallasey - Uingereza, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa juhudi kubwa alizozifanya kupiga vita rushwa na kujenga mazingira bora zaidi kwa uwekezaji.

Mhe. Lynda Chalker ametoa pongezi hizo jana tarehe 31 Agosti, 2016 Ikulu Jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais Magufuli kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo hali ya uwekezaji hapa nchini.

"Mhe Rais amefanya uamuzi sahihi wa kupiga vita rushwa na kuiweka nchi hii katika njia mpya ya uwekezaji mzuri na hicho ndicho tumekuwa tukikizungumza, nimejitahidi kutoa ushauri wangu wa namna mimi na kampuni yangu binafsi tunaweza kumsaidia, nionavyo mambo yanakwenda katika mwelekeo mzuri" Amesema Mhe. Lynda Chalker.

Kwa Upande wake Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Lynda Chalker kwa ushauri na dhamira yake ya kutaka Tanzania ipige hatua kimaendeleo na amemuomba kutumia ushawishi wake kuwahamasisha wawekezaji mbalimbali kutoka nchini Uingereza na kwingineko duniani kuja kuwekeza nchini Tanzania ili kuharakisha zaidi maendeleo.

Hata hivyo Dkt. Magufuli amesema wawekezaji wanaokuja Tanzania hawana budi kuwa wawekezaji makini.

"Ninawakaribisha wawekezaji makini kutoka Uingereza na mahali popote dunia, lakini nisingependa kupata wawekezaji wababaishaji" Amesisitiza Rais Magufuli.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es Salaam
31 Agosti, 2016

Lowassa, Mbowe Watakiwa Kuripoti Polisi Keshoi Septemba 1

 
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama hicho, Edward Lowassa na viongozi wengine waandamizi wameitwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwenda kuripoti kesho Septemba Mosi.

Hatua hiyo inatokana na viongozi hao kukamatwa juzi, baada ya kufanya mkutano maalumu wa ndani wa Kamati Kuu, na walipelekwa Kituo Kikuu cha Polisi cha Kanda hiyo na kuhojiwa kabla ya kuachiwa.

Mbali na Mbowe na Lowassa, viongozi wengine wa Chadema waliokamatwa na kutakiwa kwenda Polisi kesho ni Katibu Mkuu, Vincent Mashinji, Naibu wake, John Mnyika na Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho, Said Issa Mohammed.

“Wameitwa Polisi waende Septemba mosi kuripoti baada ya jana kukamatwa na kuhojiwa wakituhumiwa kukiuka maagizo ya Polisi,” alisema Msemaji wa Chadema, Tumaini Makene na kufafanua:

“Lakini wanaweza kwenda au wakaanzia kwenye maandamano kisha wakaenda Polisi kuripoti.”

Alisema maandamano hayo yatakuwapo kama yalivyopangwa kwani maandalizi yake yamekamilika.

Habari zaidi zilieleza, kwamba jana mchana viongozi hao walikuwa wakifanya kikao Makao Makuu ya chama hicho Kinondoni Dar es Salaam, ambapo pia walikutana na wabunge wote wa chama hicho kwa makundi tofauti.

Kwa mujibu wa mtoa habari ndani ya Chadema makao makuu katika kikao hicho walijadili mambo mengi ikiwa ni pamoja na suala la utekelezaji wa Ukuta kesho.

Mmoja wa wabunge wa Chadema alisemai kwamba walikuwa wakiwekana sawa kuhusu maandamano yao.

Alibainisha kwamba katika mkutano huo ambao Mbowe hakuwepo pia walijadili maombi ya viongozi wa dini kuwataka kusitisha maandamano hayo Septemba mosi.

“Viongozi wa dini wamekuwa wakituomba tusitishe maandamano ya Ukuta Septemba mosi, tusubiri hadi baada ya mkutano wa vyama vya siasa Septemba tatu,” alisema Mbunge huyo wa Kanda ya Ziwa.

Aliongeza: Katika mkutano huo, Lowassa na viongozi wengine walijadili hayo na ikikubalika kwa heshima ya viongozi wa dini maandamano ya Ukuta yafanyike baada ya Septemba tatu.”

Hata hivyo, mwandishi alishuhudia wabunge wengi wa chama hicho wakitoka katika mkutano huo kimya kimya bila kutaka kuzungumza na kabla muda uliopangwa kwisha, huku taarifa zikieleza kwamba mkutano huo uliahirishwa baada ya kuwepo taarifa za kutaka kuvamiwa na Polisi.

“Tumeambiwa tusambaratike, tutajulishwa wapi tutakutana tena, kama hapa au wapi,” alidokeza mmoja wa wabunge hao.

Baada ya mkutano huo kuahirishwa, Lowassa alitoka eneo hilo huku taarifa zikieleza alikuwa akielekea kwenye moja ya hoteli jijini humo kuungana na Mbowe ambapo walikuwa na mazungumzo na baadhi ya viongozi wa dini.

Lowassa Aandika Waraka Mzito Kuhusu Oparesheni UKUTA.....Asimulia Kilichomfanya Akutane na Rais Magufuli

 
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa ameandika barua kuhusu operesheni ya chama chake iliyopewa jina la Ukuta na jinsi ambavyo jeshi la Polisi na Serikali lilivyopanga ‘kuubomoa’.

Katika waraka huo, Lowassa ameeleza kuwa ameamua kushika kalamu na kuandika masikitiko yake kuhusu hali ya amani nchini akidai Serikali imekata mkono wa amani.

Ameeleza kuwa Serikali imekandamiza upinzani na demokrasia na ndio chanzo cha wao kuanzisha UKUTA kupinga ukandamizaji huo.

“Binafsi nafurahishwa na kutiwa moyo na jinsi watanzania walivyoipokea Operesheni hii, pamoja na vitisho vya dola,” ameandika. “Siku zote sisi Chadema na Ukawa kwa ujumla ni wenye kulitakia amani na utulivu Taifa letu. Maandamano haya ya Septemba 1 ni ya amani, lakini vitendo vya jeshi la polisi vimewapa wasiwasi Watanzania,” Lowassa ameongeza.

Katika andiko hilo, Lowassa amedai kuwa amekuwa akipigiwa simu na viongozi wastaafu pamoja na watu mashuhuri wakimshauri kushawishi wakae na Serikali kuzungumza ili kuepusha taifa kujiingiza katika machafuko. Aliongeza kuwa kukutana na Rais John Magufuli katika Jubilee ya miaka 50 ya ndoa ya Rais Mstaafu, Benjamini Mkapa ni sehemu ya juhudi hizo.

“Nyote ni mashahidi wa tukio la kukutana na Rais Magufuli katika Jubilei ya miaka 50 ya ndoa ya mzee Mkapa. Ulikuwa ni mwanzo wa juhudi zetu za kuwanyooshea mkono wa amani. Lakini tunashangazwa wenzetu hawako tayari kuupokea mkono huo,” ameandika.

Aliongeza kuwa katika kikao cha juzi cha ndani cha chama hicho kilichofanyika katika Hotel ya Giraffe jijini Dar es Salaam walipanga kuzungumzia jinsi ya kuunyosha zaidi mkono wa amani lakini Jeshi la Polisi ‘liliukata’.

“Kitendo kile kwangu binafsi kimezidi kuniimarisha na kunipa nguvu zaidi ya kudai demokrasia na kuheshimu katiba ambayo viongozi wetu waliapa kuifuata na kuitetea,” unasomeka waraka wa Waziri Mkuu wa zamani, Lowassa.
 

Tuesday, August 30, 2016

Serikali Kutoa Ajira Mpya 71,496 Hivi Karibuni

 
SERIKALI imeanza kuwashughulikia watumishi walionufaika na fedha za watumishi hewa ambapo hadi sasa watumishi 839 wapo katika hatua mbalimbali wakiwemo waliofikishwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na wengine wanaendelea kuhojiwa polisi kwa ajili ya kufikishwa mahakamani.

Sambamba na hilo, serikali inatarajia kutoa ajira mpya 71,496 kwa mwaka huu wa fedha baada ya kukamilisha uondoaji wa wafanyakazi hewa. 
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Angella Kairuki aliyasema hayo wakati akizungumzia utekelezaji wa mipango na mikakati ya wizara yake katika kipindi cha ‘Tunatekeleza’ kinachorushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1). Kairuki alisema,

“Kwa sasa tayari wapo watumishi wameshahojiwa na kuchukuliwa maelezo yao polisi na upelelezi utakapokamilika watachukuliwa hatua mbalimbali za kisheria, ikiwemo kufikishwa mahakamani… Tunakamilisha ushahidi na tutawatangazia tutakapokamilisha,” alisema.

Alisema waligundua kwamba kuna maofisa utumishi na wahasibu ambao siyo waaminifu, badala yake walikuwa wakielekeza fedha kwa ndugu zao na miradi yao na wengine walishastaafu lakini bado majina yao yalikuwa yakiendelea kupokea mishahara wakati walitakiwa kuondolewa kwenye mfumo.

Alisema kwa kipindi cha Machi mosi hadi Agosti 20 mwaka huu, watumishi hewa waliogundulika ni zaidi ya 16,127 na kuisababishia serikali hasara ya mabilioni ya fedha. Kwa kipindi cha Agosti pekee watumishi hao hewa wangelipwa mishahara wangeisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh bilioni 16.

“Uhakiki huu ni endelevu na tumegundua changamoto kubwa katika usimamizi wa mishahara ni uadilifu kwa watu waliokasimiwa madaraka. Maofisa Utumishi, Maofisa Utawala na Wahasibu wamepewa madaraka lakini wengi wao siyo waaminifu, hivyo kwa sasa tumeweka uwajibikaji kwa waajiri,” alisema.

Aidha alisema wanaufanyia mfumo wao maboresho zaidi ili uweze kuchakata taarifa nyingi zaidi ambapo pia sekta ya mishahara imeshushwa katika ngazi za chini zaidi hasa katika sekta za elimu na afya ambazo zimekutwa na watumishi hewa wengi zaidi ili waweze kuwa na taarifa za mtumishi mmoja mmoja.

Alisema upo muongozo ambao fedha za serikali zinaporejeshwa zinapitia hazina na kusisitiza kwamba wataendelea kuhakikisha wanasimamia fedha zote ambazo zilichukuliwa serikalini kinyume na utaratibu na isivyo halali zinarudishwa kwa mfumo sahihi.

Pia alisema wameongeza kasi ili kuhakikisha kunakuwa na nidhamu ya kazi na uwajibikaji kwa watumishi wa umma, hivyo wanaanda mkataba wa utendaji kazi kwa watumishi wa umma na ikiwezekana utaanza kutumika mwaka ujao wa fedha.

Alisema serikali imefanya maboresho makubwa katika mishahara na motisha kwa ajili ya maslahi ya watumishi wa umma, sambamba na kuhimiza taasisi mbalimbali kuweka vitendea kazi ili kuwawezesha wafanyakazi kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Akizungumzia ajira hizo mpya Kairuki aliwatoa hofu watanzania waliokuwa wanatarajia ajira serikalini na kusisitiza kwamba walichokuwa wanasubiri ni takwimu halisi kwa taasisi ili kujua ni watumishi wangapi wameondolewa.

“Baada ya kukamilisha mchakato huo, hatua nyingine zitaendelea… Hii ni neema kwa waliomaliza vyuo, cha msingi wavute subira maana tutatoa ajira 71,496 kwa mwaka huu wa fedha na hatukuzifuta ajira. 
"Nawashauri vijana wasijiingize kwenye makundi yasiyofaa wasubiri ajira zinakuja,” alisema. 
Katika hatua nyingine, Kairuki alisema, wamepokea malalamiko zaidi ya 200 kutokana na ukiukwaji wa sheria ya maadili ya viongozi wa Utumishi wa Umma ambayo inamnyima mtumishi kutotumia madaraka yake vibaya.

“Katika malalamiko hayo 142 yanahusu sheria ya maadili. Sekretarieti ya Maadili imefanya uchunguzi wa awali na malalamiko 12 yataanza kufikishwa Baraza la Maadili na hatua mbalimbali zinaweza kuchukuliwa ikiwemo kushushwa vyeo au kuachishwa kazi,” alisema.

Pia aliwaagiza maofisa utumishi kuwahudumia watumishi na kuwapa haki zao ikiwemo kuwapandisha madaraja kwa wakati pale wanapostahili. Aidha Kairuki alikemea tabia ya baadhi ya watu kughushi taarifa za utumishi wa umma na kusisitiza kwamba jambo hilo ni kosa kubwa kwa yeyote anayefanya hivyo.

“Mtu yeyote ambaye anatoa nyaraka za serikali na siyo mlengwa au anayetoa nyaraka ambayo imewekewa zuio kwa mujibu wa sheria ni kosa la jinai na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake. Tunawasisitiza watumishi wa umma kuhakikisha wanazingatia sheria hizo na mwongozo wa utoaji nyaraka na kumbukumbu za taarifa za serikali,” alisema.

UVCCM Waahirisha Maandamano Yao,watii Agizo La Jeshi La Polisi


Agosti 22, 2016 Umoja wa Vijana wa CCM tuliutangazia umma na dunia kwamba ifikapo Agosti 31 mwaka huu tutaitisha maandamano ya amani nchi nzima yenye lengo la kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk John Pombe Magufuli kwa utendaji wenye tija, ufanisi na uliorudisha imani na matumaini kwa wananchi.

Msimamo na dhamira ya kufanya maandamano hayo ya amani yenye maudhui na kusudio hilo, bado uko pale pale ingawaje si kwa tarehe tuliopanga na kutangaza awali yaani Agosti 31 mwaka huu.

Jumuiya yetu kama mjuavyo ni ya Vijana wa CCM, (UVCCM) inapata malezi kwa karibu mno na Jumuiya ya Wazazi ya CCM. Wiki ya jana Mwenyekiti wa Wazazi Taifa Nd. Abdallah Bulembo alikutana na waandishi wa habari akitutaka UVCCM tuahirishe maandamano ya Agosti 31 mwaka huu hadi wakati mwingine.

Kwa mujibu wa Katiba ya Chama Cha Mapinduzi, Jumuiya ya Wazazi ndiyo Msimamizi wa Malezi, Maadili na Adabu kwa Vijana wote nchini, sisi UVCCM tunaamini kuwa sikio halishindani na kichwa, mtoto ni mtoto kwa Wazazi wake hakui, hana jeuri wala ubishi.

Mtoto au watoto wanaokaidi amri, ushauri au maelekezo ya Wazazi wao huitwa watukutu, wenye viburi, manunda na wasioambilika. UVCCM si watukutu, hatukufunzwa tuwe wabishi, wakaidi na wenye viburi. Tumezingatia kutii maelekezo, makatazo na maonyo , tumeambiwa tuahirishe maandamano yetu nasi tumekubali na kuheshimu mambo tuliyoaswa.

Sambamba na hilo tumepata majibu ya barua yetu tuliyomwandikia Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP Ernes Mangu) inayotutaka tuache kufanya maandamano yetu kwa sababu Polisi wamezuia mikutano ya hadhara ya Vyama vya Siasa na maandamano nchi nzima.

Jambo jingine ambalo limetufanya pia tuahirishe maandamano yetu ya Amani ni taarifa ya kintelejinsia iliowasilishwa na Kamati yetu ya Usalama na Maadili ya UVCCM mbele ya kikao cha Sekreteriet yetu, nayo ilipendekeza  suala hilo liahirishwe kwa wakati huu hadi muda mwingine.

Pia jambo jingine ambalo limefanya maandamano hayo tuyabatilishe ni kulipisha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ ) ambalo litakuwa katika shughuli za maadhimisho miaka 52 tokea kuanzishwa kwake.

Wanajeshi wetu watakuwa katika kazi mbalimbali za kijeshi kwenye kambi zao na mitaani kufanya usafi wa mazingira, hivyo isingependeza na wala si heshima wakati sisi tukiandamana, wao wakifanya kazi muhimu kila mmoja wetu zinazomgusa badala yake ni vyema kuwaunga mkono jambo wanalolifanya la usafi wa mazingira.

UVCCM tumekubali, hatutaki kuingia katika uvunjaji wa sheria hasa baaada ya kutakiwa kuahirisha na mamlaka za Kisheria hadi wakati mwingine muafaka na si wakati huu.

Tunaelewa kwamba uamuzi wetu wa awali wa kutaka kuandamana kwa amani hata kama tungenyimwa kibali ungetugharimu, ungetusababishia madhara na pengine hasara, kwa wakati huu na kuona jambo lenyewe ni la kuipa Ari serikali katika kuhimiza Uwajibikaji, Utendaji na Usimamizi bora wa Uendeshaji wa masuala ya kiutawala.

Tulishusha maagizo kwa Makatibu wetu wote wa Mikoa yote 32 na Wilaya 171 ya Kichama tukiwataka waandike barua katika Ofisi za Ma RPC na OCD, washirikiane ili kuratibu maandamano na kuyafanikisha kama tulivyokusudia.

Watendaji wetu wa ngazi husika wamefuata maelekezo, wametii taratibu zetu za kiutendaji na leo tumewajulisha tena wasitishe maandamano hadi tutakapowapa tena maelekezo mengine. Tunawahimiza na kuwataka ni vyema kutii mamlaka za Kikanuni na Kisheria.

UVCCM kwa wakati huu tumeamua kuachana na maandamano badala yake tunajikita katika matayarisho ya kuwapeleka Vijana wetu wakashiriki katika Mafunzo ya Siasa, Utawala, Uongozi, Ufundi na Ujasiriamali yatakayoanza kufanyika katika Chuo chetu kilichopo huko Ihemi Mkoani Iringa ambapo kitakuwa kielelezo na alama nzuri ya kumuunga mkono Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli kwa vitendo.

Tumewataka Makatibu wetu wa Mikoa na Wilaya kuendelea na zoezi la Uratibu na Uhakiki kwa Vijana ambao watateuliwa kushiriki Mafunzo hayo huko Ihemi.

UVCCM tunarejea kusema tena kwamba dhamira ya maandamano yetu ya kusifu Utendaji wa Serikali ya awamu ya tano iko pale pale ila tutapanga tarehe nyingine katika wakati ujao badala ya kufanyika Agosti 31 mwaka huu kama tulivyotangaza hapo awali.

UVCCM tunawataka Vijana wote kuendelea kuheshimu Tunu ya Amani Umoja na Mshikamo wetu kwa Taifa.


KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
Shaka Hamdu Shaka (MNEC)
KAIMU KATIBU MKUU.

Wakili Apinga Tundu Lissu Kusomewa Mashitaka Mapya........ Hakimu aahirisha kesi hadi mwezi ujao

Upande wa Jamhuri katika kesi inayomkabili Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu na wahariri wa Gazeti la Mawio iliyopo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu umeshindwa kuwasomea washtakiwa hao mashtaka mapya baada ya wakili anayewatetea, Peter Kibatala kudai kuwa yaliyofutwa yamerudishwa kwa ‘staili’ tofauti. 
Hatua hiyo ilifikiwa baada ya Kibatala kuwasilisha hoja mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba za kupinga washtakiwa hao kusomewa mashtaka hayo mapya. 
Wakili wa Serikali Mkuu, Kishenyi Mutalemwa aliwasilisha maombi mahakamani hapo akiomba kuwasomea hati mpya ya mashtaka washtakiwa hao na Mahakama iliipokea na kuruhusu isomwe, lakini Wakili Kibatala alipinga kwa madai kuwa hayatofautiani na yale yaliyofutwa Juni 28, 2016.
Kibatala alidai katika hati mpya shtaka la kwanza na la tano ni sawa na yale yaliyokuwamo kwenye hati iliyofutwa mahakamani hapo baada ya kupingwa na kuonekana hayakustahili kwa mujibu wa sheria. 
Baada ya Kibatala kuwasilisha hoja hizo, Wakili Kishenyi aliiomba Mahakama hiyo kuiahirisha kesi hiyo kwa muda ili aweze kujibu hoja zilizotolewa na upande wa utetezi na hakimu aliridhia na kuiahirisha hadi saa sita mchana. 
Ilipofika mchana, Kishenyi alidai shtaka la kwanza na la tano ni kama hayakuwapo mahakamani na kwamba kufutwa kwake haikatazwi kuyarudisha tena na mashtaka hayo ya awali yalifunguliwa bila ya kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), lakini hivi sasa yamerudishwa yakiwa na kibali hicho. 
Kuhusu kukata rufaa, Kishenyi alidai wanakata rufaa kwenye kesi ambayo ilisikilizwa na kumalizika. Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Hakimu Simba aliiahirisha kesi hiyo na kuwa atatoa uamuzi wa hoja hizo mwezi ujao. 
Washtakiwa wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Mhariri wa gazeti hilo, Simon Mkina, Jabir Idrisa, Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob na Lissu ambao kwa pamoja walikuwa wanakabiliwa na mashtaka matano yakiwamo ya kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002

Madiwani Watatu wa Chadema Wafikishwa Mahakamani Kwa Kuhamasisha Maandamano ya UKUTA

Madiwani watatu wa Chadema na mfuasi mmoja wa chama hicho wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Rombo kwa makosa ya kufanya uchochezi. 
Madiwani hao, Nicolaus Kimario (Kirio), Anasia Kimario (Viti Maalumu), Daud Tarimo (Leto ) na mfuasi wa Chadema, Rogath Kanje walikana mashtaka hayo. 
Mwendesha mashtaka, Bernard Machivya alieleza mahakama kuwa washtakiwa walitenda kosa hilo Agosti 25, wakiwa nyumbani kwa mmoja wa washtakiwa Nicolaus Kimario. 
Aliieleza Mahakama kuwa washtakiwa wote wanne walitenda kosa hilo kwa pamoja wakifanya vikao vya kuhamasisha wananchi wajitokeze kwenye maandamano ya Ukuta Septemba Mosi. 
Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Rombo, Naomi Mwerinde aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 5 na watuhumiwa wote wataendelea kukaa rumande.

Monday, August 29, 2016

Lowassa, Mbowe Watakiwa Kuripoti Polisi Leo

Viongozi waandamizi wa Chadema akiwamo Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa jana walikamatwa na Jeshi la Polisi wakati wakiwa katika kikao cha ndani katika Hoteli ya Giraffe mkoani Dar es Salam

Lowassa, ambaye alikaa kituoni hapo kwa takribani saa tatu anaweza kuwa kiongozi wa kwanza aliyewahi kushika nafasi ya Waziri Mkuu kuhojiwa na polisi.
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu aliwataja viongozi wengine waliokamatwa kuwa ni Mwenyekiti, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu, Dk Vincent Mashinji, Naibu Katibu Mkuu Bara, John Mnyika na Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Said Issa.

Mara baada ya kukamatwa, walipelekwa katika Kituo Kikuu cha Polisi ambako baadhi ya wajumbe na wabunge waliwafuata na kuwasubiri nje ya kituo hicho kujua hatima yao. 
Viongozi hao walionekana wakiingia Polisi saa 10.30 jioni na kutoka saa 1.25 usiku, jambo ambalo liliwafanya wakae kituoni hapo kwa saa tatu. 
Lissu alisema polisi walivamia kikao hicho kilichokuwa na wajumbe 170, wakiwamo baadhi ya wabunge wa chama hicho na kuwakamata viongozi hao kwa maelezo kuwa wamekaidi amri ya Jeshi la Polisi ya kuzuia mikutano ya ndani na nje ya vyama vya siasa. 
Imeelezwa kuwa viongozi hao wa Chadema walikuwa na mkutano uliotanguliwa na kikao cha viongozi wakuu na kufuatiwa na cha viongozi hao kikijumuisha wabunge, mameya na wenyeviti wa halmashauri. 
Wakiwa katika kikao hicho, ilielezwa kuwa watu wanne waliingia wakiwa wamevalia kiraia na kuwaeleza kuwa viongozi wao wanahitajika kituo kikuu cha polisi kutokana na kufanya mkutano kinyume cha sheria. 
Mbunge wa Viti Maalumu, Upendo Peneza ambaye  alikuwa kwenye mkutano huo alisema pamoja na mambo mengine ya chama, walikuwa wakijadili suala la operesheni Ukuta la Septemba Mosi kama liendelee au lisiendelee kutokana na hali ilivyo.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro alipoulizwa kuhusu kukamatwa kwao, alisema viongozi hao walikamatwa kwa kukukaidi amri ya polisi ya kuzuia mikusanyiko ya kisiasa na kuchochea wananchi kuandamana kinyume cha sheria Septemba Mosi. 

Alisema baada ya kuachiwa kwa dhamana, viongozi hao wametakiwa kuripoti kituoni hapo leo. 
Wiki iliyopita, Jeshi la Polisi kupitia kwa Kamishana wa Operesheni na Mafunzo, Nsato Marijani lilipiga marufuku mikutano ya ndani likisema inatumika kuhamasisha watu kuvunja sheria za nchi na kupambana na askari. 

Hatua hiyo ilikuja huku jeshi hilo likiwa limepiga marufuku mikutano ya hadhara na maandamano kufuatia uamuzi wa Rais John Magufuli kuzuia shughuli  za kisiasa hadi 2020.