Adverts

Friday, October 7, 2016

Zitto Kabwe Awamwagia Sifa UKAWA ......Atia Neno Kuhusu Mgogoro wa CUF


Kiongozi Mkuu wa Chama Cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ameisifia nguvu ya vyama vya siasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwa kile walichokifanya hasa katika uchaguzi wa mwaka jana.
 
Akizungumza jana katika mahojiano maalum na kituo cha runinga cha Clouds TV, Zitto alisema kuwa chama chake hakiwezi kubeza nguvu kubwa iliyooneshwa na umoja huo na kwamba uliweka historia katika chaguzi zote zilizowahi kufanyika nchini.
 
“Ukawa umeweka historia Kubwa zaidi katika chaguzi za nchi yetu japo kuwa kuna madhaifu ila hatuwezi kupuuza nguvu ile,” alisema Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini.
 
Hata hivyo, pamoja na kusifu nguvu ya muungano huo wa hivyo vya siasa ambavyo ni Chadema, Chama Cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na NLD, Zitto alisisitiza kuwa chama chake hakitajiunga na umoja huo kutokana na maazimio na miiko waliyoiweka katika Azimio la Tabora la chama chake.
 
“Hatukuweza kujiunga na Ukawa kwasababu tuliweka kanuni zetu wazi  tulizozitangaza katika azimio la Tabora,” Zitto anakaririwa.
 
Katika hatua nyingine, Zitto alizungumzia mgogoro wa uenyekiti wa CUF unaoendelea ndani ya chama hicho na kutoa rai kwa vyama vingine vya siasa kutowafarakanisha.
 
Alisema kuwa CUF inapaswa kuachiwa suala hilo walimalize wenyewe katika vikao vyao vya ndani ya chama na sio vinginevyo. 

Aliongeza kuwa kutokana na mgogoro unaoendelea ndani ya CUF, hivi sasa ajenda yao kubwa [kupinga kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa Oktoba]imewekwa kando bali sasa wanatafuta uhalali wa kiongozi wa chama hicho.
 
“Rai yangu tusichochee kabisa mgogoro huu bali ni tuwe kama madaraja ya kufanikisha mgogoro huu kumalizimika kwa amani,” alisema.
 
Hata hivyo, mapema wiki hii Baraza Kuu la Uongozi wa CUF lilifungua shauri mahakamani kuhusu mgogoro wa uongozi ndani ya chama hicho, wakimshataki Msajili vya Vyama vya Siasa nchini pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

 Katika shauri hilo, wanapinga uamuzi wa Msajili kuandika barua ya kumtambua Profesa Ibrahim Lipumba kuwa Mwenyekiti halali wa chama hicho huku wakidai kuwa alijiuzulu na taarifa za kujiuzulu kwake waliziwasilisha kwa Msajili.
 
Baraza hilo limedai katika shauri hilo kuwa katiba na sheria ya vyama vya siasa haimpi mamlaka Msajili kuingilia maamuzi ya ndani ya vyama vya siasa. Shauri hilo bado halijaanza kusikilizwa.

0 comments:

Post a Comment