Adverts

Wednesday, January 13, 2016

day, January 13, 2016 Mwanafunzi wa Miaka 13 Aozeshwa kwa Ng’ombe 13

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Mika Nyange
Mtoto mwenye umri wa miaka 13 anayesoma darasa la sita katika Shule ya Msingi Wishiteleja wilayani Kishapu mkoa wa Shinyanga, ameozeshwa kwa nguvu na wazazi wake baada ya kupokea mahari ya ng’ombe 13.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Shinyanga juzi, Mkurugenzi wa Shirika la AGAPE, John Myola alisema mwanafunzi huyo alifungishwa ndoa ya kimila Septemba 25, mwaka jana katika Kitongoji cha Nyamikoma Kijiji cha Buchambi wilayani Kishapu.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Mika Nyange alisema hakuwa na taarifa kuhusu tukio hilo na aliahidi kuwasiliana na Mkuu wa Polisi wilayani Kishapu, ampatie taarifa kamili aitoe rasmi kwa waandishi wa habari.

Hata hivyo,alipotafutwa Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Hawa Ngh’umbi alikiri  kupokea nakala ya barua kutoka Agape iliyozungumzia juu ya kufungishwa ndoa kwa mtoto huyo. 
Alikemea kitendo hicho na kuahidi kumsaka mtuhumiwa akamatwe na kufikishwa mahakamani.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Shirika la Agape, Myola, siku ya tukio, ofisi yake ilipokea taarifa kutoka kwa wasamaria wema ambao walieleza kusikitishwa na kitendo cha mtoto huyo mdogo, kuozeshwa kinyume cha sheria za nchi na kudai kuwa zipo shutuma za viongozi wa serikali ya kijiji na kitongoji kushiriki.

Alisema baada ya kupokea taarifa hizo, alikwenda katika eneo la tukio akiongozana na polisi kutoka kituo kidogo cha Maganzo wilayani Kishapu, ambapo walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa na viongozi wa serikali ya kitongoji na kijiji, waliodaiwa kuhusika katika suala la kupatanisha mahari.

Mwanamume aliyekuwa akifunga ndoa na mwanafunzi huyo, alitajwa kwa jina la Emmanuel Njile, mkazi wa Kijiji cha Isemelo Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, ambaye alikamatwa na kufikishwa kituo cha polisi, alikofunguliwa jalada la kesi namba RB/ MGZ/495/2015 na kuwekwa mahabusu.

Alidai kuwa baada ya kusambaratisha ndoa hiyo, walipewa fomu namba tatu (PF. 3) ili wampeleke mtoto huyo hospitali, ambako alifanyiwa vipimo na daktari, ambako hata hivyo inadaiwa ilibainika hakuwa ameingiliwa kimwili.

Alisema siku mbili baadaye, Septemba 27, 2015 usiku saa 2, walipokea taarifa za kuwepo kwa kikao cha siri katika baa moja ya mjini Maganzo, kilichowahusisha baadhi ya viongozi na watendaji (wakiwemo polisi) waliokutana na kaka wa mtoto, wakijadili jambo ambalo haikufahamika ni nini.

“Kwa kweli tulipata wasiwasi juu ya kikao hicho cha usiku, tuliamini kuna mpango mchafu ulikuwa ukifanyika, na kweli asubuhi yake, Septemba 28, 2015, tulielezwa kuwa mtuhumiwa alikuwa ametolewa mahabusu na kuruhusiwa kurudi nyumbani, ambako alimchukua mtoto aliyeozeshwa na kuondoka naye.
 “Tulifuatilia na kuelezwa kuwa amekwenda kwao Kijiji cha Isemelo wilayani Igunga Mkoa wa Tabora ambako hivi sasa wanaishi kama mke na mume.Tulimwandikia barua Mkuu wa Polisi wilayani Kishapu ili kupata ufafanuzi juu ya kesi hiyo".

Akifafanua kwamba, katika barua iliyotoka kwa Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kishapu yenye Kumb. Na. A.20/08/ Vol.1/13 ya Desemba 14, 2015, mtuhumiwa aliyetajwa kuhusika na kesi iliyofunguliwa kwa jalada namba RB/ MGZ/495/2015 alikuwa ni Daudi Sagi badala ya Emmanuel Njile, hatua ambayo alisema walishangaa.

0 comments:

Post a Comment