Papa
Francis na mgombea wa Republican mwenye matamshi tata, Donald Trump
wameingia kwenye mvutano kuhusu ukristo wa mgombea huyo kufuatia
matamshi yake kuwa akichaguliwa kuwa Rais wa Marekani atajenga ukuta
mpakani mwa Mexico na Marekani ili kuzuia wahamiaji kuingia nchini humo.
Trump
alieleza hivi karibuni kuwa atachukua hatua hiyo ikiwa ni sehemu ya
jitihada za kulinda usalama wa Marekani ikiwa ni pamoja na kuzuia Watu
wenye imani ya Kiislamu kuingia nchini humo.
Kauli
hiyo ya Trump imeonekana kumkwaza Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani,
Papa Francis ambaye amesema kuwa mtu anayepanga kujenga ukuta kati ya
Marekani na Mexico badala ya kujenga daraja ‘sio Mkristo’.
“Mtu anayefikiria kujenga ukuta, kokote walipo, na sio kujenga madaraja, sio mkristo. Hii sio injili,” Papa Francis aliwaambia waandishi wa habari.
Papa
Francis alitoa kauli hiyo katika siku yake ya mwisho ya ziara ya
Mexico. Alisema kuwa hawalazimishi wakristo kumchagua au kutomchagua mtu
fulani, lakini wampime kauli zake kabla ya kufanya maamuzi katika
sanduku la kura.
Trump amejibu kauli hiyo ya Papa akieleza kuwa Kiongozi huyo hana haki ya kumhukumu mtu yeyote kuwa ni Mkristo au sio Mkristo.
“Hakuna kiongozi, hususan kiongozi wa dini, mwenye haki ya ya kuhoji imani ya kidini ya mtu mwingine,” Trump alisema.
“Kama
Vatican itashambuliwa na ISIS, ambapo kila mmoja anajua kuwa ni tuzo
muhimu ya ISIS, ninawaahidi kuwa Papa atatamani na kuomba kuwa Donald
Trump angekuwa Rais,” aliongeza Trump.
0 comments:
Post a Comment