Adverts

Tuesday, March 15, 2016

Billioni 12 Zakusanywa Kutoka Kwa Wakwepa Kodi

Na Raymond Mushumbusi- MAELEZO
Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekusanya takribani Sh. billioni 12 kutoka kwa wafanyabiashara ambao walikwepa kodi na kupewa muda wa siku 14 na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kulipa kodi hizo kwenye mamlaka hiyo.

Akitoa takwimu hizo jana mara baada ya kuapishwa kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Alphayo Kidata alisema, kila Mtanzania ana jukumu la kulipa kodi kwa mujibu wa sheria na sio kukwepa na amehaidi kulisimamia vizuri suala la ukusanyaji wa mapato katika sehemu mbalimbali ili kuongeza mapato ambayo yatasaidia kufanikisha maendeleo katika sekta mbalimbali.

“Tutajitahidi kwa kila namna kuwaelimisha wananchi wetu ili wafahamu wajibu wao na umuhimu katika kulipa kodi na sio kukwepa kulipa kodi na tunawaomba wananchi kila waendapo kupata huduma yoyote ile iwe katika sekta binafsi au Serikalini basi anatakiwa aombe stakabadhi za manunuzi au huduma ili tuweze kudhibiti upotevu wa kodi” alisema Kidata.

Kamishna Kidata aliongeza kwamba   mamlaka hiyo ipo kwa ajili ya kuwahudumia wananchi na kama kuna suala lolote au tatizo kuhusu kodi kuna ofisi katika mikoa yote ikiwa ni hatua ya kutatua shida zao na kama kuna mtumishi yoyote wa mamlaka hiyo atashindwa kumuhudumia mwanachi inavyotakiwa basi taarifa zitolewa mara moja kupitia namba zao zilizoko kwenye tovuti ya mamlaka hiyo, ambayo ni www.tra.go.tz ili kuimarisha huduma zetu kwa wateja.

Aidha Kamishna Mkuu huyo alisema kuwa watawachukulia hatua wale wote ambao hawatalipa au hawajalipa kodi zao kwa kuwapeleka mahakamani kwa kukaidi kulipa kodi halali kwa mujibu wa Sheria.

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeanzishwa kwa mujibu wa Sheria na ina mamlaka ya usimamizi wa makusanyo ya Mapato Tanzania na kwa kipindi cha hivi karibuni kumekuwa na ukwepaji wa kodi uliotokana na sakata la upotevu wa makontena katika Bandari ya Dar es Salaam hivyo kuikosesha mapato Serikali lakini jitihada thabiti zimefanywa na mamlaka hiyo kukusanya madeni kutoka kwa wakwepa kodi na kuwafikisha mahakamani ambao wamekaidi kulipa.

0 comments:

Post a Comment