Adverts

Showing posts with label Uchumi. Show all posts
Showing posts with label Uchumi. Show all posts

Friday, October 7, 2016

Mamlaka ya Mapato (TRA): Makusanyo ya Kodi mwezi Septemba 2016

 
Mkurugenzi wa Elimu na huduma kwa mlipa kodi wa TRA, Bw. Richard Kayombo amesema mwenendo wa ukusanyaji mapato ya Serikali kwa sasa ni wa kuridhisha katika  kufikia  lengo la kukusanya kiasi cha shilingi trioni 15.1 kwa mwaka fedha wa 2016/2017.

Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) imekusanya Mapato ya shilingi trilioni 1.37 kwa Mwezi September kati ya lengo la kukusanya shilingi trilioni 1.4 mwezi huo

Kuhusu zoezi la uboreshaji wa taarifa ya namba za utambulisho wa mlipa kodi linaloendelea jijini Dar es Salaam, Bw. Richard Kayombo amesema mpaka sasa TRA imetoa vyeti vipya vya TIN  kwa watu 15, 467 na zimebaki siku tisa kukamilisha zoezi hilo.
 
 Tazama video hapa
 

Sunday, October 2, 2016

Waziri Mkuu Ashangazwa Na Kodi Kubwa Soko La Dodoma.....Aagiza Baraza La Madiwani Lipitie Upya Na Kumpa Majibu

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameliagiza Baraza la Madiwani la Manispaa ya Dodoma lifanye marekebisho ya kodi inayotozwa kwenye soko la Majengo ambayo imepandishwa kutoka sh. 20,000 hadi sh. 150,000 kwa mwezi.
 
 Amesema anatambua maamuzi ya Baraza ni ya kikao halali lakini hakubaliani na ongezeko hilo ambalo ni sawa na asilimia 650 kwani linawaumiza wananchi.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana (Jumamosi, Oktoba Mosi, 2016) wakati alipotembelea soko hilo akiwa kwenye ziara ya kukagua maeneo ya kutolea huduma za jamii mjini Dodoma.

Amesema soko hilo linatakiwa lifanyiwe mapitio ili liwekwe kwenye hali nzuri na Manispaa ihakikishe maboresho hayo yanafanyika bila ya kuwaumiza wafanyabiashara.

“Kwa kuwa uamuzi wa kupandisha kodi ulifanyika kisheria na kupitishwa na baraza la Madiwani, sitaki kuvunja sheria. Nawaagiza mkazungumze tena katika baraza na muangalie namna ya kupunguza gharama hizo,” amesema.

“Hali hii haiwezekani kuachwa iendelee, huku ni kuwaumiza wananchi. Mkurugenzi wa Manispaa nenda kaitishe tena kikao, mfanye mazungumzo upya kwenye baraza lenu na mje mnieleze mmekubaliana nini” amesisitiza.

Pia ameitaka Manispaa hiyo ihakikishe makusanyo yote ya fedha katika soko hilo yanakusanywa kwa njia ya kielektroniki ili fedha hizo ziweze kuleta tija na kuwataka Mkuu wa mkoa na wilaya kuwachukulia hatua wotewatakaobainika kuiba fedha hizo.

Amesema Manispaa hiyo inatakiwa kupanua masoko kwa kujenga masoko mapya makubwa katika maeneo ya Nkuhungu, Kisasa, Mlimwa na Barabara ya Iringa ili huduma hizo zisambazwe.

Mapema akisoma risala yake, Mwenyekiti wa soko hilo, Bw. Godson Rugazama alimueleza Waziri Mkuu changamoto zinazolikabili soko hilo kuwa ni pamoja na ongezeko la kodi isiyozingatia uhalisia wa maisha na shughuli za wajasiriamali sokoni hapo. “Kodi imeongezeka kutoka sh. 20,000 hadi 150,000 kwa mwezi,” alisema.

Mwenyekiti huyo alitaja changamoto nyingine ni uchakavu wa mifereji ya maji machafu, kuvuja kwa paa la soko, bidhaa kuuzwa katika maeneo yasiyokuwa rasmi na kusababisha wateja kutoingia sokoni.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu ametembelea hospitali ya rufaa ya mkoa wa Dodoma na kukagua maeneo mbalimbali zikiwemo wodi za wagonjwa, jengo la wazazi na jengo jipya la wagonjwa wa Bima ya Afya (NHIF).

Akiwa hospitalini hapo, pia alizungumza na watumishi wa sekta ya afya na kuwataka wawahimize wananchi wajiunge na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ambao unawawezesha mtu kulipia bima ya matibabu kwa ajili ya mhusika, mwenza wake na watoto/watemezi wanne na serikali inajazia kiasi kile kile alichochangia.

Akizungumzia miundombinu ya afya mkoani humo, Waziri Mkuu alisema mkoa wa Dodoma hauna shida ya matibabu au utoaji wa huduma ya afya kutokana na miundombinu iliyopo hivi sasa.

Aliwataka wafanye kazi kwa uadilifu na uaminifu na kuongeza tija katika utendaji kazi wao huku wakitanguliza utunzaji wa mali ya umma.

“Ninawasihi mjenge tabia ya huruma kwa wagonjwa huku mkitambua unyeti wa kazi mliyonayo. Ninaamini mtatunza vifaa mlivyonavyo na siyo kuvichukua na kuvipeleka kwenye zahanati zenu au maduka yenu binafsi ya dawa,” alionya.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU

Thursday, September 1, 2016

Rais Magufuli Atoa ONYO Kwa Walioficha Mabilioni ya Pesa Nyumbani, Atishia Kubadili Noti Haraka ili Kuwakomoa

Rais John Magufuli amewataka watu walioficha fedha majumbani kuziachia ziingie kwenye mzunguko vinginevyo anaweza kuamua kuzibadili ili wakose mahali pa kuzipeleka. 

Amesema watu hao wamekuwa na utaratibu wa kutoa fedha zao katika benki na kuzificha kwa kuogopa kuwa atabaini kiasi walichonacho, hivyo akawataka kuachana na tabia hiyo kwa sababu fedha hizo ni mali yao. 
Akizungumza katika mkutano wa 14 wa mwaka wa wahandisi uliofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City jana, Rais Magufuli aliyetumia dakika 73 kuzungumza na wahandisi hao na kueleza mikakati na changamoto zinazoikabili Serikali ukiwamo wizi na ufisadi, alisisitiza;  

“Huu ujumbe ni kwa wale wanaoficha fedha, waziachie na wajiandae, naweza kuamua baada ya siku mbili tatu nabadilisha fedha na hizo zilizofichwa katika magodoro ziozee huko. Ni nafuu mzitoe mziweke katika mzunguko zikafanye kazi,” alisema. 
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na mawaziri, naibu mawaziri, makatibu wakuu na wahandisi kutoka ndani na nje ya nchi, Rais Magufuli alisema katika utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano hakuna fedha za bure. 
Alibainisha kuwa kipindi cha nyuma, fedha zilikuwa nyingi mitaani kwa sababu baadhi ya watu walikuwa wakiiba fedha za Serikali, huku akitoa mfano wa jinsi mabilioni ya fedha za watumishi hewa yalivyotafunwa, jambo alilosema sasa limedhibitiwa. 
“Nyinyi wahandisi ni wachapa kazi, huu ndiyo wakati wa kutajirika.Tumieni nafasi hii maana watu walizoea kupata fedha za bure. Waliokuwa wanatafuta dili katika wizara hawapati kitu na sasa nikijua mtendaji wa Serikali umepiga dili utaondoka tu,” alisema. 
“Fedha za bure hazipo na ndiyo maana thamani ya nchi na fedha yetu imeanza kuongezeka na mfumuko wa bei umeshuka mpaka asilimia 5.1.” 
Alisema wakati fulani akiwa anatoka mkoani Geita, mfuko wa saruji ulikuwa unauzwa Sh26,000 lakini sasa unauzwa Sh16,000. 
"Wanaoficha fedha ni wachache. Watu watapata fedha za kutosha kwa kufanya kazi. Wafikirie kufanya uwekezaji wa viwanda vyao na nyinyi wahandisi muwe namba moja.” 
Changamoto na mikakati ya serikali yake
Alisema licha ya Serikali kuamua kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kutoka 87,000 hadi 137,000, imebainika kuwa wilaya moja mkoani Arusha ina wanafunzi hewa zaidi ya 10,000 na wilaya nyingine iliyopo Mwanza ina wanafunzi hewa zaidi ya 8,000. 
Kuhusu mapato ya Serikali, alisema baada ya kuingia madarakani yalipanda kutoka Sh800 bilioni hadi Sh1.3 trilioni lakini wakati hayo yanafanyika, Serikali imebaini wafanyakazi hewa zaidi ya 16,500 na kusema hiyo ndiyo Tanzana aliyoikuta. 
Rais Magufuli pia alieleza mikakati ya kununua meli mbili, kujenga reli ya kisasa, kukarabati viwanja vya ndege na kufafanua sababu za Serikali kununua ndege mbili aina ya Bombadier Q400, ambazo zimeshalipiwa asilimia 40. 
“Hizi ndege hazili mafuta, kasi yake nzuri, zinatua uwanja wowote hata wa changarawe. Wapo wanaoziponda eti hazina kasi, kama unataka kasi kapande za jeshi,” alisema huku akicheka. 
Huku akieleza jinsi wahandisi wa nje wanavyotekeleza miradi kwa gharama kubwa, alisema katika bajeti ya mwaka 2016/17, Serikali ilitumia Sh100 bilioni kwa ajili ya kukarabati viwanja saba vya ndege vya lami, lakini wapo waliotumia Sh105 bilioni kujenga barabara ya kuruka na kutua ndege katika Uwanja wa Ndege Mwanza, fedha ambazo ni nyingi. 
“Uwanja wa ndege Dar es Salaam unaokarabatiwa sasa, zimejengwa njia tatu (za kuruka ndege) na lile jengo (la abiria) lakini zimetumia Sh650 bilioni na gharama hizo zimewekwa na wahandisi. Tunahitaji kufanya uchunguzi, maana gharama hizi ni kubwa sana, kwa nini Watanzania tunachezewa hivi?” alihoji na kuongeza, “Ni bora wangepewa wahandisi wa Tanzania wakala hizi hela.” 
Alisema wahandisi wazawa wanaweza kujipanga na kupata tenda ya kujenga reli ya kisasa, kujenga bomba la gesi kutoka Tanga kwenda Uganda na hata kujenga viwanja vya ndege. 
Wizi unavyofanyika sekta ya madini
Alisema katika sekta ya madini, nchi inaibiwa na kutoa mfano jinsi dhahabu inavyochimbwa wilayani Kahama, kisha wahusika kuchukua mchanga na kwenda nao nje ya nchi kwa ajili ya kusafishwa.
“Kinachosafishwa huko nje hatujawahi kukiona, wahandisi mmekaa kimya. Kuna uhakika gani katika kontena kama hakuna kilo 200 za dhahabu ambazo wameziyeyusha na kuzichanganya na mchanga? Hivi wahandisi tumeshindwa kuweka utaratibu wa kubaini kilichomo katika mchanga? Tunashangilia mtu anasafirisha mchanga na sisi tunakubali kuwa wanasafirisha mchanga, mchanga unaondoka na viongozi wetu hata majeshi yetu na polisi unasindikiza mali yako.”
Alisema suala hilo pia linapaswa kuwa changamoto kwa viongozi na wanasiasa na akahoji sababu za kila mgodi wa dhahabu kuwa na uwanja wa ndege, 
“Tena hizi ndege wakati mwingine zinaruka moja kwa moja. Sisi Watanzania ni watu wa ajabu sana. 
“Nasikia Profesa Muhongo (Sospeter – Waziri wa Nishati na Madini) atatoa mada katika mkutano huu, atueleze kwa namna gani mchanga wetu utaacha kupelekwa nje? Katika vitu vinavyoniumiza ni pamoja na hili. Haya mamchanga tuyashike tuangalie kilichomo humo ndani. Tanzania tumechezewa na kuibiwa mno, nipo serikalini najua. Kila mahali ni dili, ukigeuka huku dili, ukienda huku dili, kila mahali ni dili tu,” alisema.
Siri ya kuteua wahandisi wengi serikalini 
Rais Magufuli alisema, wakati akiomba kura katika kampeni za Uchaguzi Mkuu uliopita, alinadi mkakati wa kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda, lakini hakuwahi kusema watu watakaomsaidia kwa sababu aliamini wahandisi hawatamtupa mkono katika kufanikisha hilo. 
Huku akifichua siri ya kujaza wahandisi katika serikali yake, alisema taaluma hiyo ni muhimu katika maendeleo ya nchi na kuwataka kuwatumia viongozi hao kujenga uchumi wa Taifa, ikiwa ni pamoja na kuanzisha viwanda. 
“Tusipotumia wahandisi kamwe tusizungumze kuhusu maendeleo ya nchi yetu, tusahau. Nimeteua wahandisi kutekeleza mambo kwa niaba ya wahandisi. Mnatumika kujenga uchumi wa watu wengine. Jipangeni nawaunga mkono, anzisheni viwanda… kampuni zenu na kupata kazi maana hakuna nchi duniani isiyotaka kujenga watu wake,” alisema. ...

Wednesday, August 31, 2016

Makusanyo Kodi za Simu Yapanda Maradufu

Sheria ya Fedha ya Mwaka 2016 iliyopitishwa kuhusu utozaji ushuru kwenye ada ya kutuma na kupokea fedha kwenye miamala ya benki na simu, imeanza kuzaa matunda kutokana na ongezeko la mapato lililoanza kushuhudiwa kutoka kampuni za simu.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu iliyokutana jana na Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), iliambiwa kutokana na sheria hiyo iliyopitishwa Bunge baada ya kupitisha bajeti ya mwaka huu, mwezi uliopita serikali imeshuhudia ongezeko kubwa la mapato, yaliyotolewa na kampuni za simu.

Taarifa hiyo ilitolewa jana kwenye Kamati ya Kudumu ya Miundombinu, imeonesha Kampuni ya Vodacom ilikuwa ikitoa kodi ya ushuru wa bidhaa kwa fedha zinazotumwa kwa wastani wa Sh milioni 360 kwa mwezi, lakini baada ya mabadiliko ya sheria, Julai pekee mwaka huu imelipa Sh bilioni 1.9.

Mwakilishi wa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Godwin Barongo aliiambia kamati hiyo kuwa kwa upande wa Kampuni ya Tigo, walikuwa wanatoa wastani wa Sh milioni 250 kwa mwezi, lakini sasa wametoa Sh bilioni 1.48.

Barongo ambaye ni Meneja Msaidizi, Kitengo cha Walipa Kodi Wakubwa TRA alikuwa akizungumzia namna Mtambo Maalumu wa Kusimamia Mawasiliano na Udhibiti wa Mapato yatokanayo na Simu (TTMS) unaosimamiwa na Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) ulivyowezesha kufanikisha ukusanyaji mapato.

“Pamoja na mabadiliko ya sheria yaliyoanza mwezi Julai mwaka huu, kampuni za simu zilikuwa zikitoza transfer, lakini sheria ilikuwa haigusi kwenye kutoa, Baada ya hiyo, tuligundua kuwa sasa kamisheni nyingi zilipelekwa kwenye kutoa kwa sababu hakuna tozo na kwenye transfer zinapungua,” alisema Barongo.

Aliendelea kusema, “Kwa hiyo mabadiliko haya ya sheria ya sasa hivi ambayo tunatoza kwenye kuweka na kutoa, yametusaidia.” 
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso alisisitiza kuwa wabunge wanategemea Wizara ya Miundombinu kupitia sekta ya mawasiliano, ichangie mapato mengi kwa serikali.

Baada ya Bunge kupitisha mabadiliko ya sheria ya fedha yaliyopitisha utozaji kodi ya ushuru wa bidhaa katika miamala ya benki na simu za mkononi, ulijitokeza mjadala ambao baadhi ya watu walidai ushuru huo utaathiri wateja wa kampuni za simu na benki.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alifafanua kwamba serikali imeamua kutoza ushuru kwenye ada ya kutuma na kupokea fedha au vyote kwa kadri itakavyotozwa akisisitiza kwamba utalipwa na benki na kampuni na si mtumiaji au mpokeaji wa fedha katika miamala itakayofanyika.

Sunday, April 3, 2016

Tibaijuka Kitanzini Tena Sakata la Escrow.....Bodi ya Rufani ya Kodi Tanzania (TRAB) Yamuamuru Kulipa Kodi ya Shilingi Milioni 586


Mbunge wa Muleba Kusini (CCM), Profesa Anna Tibaijuka amesema yupo tayari kulipa kodi ya mapato ya Sh586 milioni iwapo Mahakama itaamuru hivyo.

Kodi hiyo inatokana na Sh1.617 bilioni alizopewa  na mfanyabiashara maarufu nchini, James Rugemalira  ambazo zilidaiwa kuchotwa katika akaunti ya Tegeta Escrow.

Profesa Tibaijuka aliyasema hayo jana baada ya taarifa kwamba Bodi ya Rufani ya Kodi Tanzania (TRAB), imeagiza utekelezaji wa suala hilo ili kutimiza matakwa ya sheria kuhusu mapato nchini.

“Ni kweli ninadaiwa kodi ya Sh586 milioni, ila nimeenda mahakamani kutaka ufafanuzi kama ni halali kufanya hivyo kwa fedha zilizotokana na mchango,” alisema Profesa Tibaijuka na kuongeza “Nilipewa fedha kwa ajili ya shule lakini nadaiwa kama ni kipato binafsi, hivyo nataka Mahakama iseme, ikikubali nitalipa bila shida yoyote.”

Mbunge huyo alifafanua kuwa, anatambua kulipa kodi ni suala la kila mwananchi na anachotaka ni ufafanuzi wa uhusiano uliopo kati ya mapato na kodi.

Alisema lengo ni kutaka kujua iwapo mchango ni sehemu ya fedha zinazostahili kutozwa kodi, bila kujali zimepokelewa zikiwa taslimu au kupitia kwenye akaunti benki.

“Nipo msibani hivi sasa. Watu wanakuja kunipa pole, wengine wanatoka Dar na wasioweza wanatuma michango yao na hapa ndipo nisipoelewa dhana ya kodi kwenye michango. Hii nayo inastahili kuingizwa kwenye mkumbo huo?” alihoji.

Msemaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo alithibitisha kutolewa kwa hukumu hiyo kwenye pingamizi la makadirio aliloliweka mbunge huyo na kueleza kuwa bado anaweza akatafuta haki kwenye mamlaka za juu kama hajaridhika.

“Shauri lake liliamriwa Machi 29 na akatakiwa kulipa kiwango hicho alichokadiriwa,” alisema.

Mbunge huyo wa Muleba Kusini, alitakiwa kulipa fedha hizo baada ya TRAB kutupilia mbali rufaa yake ya kupinga kulipa zaidi ya Sh500 milioni.

Profesa Tibaijuka, Waziri wa zamani wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, alikata rufaa hiyo baada ya TRA kumtaka alipe kodi ya mapato Sh586,364,625 kutokana na fedha alizopokea kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited, Rugemalira.

Profesa Tibaijuka ambaye alipokea fedha hizo kupitia akaunti yake iliyopo Benki ya Mkombozi, zilisababisha kuvuliwa uwaziri na Rais mstaafu, Jakaya Kikwete.

Alisema fedha hizo hazikuwa zake binafsi bali zilitolewa msaada kwa Taasisi ya Joha Trust.

Hata hivyo, TRA kupitia kwa Wakili wake, Noah Tito ilisema Tibaijuka anawajibika kulipa kodi hiyo kwani fedha hizo ziliingia katika akaunti yake binafsi.

Monday, March 28, 2016

Zaidi ya Wafanyakazi 400 wa TTCL Kupoteza Ajira


Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) ipo kwenye maandalizi ya kupunguza wafanyakazi wasiohitajika kwa sasa kutokana na kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia.

TTCL inayotoa huduma za simu na pia kutoa mitandao kwa kampuni zilizo na leseni ya huduma hizo, itapunguza wafanyakazi 400 ili kuongeza ufanisi na hivyo kumudu ushindani katika sekta ya mawasiliano dhidi ya kampuni binafsi. 
Mapema mwaka jana, Serikali iliamua kununua asilimia 35 ya hisa za TTCL zinazoshikiliwa na kampuni kubwa ya huduma za simu nchini India, Bharti Airtel na baadaye mwezi Mei, 2015 aliyekuwa Naibu Waziri wa Sayansi na Mawasiliano, January Makamba aliliambia Bunge kuwa Serikali iko katika maandalizi ya mwisho ya kumiliki hisa zote za kampuni hiyo kubwa kwa huduma za simu za mezani nchini.

Chanzo cha habari kutoka ndani ya kampuni hiyo kinaeleza kuwa kati ya wafanyakazi 1,500 wa TTCL, zaidi ya 400 watapoteza ajira katika mpango huo wa kudhibiti gharama za uendeshaji.

“TTCL itaomba fedha ili kuwalipa wafanyakazi zaidi ya 400 wanaotakiwa kupunguzwa,” alisema mtoaji habari huyo .

“Kuna wafanyakazi wanaingia asubuhi na kutoka jioni bila kufanya kazi yoyote ile na mwisho wa mwezi anakula mshahara zaidi ya Sh800,000. Kumuachisha kazi inakuwa vigumu sana, lakini kama TTCL itasaidiwa na Serikali kufanikisha hilo, itakuwa imejikwamua kwa kiwango fulani.”

Hata hivyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Dk Kamugisha Kazaura alisema maandalizi ya kupunguza wafanyakazi yataanza mwezi Aprili kupitia ukaguzi maalumu wa rasilimali watu.
Alisema hatua ya awali kwa sasa ni kuangalia mpango mkakati wa kampuni hiyo jinsi gani inaweza kujijenga upya kutokana na changamoto ya ushindani wa kibiashara.

“Kwa sasa siwezi kusema ni wafanyakazi wangapi wanatakiwa kupunguzwa kutoka miongoni mwa 1,500 kwa kuwa kila mmoja amekuwa akiwasilisha taarifa yake mwisho wa mwaka na wapo wanaotimiza na wengine wanashindwa kutimiza malengo ya kampuni, mchango wao unakuwa kidogo,” alisema.

Dk Kazaura alisema katika lengo la mpango huo ni kuangalia jinsi gani watalaamu waliopo wanatumika kuendana na mabadiliko ya teknolojia.

Alisema kuna wataalamu waliopo kwa sasa ambao hutumika katika shughuli za uzalishaji, lakini kulingana na mabadiliko ya kazi nyingi kufanywa na teknolojia mpya na nafasi ya kazi nyingi katika taaluma zao zimepungua.

“Pamoja na hivyo lakini itakuwa vigumu kuwafahamu ni wangapi ambao hawazalishi katika kampuni hadi kazi hiyo ya HR auditing (ukaguzi wa rasilimali watu) itakapokamilika. Itakuwa tathmini itakayotoa mwelekeo mpya wa kampuni,” alisema.

Alipoulizwa kuhusu mpango wa TTCL kuomba msaada serikalini, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alisema hana taarifa yoyote.

Hata hiyo, alisema TTCL ina mamlaka yake ya kujiamulia kuajiri au kupunguza wafanyakazi bila kuingiliwa na Serikali.

Tuesday, March 22, 2016

Ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi Toka Uganda Hadi Tanzania Uko Palepale Licha ya Mazungumzo yanayoendelea Kati ya Kenya na Uganda

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limesema mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Uganda mpaka Bandari ya Tanga utafanyika kama marais wa nchi hizo mbili walivyokubaliana.

Wameeleza kuwa kwa sasa makubaliano yako katika hatua za mwisho ili ujenzi wa mradi huo kuanza huku nchi za Kenya na Uganda wakiendelea na mazungumzo katika kufikia mwafaka wa jambo hilo.

Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dk James Mataragio alisema hivi karibuni kumekuwa na taarifa za mradi huo kukwama kutokana na Kenya kudaiwa kukubaliana na Uganda kupitisha mradi huo nchini mwao.

Akizungumzia suala hilo, Dk Mataragio alisema ni kweli awali kulikuwa na makubaliano ya nchi hizo mbili kupitisha mradi huo Kenya kutoka Hoima hadi Bandari ya Lamu, lakini kwa sababu mbalimbali Uganda waliamua kupitisha Bandari ya Tanga.

Alieleza ingawa umbali kutoka Uganda hadi bandari za Kenya ni karibu kwa kilometa chache kuliko Tanga zipo sababu zilizofanya bomba hilo kufikishwa Tanga. Sababu hizo ni pamoja na gharama kubwa za ujenzi kwenda Kenya na bandari ya Tanga kuwa na kingo za asili hivyo kuweza kusafirisha mafuta mwaka mzima.

Alisema pia ujenzi wa bomba hilo hadi bandari ya Tanga haupiti sehemu yenye makazi ya watu wengi hivyo kupunguza gharama, huku bomba likipita maeneo mengi ya tambarare bila kuwa na miinuko inayofanya kuongeza gharama za kupampu.

Alisema tayari timu za wataalamu zimekutana na kukubaliana masuala kadhaa ya ujenzi huo pamoja na kusaini mpango wa utekelezaji wa mradi. 
Dk Mataragio alisema kuhusu gharama ni kawaida siyo kubwa kama inavyoelezwa na baadhi ya watu hivyo ni vema watanzania wakaelewa kuwa hakuna tatizo la kukwama kwa mradi huo kwa sababu yoyote.

Kampuni zinazozalisha mafuta nchini Uganda ni Tullow kutoka Ireland, Kampuni ya Ufaransa ya Total na Kampuni ya CNOC kutoka China.

Wakati hayo yakielezwa hivi karibuni, Makamu wa Rais wa Kampuni ya Total Afrika Mashariki, Javier Rielo alimueleza Rais John Magufuli kuwa kampuni hiyo itaanza ujenzi huo haraka iwezekanavyo, kwa kuwa fedha za kutekeleza mradi huo zipo.

Bomba hilo la kutoka Tanga hadi Uganda litakuwa na urefu wa kilometa 1,410 na litasafirisha mafuta ghafi kutoka ziwa Albert nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga na litajengwa kwa gharama ya Dola za Marekani bilioni nne.

Unatarajiwa kuzalisha ajira za moja kwa moja 1,500 na ajira zisizo za moja kwa moja 20,000 huku ukitarajia kukamilika baada ya miaka mitatu hadi minne.

Soko la Feri Latakiwa kutafuta Gesi ya Bei Nafuu

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Bodi ya soko la Kimataifa la Samaki la Feri, kukutana na makampuni mbalimbali yanayouza gesi ili kupata kampuni inayouza kwa bei nafuu zaidi lengo likiwa ni kuwapunguzia gharama wakaangaji wa samaki sokoni hapo.

Pia Waziri Mkuu Majaliwa alimtaka Meneja wa soko hilo, Bw. Solomon Mushi kuhakikisha wanakuwa na kifaa maalumu cha kupimia ujazo wa mitungi ya gesi sokoni hapo ili kubaini kama ni sahihi.

Ametoa agizo hilo jana mchana (Jumanne, Machi 22, 2016) wakati alipofanya ziara ya ghafla katika Soko la Kimataifa la Samaki la Feri iliyokuwa na lengo la kuangalia mfumo wa majiko ya gesi sokoni hapo ambapo aliridhishwa na unavyofanya kazi.

Waziri Mkuu ambaye ametumia dakika 44 kulitembea soko hilo, alitoa maagizo hayo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara ambao wamesema wamekuwa wakiuziwa gesi kwa bei kubwa ambayo imekuwa ikiongezeka mara kwa mara.

Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara hao, Bw. Ally Iddi amesema awali walikuwa wanauziwa mtungi wa gesi wenye ujazo wa kilo 32 kwa sh. 70,000 na sasa umeongezeka hadi sh. 98,000 kiasi ambacho ni kikubwa ukilinganisha na uzalishaji wao. “Nimeulizia kwenye baadhi ya maduka na kukuta mtungi wenye ujazo kama huo unauzwa sh. 75,000,” alisema.

Kijana mwingine ambaye ni mkaangaji wa samaki, Bw. Mwanya Selemeni alisema hivi sasa hali ya soko la feri ni nzuri tofauti na walivyokuwa wakitumia kuni kwa sababu hakuna moshi. Alimuomba Waziri Mkuu ahakikishe wanafikishiwa gesi ya kutoka Mtwara ili gharama ziweze kupungua.

Mfanyabiashara mwingine wa soko hilo, Bi. Mariam Samweli ambaye alikuwa akiuza kuni na sasa yeye na wenzake wanataka kufanya biashara nyingine lakini banda walilokuwa wakilitumia halina umeme licha ya kuwa wameomba mara nyingi. “Tunaomba kupatiwa umeme ili tuweke vipepeo tuweze kufanya biashara nyingine,” alisema.

Waziri Mkuu pia alitembelea eneo la mnada wa kuuza samaki sokoni hapo ambako alielezwa matatizo ya umeme na uzibaji wa mitaro ya maji machafu hali ambayo inatishia usalama wa afya zao.

“Kuna jipu la umeme hapa, tunachangishwa hela na kumpa mtu ambaye hatumjui lakini hatujawahi kuona risiti, wao wanaweka umeme juu kwa juu na umeme wenyewe wala haukai. Mita tunayo hapa lakini hata namba hatujapewa,” alisema Bw. Omari Masoud kwa niaba ya wenzake.

Kuhusu tatizo la uzibaji mitaro na kutiririsha majitaka, kiongozi wa mama lishe sokoni hapo, Bi. Fatma Ally aliomba watatuliwe tatizo hilo ambalo limedumu kwa zaidi miezi miwili.

Akijibu kero zao, Waziri Mkuu alimwagiza Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Bw. Raymond Mushi asimamie suala la kuweka umeme kwenye hilo banda pamoja ahakikishe mama lishe wa soko hilo upande wa mnadani waanze kutumia majiko ya gesi badala ya mkaa.

Kuhusu mitaro, alimwagiza meneja wa soko hilo, Bw. Solomon Mushi aimarishe uzibuaji wa mitaro katika soko hilo.  

“Mwambie mkandarasi azibue mitaro kila siku jioni na watumiaji wa soko waache kutumia mifuko ya plastiki kwa sababu inapoingia kule inaziba na wala haiozi,” alisema.

Aliwataka wafanyabiashara waimarishe usafi kwa sababu ni sehemu ya chakula. “Lengo letu ni kufanya soko hili liwe kwenye viwango vya kimataiafa ili mteja anapokuja kununua samaki wabichi ama wa kukaanga awe na chaguo,” alisema.

Kwa upande wake, Meneja wa soko hilo, Bw. Mushi alisema bodi ya soko hilo ambayo imeundwa hivi karibuni itakutana kesho kwa mara ya kwanza na miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa ni maelekezo yaliyotolewa na Waziri Mkuu.

IMETOLEWA NA: 
OFISI YA WAZIRI MKUU
2 MTAA WA MAGOGONI, 
S.L. P. 3021,11410 -DAR ES SALAAM
JUMANNE, MACHI 22, 2016.

Friday, March 18, 2016

Wachina Waliokutwa na Vipande 728 Vya Meno ya Tembo Wahukumiwa Kifungo cha Miaka 30 au Faini ya Bilioni 108


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewahukumu raia wawili wa China waliokutwa na hatia ya kuua tembo 226 adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela au kulipa faini ya Sh108.7 bilioni.

Pia, imeamuru magari matatu ya washtakiwa hao yenye usajili wa namba T 317 BXG, T 777 BET na T 728 BGP pamoja na vipande 728 vya meno ya tembo walivyokutwa navyo vitaifishwe na Serikali.

Akitoa hukumu hiyo jana, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Cyprian Mkeha alisema katika shtaka la kushawishi askari polisi na maofisa wa wanyamapori wapokee rushwa ya Sh30.2 milioni ili wasiwapekue na kuwafikisha katika mikono ya sheria, kila mshtakiwa amehukumiwa kifungo cha miaka mitano jela ama kulipa faini ya Sh1 milioni.

Akiendelea kusoma hukumu hiyo, Hakimu Mkeha aliwaachia huru washtakiwa hao katika shtaka la kukutwa na ganda la risasi.

Raia hao wawili wa China, Xu Fujie na Huang Gin waliokuwa wakitetewa na mawakili, Edward Chuwa na Nehemia Nkoko, waliadhibiwa adhabu hizo baada ya Mahakama kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na mashahidi tisa wa upande wa mashtaka pamoja na utetezi wao.

Hakimu Mkeha alipokuwa akisoma hukumu hiyo, alisema katika shtaka la kukutwa na vipande 706 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh5.4 bilioni bila ya kuwa na kibali, kila mshtakiwa anatakiwa alipe fidia ya Sh54.35 bilioni na kwamba, iwapo watashindwa watumikie kifungo cha miaka 30 jela. 

Akiendelea kuisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkeha alisema ametoa adhabu hizo kwa kuzingatia uzito wa maombi ya mawakili wa Serikali, Faraja Nchimbi na Paul Kadushi na maombi ya utetezi ya kutaka wapunguziwe adhabu.

“Kwa kuzingatia hali halisi ya kesi, ushahidi, hasara ambayo Taifa imeipata kutokana na Tembo hao 226 waliopoteza maisha kwa kuuawa na washtakiwa ni wazi washtakiwa walitishia maisha ya vizazi vya tembo waliomo ndani ya mipaka ya nchi yetu,” alisema Hakimu Mkeha.

Alisema ameridhishwa na ushahidi uliotolewa na mashahidi wa upande wa mashtaka kwa kuwa umethibitishwa pasipo kuacha shaka yoyote.

Kwa upande wa Mawakili wa Serikali, Nchimbi aliiomba Mahakama iwape adhabu kali washtakiwa hao kwa kuwa kati ya kipindi cha 2010 na Desemba 2013, jumla ya tembo 892 waliuawa nchini.

Alisema washtakiwa hao waliingia nchini 2010 hadi Novemba 2013 walipokamatwa kwa makosa hayo na kuwapo kwao rumande, matukio ya mauaji ya tembo yalipungua.

Nchimbi alibainisha kuwa washtakiwa hao waliua robo ya tembo wanaouawa hapa nchini na kwamba, kutokana na wingi wa nyara walizokutwa nazo, inaonekana wazi ni miongoni mwa vinara, wawezeshaji na wahusika wa shughuli za ujangili zinazoendelea nchini.

Alisisitiza kuomba wapewe adhabu kali kwa kuwa tembo ni miongoni mwa wanyama watano wanaoongeza mapato la Taifa kupitia utalii.

Wakili wa utetezi, Nkoko aliiomba Mahakama iwapunguzie adhabu wateja wao kwa kuwa walikwisha kaa rumande miaka mitatu.

Washtakiwa hawa walikamatwa na nyara hizo za Serikali na aliyekuwa Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Balozi Hamis Kagasheki.

Wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, upande wa mashtaka ukiendeshwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi, uliwaita mashahidi tisa wakiwamo wapelelezi, majirani wa washtakiwa walioshuhudia upekuzi, maofisa kutoka polisi na Wizara ya Maliasili na Utalii ambao walitoa ushahidi dhidi ya washtakiwa hao.

Miongoni mwa ushahidi wao, walidai kuwa Oktoba 20, 2013, walipokea taarifa kuwa kuna meno ya tembo yanasafirishwa kutoka mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma kwenda Dar es Salaam na yangeuzwa eneo la Biafra Kinondoni, Dar es Salaam.

Walidai kuwa Novemba 2,2013, waliona gari likiendeshwa na raia hao wa China walilifuatilia hadi kubaini shehena hizo za meno ya tembo zilipohifadhiwa. 

Wednesday, March 16, 2016

Rais Magufuli Apiga MARUFUKU Kukodi Mitambo ya Kuzalisha Umeme


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli jana tarehe 16 Machi, 2016 ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme wa Kinyerezi namba mbili, uliopo katika wilaya ya Ilala Mkoani Dar es salaam, ambao utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kuzalisha megawatts 240 za umeme.
 
Mradi huo ambao utazalisha umeme kwa kutumia gesi asilia inayosafirishwa kwa bomba kutoka Mtwara, unatarajiwa kuanza kuzalisha umeme katika kipindi cha kuanzia miezi 21 hadi 28 utakapokamilika kabisa.
 
Kuanza kwa ujenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme huo, kunafuatia juhudi zilizofanywa na serikali ya awamu ya tano ya kufanikisha upatikanaji wa shilingi bilioni 120, ikiwa ni asilimia 15 ya fedha zilizopaswa kutolewa na Tanzania na fedha nyingine shilingi Bilioni 292 zimetolewa na Japan.
 
Mradi huu umetanguliwa na mradi wa Kinyerezi namba moja ambao una uwezo wa kuzalisha megawatts 150 za umeme, na mitambo yake tayari imeanza uzalishaji wa megawatts 105 zilizoingizwa katika gridi ya Taifa.
 
Pamoja na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa Kinyerezi namba mbili, Rais Magufuli amekagua mitambo ya kuzalisha umeme ya mradi wa Kinyerezi namba moja, ambapo Mkuu wa Kituo cha Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) cha Kinyerezi Mhandisi John Mageni, ametoa maelezo kuwa shirika hilo lina mpango wa kupanua uzalishaji wa umeme katika mradi huo kutoka megawatts 150 hadi kufikia megawatta 335, kwa kuongeza mitambo ya kufua umeme kwa teknolojia inayojumuisha matumizi ya gesi asilia na mvuke uzalishwao na mitambo hiyo.
 
Baadaya ya kupokea maelezo hayo, Rais Magufuli ameridhia kuwa serikali yake itatoa Dola za kimarekani milioni 20, kwa ajili ya kufanikisha upanuzi wa mradi huo na ameagiza kuwa wataalamu wa TANESCO washirikiane na Mkandalasi kuhakikisha upanuzi huo unafanyika haraka iwezekanavyo, badala ya muda wa miezi 12 uliopangwa.
 
Akizungumza na wananchi waliojitokeza katika sherehe za uzinduzi wa mradi huo, Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameiagiza Wizara ya Nishati na Madini na TANESCO, kuanza kuachana na mitambo ya kukodi kwa ajili ya kuzalisha umeme, na badala yake nchi ijenge mitambo yake yenyewe ili kuondokana na gharama kubwa za nishati hiyo muhimu.
 
“Waziri, ukiona mtaalamu anakuletea mapendekezo ya kutaka kukodi mitambo ya kuzalisha umeme, badala ya kuleta mapendekezo ya kununua mitambo yetu wenyewe ujue mtaalamu huyo hafai, mtoe” Amesisitiza Rais Magufuli
 
Ameongeza kuwa tafiti zimethibitisha kuwa hadi sasa Tanzania ina zaidi ya futi za ujazo Trilioni 57 za gesi asilia, ambayo itazalisha umeme wa kutosheleza mahitaji ya ndani, na umeme mwingine kuuzwa nje ya nchi ikiwemo Kenya ambayo tayari imeomba kuuziwa umeme kutoka Tanzania.
 
Aidha, Rais Magufuli ametoa onyo kwa TANESCO kuwa hatarajii kusikia bwawa la maji la Mtera limeishiwa maji, kwa kuwa katika msimu huu wa mvua maeneo ya Iringa yalikuwa na mvua nyingi ambazo zimesababisha hadi mafuriko mafurukio.
 
Kwa upande wake, Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo amesema tangu serikali ya awamu ya tano iingie madarakani, juhudi zilizofanyika zimefanikisha kuongeza uzalishaji wa umeme kutoka megawatts 800 hadi kufikia megawatts 1,000 kiasi ambacho ni pungufu kwa megawatts 20 tu, ikilinganishwa na mahitaji ya megawatts 1020 za sasa.
 
Ameongeza kuwa pamoja na kuweka jiwe la msingi la mradi wa Kinyerezi namba mbili, hivi karibuni serikali inatarajia kujenga miradi mingine ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia, ikiwemo Kinyerezi namba tatu utakaozalisha megawatts 600, Kinyerezi namba nne utakaozalisha megawatts 300, na mingine itakayojengwa Lindi na Mtwara.
 
Prof. Muhongo amebainisha kuwa mpaka sasa gesi asilia inazalisha kati ya asilimia 50 na 60 ya umeme wote hapa nchini, Maji yanazalisha asilimia 30 hadi 40, na umeme unaozalishwa kwa mafuta hauvuki asilimia 10.
 
Sherehe hizo zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Balozi wa Japani hapa nchini Mheshimiwa Masaharu Yoshida, Wabunge wa kamati ya Nishati na Madini, wafadhili wakiwemo Benki ya Dunia, Benki ya Afrika na Shirika misaada la Japan (JICA.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
16 Machi, 2016

Tuesday, March 15, 2016

Serikali Yatangaza Rasmi Kugundulika kwa Futi za Ujazo wa Gesi Tirioni 2.17 katika Bonde la Ruvu

Serikali imetangaza rasmi kugundulika kwa futi za ujazo wa Gesi Tirioni 2.17 katika Bonde la Ruvu mkoani Pwani,  katika eneo lijulikanalo kama Mamba Kofi One ikiwa ni moja ugunduzi ulifanywa na Kampuni ya Dodsal ikishirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

Akitoa tamko hilo mbele ya vyombo vya habari ofisini kwake Dar es Salaam jana asubuhi, Waziri wa  Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alisema kuwa hadi kufikia Machi mwaka huu jumla ya gesi yote iliyogunduliwa nchini ni trioni 57.23.

"TPDC imerekebisha muundo wake tunataka iwe inajishughulisha  na utafutaji wa gesi ya mafuta hivyo kufuatana na sheria ya petroli ya mwaka jana kazi zote zitasimamiwa na TPDC na haitaendelea kusimamia makampuni mengine badala yake tuameazisha wakala wakusimamia kazi ," alisema Muhongo.

Akitolea ufafanuzi kuhusiana  na kugundulika kwa gesi hiyo asilia iliyopo nchi kavu imefikia futi za ujazo tirioni 10.17, na baharini katika kina kirefu cha futi za ujazo ni 47.08.

Waziri Muhongo alisema ufumbuzi huo umefanywa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa kushirikiana na Kampuni ya Haydrocarbons and Power Limited (DODSAL) hivyo wakiendelea na utafiti wataweza kuvuka hata futi 10 kama walivyo dai.

Alisema kuwa takribani futi za ujazo  elfu moja zina uwezo wakuzalisha jumla ya megawati za umeme zipatazo 5000 wakati huo bado wanaendelea na  utafiti wa gesi katika maeneo ya kusini mwa Tanzania ambapo kumegundulika kuwa na gesi nyingi .

"Nilazima taifa letu liwe na umeme mwingi, na umeme wa kutosha kwani tukifanya hivyo tunaweza kufikia kwenye bigawati kama nchi za kusini walivyoweza kupata umeme mwingi," alisema Muhongo.

Akijibu maswali kuhusiana  na kunufaika kwa wananchi na gesi hiyo alisema tayari wameaza kunufaika kwani kabla ya awamu ya tano ya Rais Dk. Jonh Magufuli,  jumla ya megawati 700 hadi 800 ndizo zilikuwa zikitumika katika matumizi ya umeme ambapo katika kipindi cha  awamu ya tano jumla megawati 1000 zinaendelea kutumika.

"Ifahamike kuwa faida ya gesi kwa wananchi ni ya siku nyingi kwani viwanda takribani 37 vimekuwa vikitumika kwa matumizi ya gesi kikiwemo kiwanda cha Saruji " alisema.

Awali kabla ya uzinduzi huo Meneja Utafiti wa Shirika la Maendeleo ya Mafuta na Gesi (TPDC), Venosa Ngowi alisema wanatarajia kumpatia ripoti ya mapendekezo ya juu ya gharama za uuzaji wa gesi nchini ifikapo Aprili,20 mwaka huu.

Ngowi alisema zoezi linalofanyika ni mazungumzo ya wawekezaji na watalamu wa nchi husika kuweza kufanya uhakiki wa gharama wa bei za gesi nchini.

Alisema moja ya changamoto wanazokutanazo ni kuwepo kwa gharama nyingi  zinazo muhusu mwekezaji.

Billioni 12 Zakusanywa Kutoka Kwa Wakwepa Kodi

Na Raymond Mushumbusi- MAELEZO
Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekusanya takribani Sh. billioni 12 kutoka kwa wafanyabiashara ambao walikwepa kodi na kupewa muda wa siku 14 na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kulipa kodi hizo kwenye mamlaka hiyo.

Akitoa takwimu hizo jana mara baada ya kuapishwa kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Alphayo Kidata alisema, kila Mtanzania ana jukumu la kulipa kodi kwa mujibu wa sheria na sio kukwepa na amehaidi kulisimamia vizuri suala la ukusanyaji wa mapato katika sehemu mbalimbali ili kuongeza mapato ambayo yatasaidia kufanikisha maendeleo katika sekta mbalimbali.

“Tutajitahidi kwa kila namna kuwaelimisha wananchi wetu ili wafahamu wajibu wao na umuhimu katika kulipa kodi na sio kukwepa kulipa kodi na tunawaomba wananchi kila waendapo kupata huduma yoyote ile iwe katika sekta binafsi au Serikalini basi anatakiwa aombe stakabadhi za manunuzi au huduma ili tuweze kudhibiti upotevu wa kodi” alisema Kidata.

Kamishna Kidata aliongeza kwamba   mamlaka hiyo ipo kwa ajili ya kuwahudumia wananchi na kama kuna suala lolote au tatizo kuhusu kodi kuna ofisi katika mikoa yote ikiwa ni hatua ya kutatua shida zao na kama kuna mtumishi yoyote wa mamlaka hiyo atashindwa kumuhudumia mwanachi inavyotakiwa basi taarifa zitolewa mara moja kupitia namba zao zilizoko kwenye tovuti ya mamlaka hiyo, ambayo ni www.tra.go.tz ili kuimarisha huduma zetu kwa wateja.

Aidha Kamishna Mkuu huyo alisema kuwa watawachukulia hatua wale wote ambao hawatalipa au hawajalipa kodi zao kwa kuwapeleka mahakamani kwa kukaidi kulipa kodi halali kwa mujibu wa Sheria.

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeanzishwa kwa mujibu wa Sheria na ina mamlaka ya usimamizi wa makusanyo ya Mapato Tanzania na kwa kipindi cha hivi karibuni kumekuwa na ukwepaji wa kodi uliotokana na sakata la upotevu wa makontena katika Bandari ya Dar es Salaam hivyo kuikosesha mapato Serikali lakini jitihada thabiti zimefanywa na mamlaka hiyo kukusanya madeni kutoka kwa wakwepa kodi na kuwafikisha mahakamani ambao wamekaidi kulipa.

Monday, March 14, 2016

Kesi ya IPTL Dhidi ya Zitto Kabwe kusuluhishwa Machi 23 Kwa Siri


Mahakama Kuu inatarajia kusuluhisha kesi iliyofunguliwa na Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) dhidi ya Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe na wenzake Machi 23, mwaka huu.

Kesi hiyo namba 175 ya mwaka 2014 ilipangiwa kuanza kufanyiwa usuluhishi jana mbele ya Jaji Salvatory Bongole, lakini ilishindikana kutokana na upande wa walalamikaji ambao ni IPTL kushindwa kufika mahakamani.

Hata hivyo, Kaimu Msajili wa Mahakama hiyo Kitengo cha Usuluhishi, Beda Nyaki alisema kesi hiyo itasikilizwa kwa siri baina ya pande hizo.

“Kesi hii haiwezi kuripotiwa kwenye vyombo vya habari kwa sababu ipo katika hatua za kwanza za usuluhishi, hivyo kitu kitakachoongolewa baina ya walalamikaji na walalamikiwa kitakuwa ni siri yao,” alieleza Nyaki.

Alisema kusikilizwa kwa faragha kwa kesi hiyo ni hatua ya kupunguza gharama na muda.

Katika kesi hiyo, Kampuni za IPTL, Pan Africa Power Solutions (T) Limited na Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni hizo, Harbinder Sing Seth walifungua madai ya Sh500 bilioni dhidi ya Zitto, Mhariri wa gazeti la Raia Mwema, Kampuni ya Raia Mwema na Kampuni ya Flint Graphics ikiwa fidia kwa kuwakashfu kuhusiana na sakata la uchotwaji wa zaidi ya Sh300 bilioni katika Akaunti ya Tegeta Escrow.

Mawakili wanaomtetea Zitto ni Wakili Ntemi Masanja na Ivone Sianga ambao walidai kuwa walalamikaji walishindwa kufika mahakamani hapo na kusababisha kuahirishwa kwa kesi.

Ilidaiwa kuwa walalamikaji hao walichukua hatua ya kufungua kesi hiyo kufuatia makala aliyoyaandika Zitto katika gazeti la Raia Mwema la Agosti 13, 2014 katika ukurasa wa saba na wa 14, ikiwa na kichwa cha habari “Fedha za IPTL ni mali ya umma.’’

Walalamikaji hao walidai kuwa makala hiyo ni ya upotoshaji na ilikuwa na lengo la kuwachafua mbele ya jamii.