Askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kambi ya Ikola wamelazimika
kulinda nyumba ya mganga wa Zahanati ya Kapalamsenga iliyopo Wilaya ya
Mpanda mkoani Katavi baada ya wanakijiji kupanga kutelekeza mwili wa
mgonjwa wanayedai daktari huyo amesababisha kifo chake kwa kukataa
kumtibu.
Tukio hilo lilitokea juzi saa 10.00 alfajiri baada ya
wanakijiji kupata taarifa kuwa mgonjwa wao huyo, Bibiana Karangi (49)
ambaye mganga huyo alidaiwa kukataa kumtibu, amefariki.
Mwenyekiti
wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda, Hamad Mapengo alisema siku ya tukio
saa saba usiku, mgonjwa huyo alifikishwa katika zahanati ya kijiji
hicho na walipomuamsha mganga huyo nyumbani kwake umbali mita 20,
alikataa akiwataka wampeleke Kituo cha Afya Karema.
Inadaiwa kuwa
mgonjwa huyo alipofikishwa Kituo cha Afya Karema aligundulika kuwa na
upungufu wa damu, hivyo alitakiwa apelekwe Hospitali ya Wilaya ya
Mpanda, lakini wakati akiwa bado kituoni hapo alifariki dunia.
Baada
ya mgonjwa huyo kufariki, wanakijiji hao walipata taarifa ndipo
waliamua kukusanyika kwa lengo la kwenda Karema kuchukua mwili wa
marehemu na kuupeleka nyumbani kwa mganga wa zahanati hiyo ili wamsusie
afanye maziko mwenyewe wakidai ndiye aliyesababisha kifo hicho kwa
kutompatia huduma mapema.
Kutokana na mpango huo, viongozi wa
kata hiyo walipata taarifa hizo na kuomba msaada kwa wanajeshi wa Ikola
ambao walifika na kuizingira nyumba ya mganga huyo, hivyo kuwalazimu
wananchi hao kuanza kutawanyika.
Mwenyekiti huyo alisema
kutokana na mazingira hayo ilimlazimu yeye na kaimu mganga mkuu wa
Wilaya ya Mpanda, Dk Naibu Mkongwa kwenda kumuondoa mganga huyo na
kumpeleka mjini Mpanda kwa kuhofia usalama wake na familia yake.
Baada ya kuondolewa kijijini hapo ndipo askari wa JWTZ walipoondoka nyumbani kwa mganga huyo.
Ofisa
Tarafa wa Karema, Zawadi Mirambo alifika kijijini hapo na kufanya kikao
na wananchi, lakini maoni ya wanakijiji hao yalitofautiana na wauguzi
ambao walidai mgonjwa huyo alikuwa na maradhi, hivyo ushauri wa kwenda
kituo cha jirani ulikuwa sahihi.
Hata hivyo, wanakijiji hao
walidai imekuwa ni kawaida kwa mganga huyo kukataa kutoa huduma kwa
wagonjwa usiku hata kwa wajawazito.
0 comments:
Post a Comment