Adverts

Wednesday, March 30, 2016

Meya Wa Jiji La Dar Es Salaam, Isaya Mwita Aapishwa


Meya Wa Jiji La Dar Es Salaam, Isaya Mwita amesema kati ya Aprili 10 na 11 ataitisha kikao cha kwanza cha Baraza la Jiji, kwa ajili ya kumpata naibu meya.

Mwita aliyasema hayo jana  muda mfupi baada ya kuapishwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Sokoine.

Machi 22, Mwita alichaguliwa kuwa meya wa Jiji la Dar es Salaam baada ya kupata kura 84 dhidi mpinzani wake, Yusuf Yenga (CCM) aliyeambulia 67.

Mwita alisema kinachoendelea hivi sasa ni taratibu za kuwapata wajumbe watakaoingia katika baraza hilo, ambalo lipo tofauti na lililomchagua yeye.

“Ningeweza kuitisha baraza hili hata Ijumaa, lakini sheria inanitaka nikishateuliwa, niitishe baada ya siku saba,” alisema Mwita ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Vijibweni (Chadema).

Machi 23, Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe alisema kuwa naibu meya atapatikana katika Baraza la Jiji litakaloongozwa na meya akishirikiana na yeye.

Hata hivyo, Kabwe alisema jana kuwa wanaendelea na maandalizi ya baraza hilo, ikiwamo kusubiri kuwasilishwa kwa akidi ya wajumbe watakaoshiriki kikao hicho.

Baada ya kuapishwa, Mwita aliwaambia wanahabari kuwa anadhamiria kuwa kiongozi muunganishi bila kujali tofauti za kiitikadi.

Alisema hatarajii kipindi chake cha uongozi kiwe na vurugu au machafuko katika Jiji la Dar es Salaam.

‘’Viongozi wangu wa chini wajisikie amani, kwani mimi nitakuwa kiongozi bora kwa watu wote. Wala sikuja kwa ajili ya kuleta machafuko na ugomvi, bali nahitaji amani ili tutafute maendeleo,’’ amesema.

Mwita alisisitiza ushirikiano kwa viongozi wote ili washughulikie changamoto za muda mrefu katika jiji hilo – usafiri, miundombinu, afya, elimu, na huduma nyingine za jamii.

0 comments:

Post a Comment