Adverts

Saturday, March 12, 2016

Mwenyekiti wa CHADEMA Ahukumiwa Kifungo cha Miezi 6 Kwa Kosa la Kumsaidia Ndugu Yake Kujitetea Mahakamani


Mwenyekiti wa Chadema, Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza, Jacob Munyaga (60), amehukumiwa adhabu ya kifungo cha miezi sita gerezani kwa kosa la kumsaidia ndugu yake maelekezo ya namna ya kujitetea mahakamani.

Ilidaiwa kuwa kiongozi huyo alimsaidia mtuhumiwa Charles Mloba namna ya kujieleza mahakamani dhidi ya shauri la kujeruhi linalomkabili, kinyume cha sheria inayotoa fursa hiyo kwa mawakili pekee.

Hukumu hiyo ilitolewa juzi na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa wilaya hiyo, Francis Kishenyi akitumia kifungu cha 114(1) (A) cha Sheria ya Makosa ya Jinai namba 16 ya mwaka 2002 inayotoa adhabu kwa yeyote anayefanya kazi ya uwakili au usaidizi wa kisheria bila kuwa na sifa.

“Kwa mujibu wa kifungu hicho, adhabu kwa mshtakiwa inaweza kuwa kulipa faini ya Sh500 au kifungo cha miezi sita jela.

"Mahakama hii imeamua utumikie kifungo cha miezi sita jela kwa sababu umebainika kufanya vitendo hivi mara kwa mara,”
alisema hakimu huyo.

Alisema mshtakiwa huyo ana haki ya kukata rufaa kupinga adhabu hiyo ndani ya siku 30 kuanzia jana.

Awali, akijitetea kabla ya hukumu, Munyaga alidai alimsaidia mshtakiwa ambaye ni ndugu yake baada ya kumuomba amwelekeze namna ya kujitetea mahakamani dhidi ya mashtaka yanayomkabili.

Mshtakiwa Charles Mloba na mwenzake Mafuru Iloze, wote wakazi wa Kisiwa cha Ilugwa wilayani Ukerewe wanakabiliwa na kesi ya kujeruhi kinyume na kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Jinai iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002

0 comments:

Post a Comment