Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia
salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Njombe Dkt. Rehema Nchimbi,
kufuatia kifo cha ghafla cha Mkuu wa Wilaya ya Njombe Bi. Sara Dumba,
Kilichotokea jana jioni tarehe 21 Machi, 2016.
Bi.
Sara Dumba aliugua ghafla kuanzia jana mchana na baadaye kukimbizwa
katika hospitali ya Mkoa wa Njombe (Kibena), ambako wakati akipatiwa
matibabu alifariki dunia majira ya saa moja za jioni.
Katika
salamu hizo Rais Magufuli ameelezea kushitushwa na kifo cha ghafla cha
Bi. Sara Dumba, ambaye amesema alimfahamu kwa uchapakazi wake, uaminifu
na uadilifu katika utumishi wa umma na katika uongozi.
"Nimeshitushwa
sana na kifo cha Mkuu wa Wilaya ya Njombe Bi. Sara Dumba, kwa mara
nyingine Taifa limempoteza mtu muhimu ambaye mchango wake ulikuwa bado
unahitajika" amesema Rais Magufuli.
Dkt.
Magufuli amebainisha kuwa Marehemu Sara dumba atakumbukwa kwa kazi
kubwa aliyoifanya ya kuhimiza maendeleo ya wananchi, hususani katika
kilimo na ufugaji, kuhimiza nidhamu ya utumishi serikalini na kuwatetea
wananchi wa hali ya chini wakati wote wa majukumu yake ya ukuu wa
wilaya.
Rais
Magufuli amesema anaungana na familia ya marehemu, ndugu, jamaa,
marafiki na wote walioguswa na msiba huu mkubwa, katika kipindi hiki
kigumu na pia amewataka wote kuwa na subira na uvumilivu.
Amemuombea kwa Mwenyezi Mungu aipumzishe roho yake mahali pema peponi, Amina.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
22 Machi, 2016
0 comments:
Post a Comment