Shirika
la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limesema mradi wa ujenzi wa
bomba la mafuta ghafi kutoka Uganda mpaka Bandari ya Tanga utafanyika
kama marais wa nchi hizo mbili walivyokubaliana.
Wameeleza
kuwa kwa sasa makubaliano yako katika hatua za mwisho ili ujenzi wa
mradi huo kuanza huku nchi za Kenya na Uganda wakiendelea na mazungumzo
katika kufikia mwafaka wa jambo hilo.
Mkurugenzi
Mtendaji wa TPDC, Dk James Mataragio alisema hivi karibuni kumekuwa na
taarifa za mradi huo kukwama kutokana na Kenya kudaiwa kukubaliana na
Uganda kupitisha mradi huo nchini mwao.
Akizungumzia
suala hilo, Dk Mataragio alisema ni kweli awali kulikuwa na makubaliano
ya nchi hizo mbili kupitisha mradi huo Kenya kutoka Hoima hadi Bandari
ya Lamu, lakini kwa sababu mbalimbali Uganda waliamua kupitisha Bandari
ya Tanga.
Alieleza
ingawa umbali kutoka Uganda hadi bandari za Kenya ni karibu kwa
kilometa chache kuliko Tanga zipo sababu zilizofanya bomba hilo
kufikishwa Tanga. Sababu hizo ni pamoja na gharama kubwa za ujenzi
kwenda Kenya na bandari ya Tanga kuwa na kingo za asili hivyo kuweza
kusafirisha mafuta mwaka mzima.
Alisema
pia ujenzi wa bomba hilo hadi bandari ya Tanga haupiti sehemu yenye
makazi ya watu wengi hivyo kupunguza gharama, huku bomba likipita maeneo
mengi ya tambarare bila kuwa na miinuko inayofanya kuongeza gharama za
kupampu.
Alisema
tayari timu za wataalamu zimekutana na kukubaliana masuala kadhaa ya
ujenzi huo pamoja na kusaini mpango wa utekelezaji wa mradi.
Dk
Mataragio alisema kuhusu gharama ni kawaida siyo kubwa kama
inavyoelezwa na baadhi ya watu hivyo ni vema watanzania wakaelewa kuwa
hakuna tatizo la kukwama kwa mradi huo kwa sababu yoyote.
Kampuni
zinazozalisha mafuta nchini Uganda ni Tullow kutoka Ireland, Kampuni ya
Ufaransa ya Total na Kampuni ya CNOC kutoka China.
Wakati
hayo yakielezwa hivi karibuni, Makamu wa Rais wa Kampuni ya Total
Afrika Mashariki, Javier Rielo alimueleza Rais John Magufuli kuwa
kampuni hiyo itaanza ujenzi huo haraka iwezekanavyo, kwa kuwa fedha za
kutekeleza mradi huo zipo.
Bomba
hilo la kutoka Tanga hadi Uganda litakuwa na urefu wa kilometa 1,410 na
litasafirisha mafuta ghafi kutoka ziwa Albert nchini Uganda hadi
Bandari ya Tanga na litajengwa kwa gharama ya Dola za Marekani bilioni
nne.
Unatarajiwa
kuzalisha ajira za moja kwa moja 1,500 na ajira zisizo za moja kwa moja
20,000 huku ukitarajia kukamilika baada ya miaka mitatu hadi minne.
0 comments:
Post a Comment