VIONGOZI
wa dini wa Tanzania Bara na Visiwani wamekutana visiwani Zanzibar na
kuja na tamko juu ya hali ya amani visiwani humo ambalo pamoja na
masuala mengine, wamehimizana kujitenga na siasa za vyama.
Aidha,
viongozi hao kutoka madhehebu ya Kikristo, Kiislamu na Jumuiya ya Hindu
wametaka wananchi watakaoshiriki kupiga kura katika uchaguzi wa marudio
wahakikishiwe amani inatawala na wale ambao hawatashiriki,
wasibughudhiwe na pia wahakikishiwe amani.
Pia
wametaka vyama vya siasa vinavyotoa kauli na taarifa zisizo sahihi na
hivyo kuleta uchochezi viache mwenendo huo ili kudumisha amani kwani
kila mmoja ana wajibu wa kuitetea tunu hii ya taifa.
Kikao
cha viongozi hao kilifanyika juzi visiwani hapa chini ya Baraza la
Viongozi wa Dini mbalimbali kwa Ujenzi wa Amani Tanzania (IRCPT).
Taarifa
iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na baraza hilo, imetaja baadhi
ya viongozi wa dini walioshiriki kuwa ni Askofu wa Kanisa la Anglikana,
Jimbo la Dar es Salaam, Valentino Mokiwa, Askofu wa Jimbo Katoliki la
Zanzibar, Augustino Shao na Shehe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Salum.
Wengine
ni Askofu Dickson Kaganda; Shehe Norman Jongo ambaye ni mfanyakazi,
Ofisi ya Mufti, Zanzibar; Shehe wa Tumbatu, Abdul Yusuf Mzee, Ismail
Asahil na Godda Muyya ambaye ni Mwenyekiti wa Inter religious Peace
Council, Tanzania
Wakizungumzia
hali halisi ya Zanzibar na nini kifanyike kudumisha amani, viongozi hao
walisema viongozi wa dini wajitenge na siasa za vyama kwani wao
wanapaswa kuwa nguzo za jamii zenye imani na asili tofauti, wasuluhishi
na watetezi wa amani nchini.
Walisema wana mashaka kwamba kuna mgawanyiko miongoni mwa jamii unaosababishwa na tofauti mbalimbali zikiwemo za kisiasa.
Baada
ya majadiliano ya kina, mambo mengine waliyoazimia ni kwamba, kwa
kutambua kuwa Zanzibar ni moja na watu wake ni wamoja, amani ni tunu
adhimu kwa Watanzania wote.
Waliwapongeza
Wazanzibari kwa kuwa wavumilivu na kulinda amani katika kipindi cha
kuanzia uchaguzi uliofutwa hadio sasa. Walitaka pia vyombo vya usalama
wawabaini na kuwachukulia hatua vikundi vya uvunjifu wa amani ili
wananchi waishi kwa amani.
Walivitaka
vyombo husika kutumia nguvu inayostahili badala ya kuogopesha umma.
Viongozi hao wa dini wameitaka Tume ya Uchaguzi kuwa waadilifu kusimamia
haki, sheria, kanuni na uwazi kudumisha amani katika kipindi hiki cha
uchaguzi.
Vile
vile wamevitaka vyombo vya habari kusaidia kuhakikisha nchi inapita
kwenye uchaguzi kwa usalama na amani kwa kutoa taarifa sahihi,
kuzingatia maadili na kufuata taratibu na sheria zilizopo.
0 comments:
Post a Comment