WAZIRI
Mkuu, Kassim Majaliwa ametoboa siri ya kuteuliwa mwanajeshi kuongoza
Mkoa wa Kagera, moja ya mikoa iliyoko pembezoni na yenye tishio kubwa la
wahamiaji haramu na matatizo ya ardhi.
Hivi
karibuni, Rais John Magufuli alifanya uteuzi wa wakuu wa mikoa 26 ya
Tanzania Bara na kumteua Meja Jenerali mstaafu, Salum Mustafa Kijuu kuwa
Mkuu mpya wa Mkoa wa Kagera.
Mbali
ya Meja Jenerali mstaafu Kijuu, Rais Magufuli pia aliwateua wanajeshi
wengine watatu kuongoza mikoa ya Katavi, Geita na Kigoma katika uteuzi
huo wa Machi 13.
Hao
ni Meja Jenerali mstaafu, Ezekiel Kyunga (Geita), Meja Jenerali
mstaafu, Raphael Muhuga (Katavi) na Brigedia Jenerali mstaafu Emmanuel
Maganga (Kigoma).
Akifanya majumuisho ya ziara yake ya siku tatu mkoani Kagera wiki iliyopita, Waziri Mkuu Majaliwa alisema: “Hapa kwenu Kagera kuna tatizo kubwa la waharamiaji haramu na uvamizi wa ardhi.
"Wavamizi wengine wanalima bangi katika maeneo yetu badala ya kufuga na kulima.
“Waondoeni au punguzeni maeneo yao na lindeni mipaka yetu. Mapori ya Kimisi na Burigi yamegeuzwa maficho ya wahamiaji haramu,” alieleza Waziri Mkuu.
“Ndio
maana tumemleta Meja Jenerali Kijuu. Shughuli yake huyu siyo nyepesi.
Atatembea mwenyewe huko. Huyu si alikuwa Kamandi ya Infantry (askari wa
miguu), kwa hiyo ataimudu shughuli hii vizuri.”
Mkoa
huo umewahi pia kuongozwa na wakuu wa mikoa ambao ni wanajeshi katika
miaka ya nyuma na baadhi yao ni Abdallah Twalipo, Tumainieli Kiwelu,
Ayoub Simba, Fabian Massawe, Silas Mayunga na Enos Mfuru.
Mkoa
wa Kagera unakabiliwa na tishio kubwa la wahamiaji haramu wanaingia
nchini kutoka nchi jirani na wanamiliki ardhi kinyume cha sheria
kutokana na udhaifu wa viongozi waliokabidhiwa dhamana ya kusimamia.
Unapakana
na Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi. Aidha, Waziri Mkuu aliiagiza Idara
ya Uhamiaji nchini hasa mkoani Kagera kubadilika ambapo alihoji kwa
nini hawavai sare za jeshi lao na kuingia msituni kusaka wahamiaji
haramu badala yake wanavaa suti maofisini.
0 comments:
Post a Comment