Adverts

Saturday, August 27, 2016

JWTZ Lawatoa Hofu Wananchi.......Lasema Septemba 1 Litasherehekea Miaka 52 kwa Kufanya Usafi Mtaani

 
Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) leo linaanza shamrashamra za maandalizi kuelekea siku ya maadhimisho ya 52 ya majeshi inayotarajiwa kufanyika Septemba Mosi mwaka huu kwa kufanya usafi na upandaji miti katika kambi za jeshi na baadhi ya taasisi nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Jijini Dar es Salaam, Msemaji wa JWTZ Kanali Ngemela Lubinga aliwatoa hofu wananchi kuwa wasitishike pindi watakapoona wanajeshi katika maeneo ya karibu na makazi yao.

“Kesho (leo) tuaanza kufanya usafi kuanzia maeneo ya Kawe hadi karibu na kambi ya Lugalo, na kwamba niwatoe hofu wananchi pindi watakapoona wanajeshi wengi mitaani kwa kuwa hatuna nia mbaya hivyo wasitufikilie vibaya,” alisema.

Alisema jeshi hilo litafanya usafi pamoja na upandaji miti katika baadhi ya maeneo nchini hadi siku ya kilele cha maadhimisho hayo. Pia wanajeshi watajitolea damu salama katika hospitali za kambi za jeshi.

“Siku kuu ya majeshi itaadhimishwa pamoja na wanajeshi kujitolea damu kwenye vituo maalumu vya kutolea damu salama mikoani, katika hospitali zetu za kanda,” alisema na kuongeza.

“Sanjari na utoaji damu, madaktari wetu JWTZ watatoa huduma za tiba bure kama upimaji wa virusi vya Ukimwi, kisukari, na upimaji wa shinikizo la damu. “

“Kama ilivyo mila na desturi ya majeshi kufanya usafi na utunzaji wa mazingira, kuelekea siku ya maadhimisho tutafanya usafi na kupanda miti maeneo ya jirani na kambi na kwenye taasisi za kiraia kadri mahusiano yatakavyofanyika na taasisi hizo, ” alisema.

Pia alisema siku hiyo ya maadhimisho itaadhimishwa kwa kuienzi michezo na kudumisha urafiki baina ya JWTZ, wananchi, na Taasisi na kwamba mashindano mbalimbali yatafanyika.
Tarehe hiyo hiyo  ya Septemba 1 , Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetengaza kufanya maandamano na mikutano nchi nzima ili kulaani kile wanachokiita udikteta unaofanywa na serikali ya awamu ya tano.

Tayari tangazo hilo la Chadema limepingwa vikali na Rais John Magufuli, Waziri Mkuu Majaliwa Kassim, Mwigulu Nchemba, Waziri wa Mambo ya Ndani na Nsato Marijani, Kamishina wa Jeshi la Polisi, Operesheni na Mafunzo huku chama hicho kikiendelea kusisitiza azma yake.

0 comments:

Post a Comment