SERIKALI
Mkoa wa Dodoma imesema Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa atahamia rasmi
mkoani humo mara baada ya kumalizika kwa vikao vya Bunge vinavyoanza
wiki ijayo, Septemba 6.
Mkuu
wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana alisema baada ya kufika Dodoma,
ataanza kuratibu utaratibu wa wizara mbalimbali kuhamia katika Makao
Makuu hayo ya nchi.
Pamoja
na hayo Jeshi la Polisi limejipanga kuongeza vituo vya Polisi ili
kuimarisha ulinzi wakati serikali itakapohamia na hakuna mwananchi
atakayenyang’anywa ardhi yake kwa sababu yoyote ile.
Katika
mkutano wake na waandishi wa habari jana, Rugimbana alisema kama mkoa
walishauri ujio huo ufanyike mara baada ya kikao cha Bunge na Waziri
Mkuu ameridhia suala hilo.
Alisema
Waziri Mkuu atakuwa Mratibu wa wizara zote kuhamia Dodoma na kazi hiyo
ataianza rasmi mara baada ya kuwasili mkoani humo.
Alisema maandalizi yanaendelea vizuri na ukarabati wa nyumba ya Waziri Mkuu umefikia asilimia 90.
Alisema Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Christine Mndeme aliyekutana na makundi mbalimbali kwa ajili ya mapokezi ya Waziri Mkuu.
“Awali
tulisema atakuja Septemba Mosi lakini baada ya kushauriana tumeona aje
mara baada ya vikao vya Bunge kwani pilikapilika nyingi zitakuwa
zimepungua, kama serikali ikiamua kuja leo tutaipokea kwani maandalizi
ya serikali kuja Dodoma yamekamilika kwa asilimia 70,” alisema.
0 comments:
Post a Comment