Serikali
ya Awamu ya Tano imedhamiria kuwaunga mkono na kuwatumia wahandisi wa
ndani wenye ujuzi mbalimbali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo
ikiwemo ujenzi wa viwanda, reli, barabara na miundombinu mingine.
Hayo yamesema na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, alipokuwa akifungua Mkutano wa 14 wa mwaka wa wahandisi unaofanyika kwa siku mbili kuanzia leo tarehe 01 Septemba, 2016 katika ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam.
Dkt.
Magufuli amesema atafurahi kuona miradi inayohusisha kazi za kihandisi
na hasa wakati huu ambapo nchi inaelekea katika uchumi wa viwanda
inatekelezwa kwa kutumia wahandisi wa ndani na hivyo amewataka kujipanga
sawasawa ili kukabiliana na changamoto hiyo.
"Nyinyi
wahandisi mkiamua nchi hii iende kwenye uchumi wa kati tutafika,
mkiamua nchi hii iende kwenye uchumi wa viwanda tutafika, na msipoamua
hatutafika.
"Sasa
hivi kuna ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard
gauge) kwani nyinyi mnashindwa kujenga?" Amehoji Rais Magufuli huku
akisisitiza kuwa Serikali yake ipo tayari kuwaunga mkono pale
watakapohitaji msaada.
Hata
hivyo Dkt. Magufuli amewakumbusha umuhimu wa kufanya kazi kwa ubora,
ushirikiano na upendo miongoni mwao huku akielezea kusikitishwa kwake na
baadhi ya wahandisi ambao wamekuwa wakifanya vitendo vya ukiukwaji wa
maadili ikiwemo kushirikiana na wakandarasi na wazabuni kuzidisha
viwango vya makadirio ya gharama za miradi na manunuzi ya Serikali ili
kujipatia fedha isivyo halali na kupitisha miradi iliyojenga chini ya
viwango.
Rais
Magufuli ameongeza kuwa Serikali yake itaendelea kuchukua hatua kali
dhidi ya wote wanaotumia vibaya fedha za umma na amesisitiza kuwa hatua
zaidi za kuhakikisha kunakuwa na nidhamu katika matumizi ya fedha za
Serikali zitachukuliwa.
"Kuna
watu wanasema mzunguko wa pesa umepungua na hali imekuwa ngumu, hizo
pesa zilizokuwa zinachezewa huko mitaani zilikuwa pesa za Serikali, mimi
nataka pesa ziende kwenye miradi ya maendeleo na ndio maana bajeti ya
maendeleo tumeongeza kutoka asilimia 26 hadi asilimia 40" Amesisitiza
Rais Magufuli.
Katika
tukio jingine, Rais Magufuli amewatembelea Askari wa Jeshi la Wananchi
Tanzania (JWTZ) Kikosi cha 603 (Air Wing) kilichopo Ukonga Jijini Dar es
Salaam na kuwapongeza kwa kuadhimisha miaka 52 ya tangu kuanzishwa kwa
Jeshi hilo.
Katika kuadhimisha miaka 52 ya JWTZ Askari wa Jeshi hilo wamefanya usafi katika maeneo mbalimbali.
Pamoja
na pongezi hizo Rais Magufuli amekagua baadhi ya ndege zinazotumiwa na
Jeshi hilo na amewahakikishia Wanajeshi kuwa Serikali yake itaendelea
kuliimarisha Jeshi hilo kwa vifaa na maslai ya Askari ili kuendelea kuwa
na Jeshi bora, la kisasa na lililo tayari kuilinda nchi wakati wote.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es Salaam
0 comments:
Post a Comment