Adverts

Sunday, April 3, 2016

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga amkamua jipu Mhandisi wa manispaa....Amsweka Rumande huku Mkurugenzi wake Akishuhudia

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro amemsweka rumande Muhandisi wa halmashauri ya manispaa ya Shinyanga Simoni Ngagani, baada ya kupuuza agizo lake la kufanya maandalizi mapema ya kununua kokoto na Saruji kwa ajili ya kusimika mapipa 50 ya kutunzia uchafu kwenye mitaa mbalimbali katika manispaa ya Shinyanga ikiwemo eneo la kituo cha mabasi yaendayo wilayani.

Tukio hilo limetokea juzi asubuhi mjini Shinyanga wakati mkuu huyo wa wilaya akiwa na msafara wake alipowasili katika eneo la stendi ya mabasi yaendayo wilayani kwa lengo la kufanya uzinduzi wa kusimikwa kwa mapipa hayo na kukuta maandalizi hayajakamilika.

Matiro alimuagiza Mhandisi huyo kufanya maandalizi hayo mapema mbele ya mkurugenzi wake wa manispaa ya Shinyanga Kalinjuna Lewis, kuwa ataandaa vifaa hivyo majira ya saa moja asubuhi ili zoezi la  kusimika mapipa hayo likamilike haraka, na baada ya hapo wafanye usafi wa mazingira lakini agizo hilo lilipuuzwa na mhandisi huyo .

Mkuu huyo alipomhoji mhandisi kwanini alipuuzia agizo lake la kufanya maandalizi mapema, mhandisi huyo alisema sababu iliyomkwamisha ni kukosekana kwa pesa za kununua kokoto na saruji kwani mvua kubwa ilinyesha na kushindwa kwenda benki, na alivyoamka asubuhi ndipo atakafuta dhana hizo.

Hata hivyo mkuu huyo hakuridhika na majibu hayo ndipo DC alipochukua uamuzi ya kumsweka rumande kwa kumuagiza mkuu wa kituo cha polisi wilaya ya Shinyanga kumkamata na kumuweka ndani mhandisi huyo wa ujenzi manispaa hiyo Samson Ngagani kwa kosa la kuchelewesha maandalizi ya vifaa vya ujenzi vilivyopangwa kutumika kusimika mapipa ya taka.

“Haiwezekani tukubaliane tuamke mapema ili tufanye kazi hii haraka na pia tuingie Mitaani kufanya usafi, ambapo mimi nimeamka saa 11 nikajiandaa harafu wewe una kuja saa mbili tena bila ya kufanya maandalizi yeyote hii ni kunidharau, hivyo naagiza OCD mkamate akakae Rumande kwanza ili liwe fundisho kwa wengine” ,alisema Matiro.

Katika uzinduzi huo Matiro alisema mapipa hayo ya taka ambayo idadi yake ni zaidi ya 50 yatawekwa katika maeneo mbali mbali ya manispaa ya Shinyanga na wananchi wanatakiwa kuyalinda. 
Awali akiongea katika uzinduzi huo, mkurugenzi wa manispaa ya Shinyanga Lewis Kalinjuna alisema mapipa hayo yamepatikana kutokana na wadau mbali mbali kujitolea kuchangia baada ya kuhamasishwa na mkuu huyo wa wilaya ambapo pipa moja limegharimu shilingi elfu 90.

Naye afisa afya wa manispaa ya shinyanga Elly Nakuzelwa alisema lengo la kuweka mapipa hayo ya taka ni kuhakikisha manispaa ya Shinyanga inakuwa katika hali ya usafi ili kuondoa magonjwa ya miripuko yanayosababishwa na uchafu ikiwemo kipindupindu. 
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akimhoji Mhandisi wa ujenzi wa manispaa ya Shinyanga Simon Ngagani (katikati mwenye kaunda suti)kwa kupuunza agizo lake la kufanya maandalizi mapema ya kununua vifaa vya ujenzi vya kusimikia Mapipa ya uchafu 50 katika mitaa mbalimbali ya Mji wa Shinyanga ,na mwenye traksuti kushoto ni Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Kalinjuna Lewis akishuhudia Mtumishi wake akikamuliwa Jipu na hatimaye kuswekwa rumande kwa kumpuuza DC huyo

0 comments:

Post a Comment