Wakala
wa mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) na wadau wake wameagizwa
kuzimaliza changamoto zinazochelewesha kuanza kwa mradi huo ili huduma
ya usafiri iweze kuanza haraka iwezekanavyo.
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),
Bw. George Simbachawene alitoa agizo hilo mwishoni mwa juma katika
kikao chake na uongozi wa wakala pamoja na wadau wake.
“Kuna baadhi ya changamoto ndogondogo zimebaki...nimetaka wazimalize haraka ili mabasi yaanze kutoa huduma,”
Bw. Simbachawene aliwaambia waandishi wa habari mara baada ya kikao
hicho. Mradi huo uliosubiriwa kwa muda mrefu unatarajiwa kuanza mwezi
huu wa Nne.
Aliwataja
baadhi ya wadau wanaotakiwa kufanya kazi na wakala huo kuhakikisha kuwa
mradi unaanza kuwa ni Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Wakala wa
Usafiri wa Majini na Nchi kavu (SUMATRA), Jeshi la Polisi Kikosi cha
Usalama Barabarani, Wakala wa Serikali Mtandao (EGA), Msajili wa
Hazina, UDA-RT na MAXCOM.
Changamoto
zinazotakiwa kutatuliwa kwa haraka ni pamoja na kukwama kwa baadhi ya
vifaa vya mradi kutokana na kutolipiwa katika Mamlaka ya mapato (TRA),
kuweka mifumo ya nauli na kadi zake, umeme, kujenga uzio katika vituo,
kuongeza ulinzi na ofisi ya kuongozea mabasi.
Aliwataka
uongozi wa wakala wa DART kumpatia ripoti ya maendeleo kila baada ya
siku mbili kwake ili na yeye aweze kupeleka ripoti kwa Waziri Mkuu kila
wiki.
“Tutaendelea kuwa na vikao vya kila siku, siku mbili na kila wiki hadi hapo huduma hii itakapoanza kufanya kazi,” alisema.
Tayari mabasi mawili yameshaanza kufanya majaribio na idadi inatarajia kuongezeka hivi karibuni.
Kaimu
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa DART, Mhandisi Ronald Lwakatare alisema
kikao hicho kilikuwa na mafanikio na ni njia nzuri ya kuharakisha yale
yanayotakiwa kukamilishwa haraka ili mradi huo uanze.
“Tumejipanga na wadau wote wameitikia wito, tunataraji mradi utaanza kutoa huduma kwa wananchi haraka,”alisema Bw. Lwakatare.
Aliwataka
wakazi wa jiji kuendelea kuwa watulivu na kuvuta subira kwani mradi wao
umeiva na wataanza kuona matunda yake hivi karibuni kwa kuwa yaliyobaki
ni mambo madogomadogo.
“Pia
tunawaomba waendelee kutoa ushirikiano wa kuilinda miundombinu, kwenye
vituo kuna vitu vingi vinafungwa, wasiwe chanzo cha uharibifu,” alisema.
Alisisitiza kuwa watu wasiwe chanzo cha hujuma kwani kufanya hivyo ni kuhujumu taifa lao wenyewe.
0 comments:
Post a Comment