Adverts

Showing posts with label Afrika. Show all posts
Showing posts with label Afrika. Show all posts

Thursday, September 1, 2016

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Azindua Ripoti Ya Hali Ya Hewa Barani Africa

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa Afrika wajiulize wanaweza kuchangia kitu gani katika kuboresha maisha ya mamilioni ya wakazi wa bara hilo.

Ametoa kauli hiyo Alhamisi, Agosti 31, 2016 usiku  wakati akizungumza na wawakilishi wa taasisi za kimataifa waliohudhuria uzinduzi wa taarifa ya Taasisi ya Kuboresha Mazingira ya Uwekezaji barani Afrika (ICF) uliofanyika kwenye hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo alisema taasisi hiyo imesaidia kukuza uwekezaji kupitia miradi katika nchi mbalimbali za Afrika kwa kuimarisha mifumo ya ukusanyaji kodi, usajili wa biashara za wajasiriamali na upatikanaji wa leseni za biashara.

“Kutokana na kazi inayofanywa na taasisi hii, hali ya uwekezaji katika nchi nyingi imeimarika na bara la Afrika limekuwa mbia kwa wawekezaji kutokana na ushirikiano baina ya Serikali za nchi husika na sekta binafsi. Uchumi wa nyingi za Afrika umeimarika kuliko hapo awali,” alisema.

Akitoa mfano, Waziri Mkuu alisema zaidi ya wajasiriamali 500 kutoka Tanzania walipatiwa mafunzo kwa ushirikiano baina ya ICF, Serikali na ESAURP ili kuwajengea uwezo waweze kufanya biashara zao kwa tija zaidi. “Mafunzo hayo yaliwalenga wajasiriamali wadogo na wa kati ambao wanajihusisha na uvuvi, biashara za rejereja na jumla kutoka mikoa ya Mwanza na Dar es Salaam”.

“Kupitia mafunzo hayo, wajasiriamali hao waliweza kusajili biashara, kurasimisha biashara zao, kuongeza mitaji na kujua namna ya kutunza taarifa za biashara zao,” alisema.

Mapema, Mwenyekiti Mwenza wa taasisi hiyo ambaye pia ni Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Mhe. Benjamin Mkapa alisema kuna haja ya wananchi kubadili mitazamo yao juu ya sekta binafsi kwani nayo ni muhimu katika ujenzi wa uchumi kwa nchi yoyote ile.

“Watu wengi wanahisi kwamba wawekezaji ni wabaya. Hii si kweli. Tunapaswa kujenga mazingira ya kuwakubali kwa sababu wanakuja na mitaji yao na wao wanawakilisha michango kutoka kwa mamilioni ya wafanyakazi kutoka kwenye nchi zao. Hatupaswi kuwaona kwamba ni maadui,” alisema.

Alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais Mstaafu wa Serikali ya awamu ya nne, Mhe. Jakaya Kikwete kwa uamuzi wake wa kukubali kuiruhusu taasisi hiyo ya ICF iweke makao yake makuu hapa nchini wakati ilikuwa imeshakataliwa kufanya hivyo katika nchi nyingi ambako ilipeleka maombi yake.

Aliwataka viongozi mbalimbali watumie uzoefu uliowekezwa na taasisi hiyo kwenye uboreshaji wa mifumo ya mahakama na ukusanyaji kodi, utoaji wa leseni, urasmishaji wa biashara za wajasiriamali wadogo.

“Tunayo maeneo mengi ambayo tumefanya vizuri iwe ni katika TEHAMA, miundombinu, mahakama au mambo ya forodha. Uamuzi ni wenu juu ya jambo lipi muanze nalo katika kuboresha huduma ili kuharakisha maendeleo ya bara hili,” alisema.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,

ALHAMISI, SEPTEMBA MOSI, 2016

Tanzania yateuliwa kuwa Mwenyekiti wa Siasa, Ulinzi na USalama wa Nchi za SADC


Mkutano wa Wakuu wa nchi na Serikali umemalizika katika mjini Mbabane Swaziland ambapo Tanzania imeteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Asasi muhimu na nyeti ya Siasa, Ulinzi na USalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika- SADC- (SADC Organ On Politisc, Defence and Security Cooperation) ambapo nchi ya Angola imeteuliwa kuwa Makamu mwenyekiti wa asasi hiyo.

Jukumu kubwa la asasi hiyo litakuwa ni kuangalia masuala yote yanahusiana na Siasa, ulinzi na usalama katika ukanda wa SADC huku changamoto kubwa ikiwa ni namna ya kutafuta suluhu ya kudumu hususani katika eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo- DRC na Lesotho.

Akizungumzia mambo muhimu yaliyojiri kwenye Mkutano huo wa 36 wa SADC mjini Mbabane – Swaziland, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia  Suluhu Hassan ambaye alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Magufuli amesema mkutano huo umekuwa wa mafanikio makubwa na amehimiza ushirikiano miongoni mwa nchi wanachama katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa nchi wanachama wa SADC kwa sasa zinatakiwa kuongeza juhudi katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi na kuzitafutia ufumbuzi haraka kama hatua ya kujenga ustawi bora wa wananchi wa kanda hiyo.

Kuhusu Mpango wa Mfalme wa Swaziland wa III wa kujenga Chuo Kikuu cha SADC nchini mwake kabla ya mkutano ujao wa SADC hapo mwakani chuo ambacho kwa kuanzia kitatoa ufadhili wa masomo ya Sayansi,Ugunduzi na Utafiti kwa wanafunzi wanaotoka kwenye nchi wanachama wa SADC, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema mpango huo ni mzuri na utasaidia kutoa wataalamu wengi hasa wanasayansi katika ukanda wa SADC na serikali ya Tanzania inaunga mkono mkakati huo.

Kuhusu Tanzania kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama kwa nchi za SADC, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Kikanda na Kimataifa Dkt Augustine Mahiga amesema Tanzania itahudumu katika asasi hiyo kwa mwaka MMOJA na anaimani kuwa changamoto za kisiasa zilizopo katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Lesotho zipatiwa ufumbuzi.

Mkutano wa wakuu wa nchi na serikali wa SADC pia umeiteua nchi ya Swaziland kuwa mwenyekiti wa SADC na Jamhuri ya Afrika Kusini imeteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa SADC.

Katika mkutano huo wakuu wa nchi na serikali wametia saini rasimu za maboresho ya mikataba mbalimbali ya jumuiya hiyo ikiwemo mkataba wa kuboresha itifaki ya SADC dhidi ya rushwa, maboresho ya itifaki ya ushirikiano wa siasa, ulinzi na usalama ya SADC na maboresho ya itifaki ya biashara.

Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
Mbabane
Swaziland

1-Sep-16

Wednesday, August 31, 2016

Fujo Gabon baada ya Bongo kutangazwa mshindi

Majengo ya bunge mjini Libreville

Fujo zimezuka katika mji mkuu wa Gabon, Libreville baada ya Rais Ali Bongo kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanyika Jumamosi.

Mgombea wa upinzani Jean Ping amesema watu wawili wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa baada ya vikosi vya usalama kuvamia makao makuu ya chama chake.

Serikali imesema inawaandama "wahalifu wenye silaha" ambao awali walikuwa wameteketeza majengo ya bunge.

Bw Ping amepinga matokeo ya urais ambayo yalionyesha Rais Bongo alishinda uchaguzi kwa kura chache. Hii inampa fursa ya kuongoza taifa hilo kwa muhula mwingine wa miaka saba.

"Walishambulia mwendo wa saa 01:00 (00:00 GMT). Ni kikosi cha wanajeshi walinzi wa rais. Walikuwa wanarusha mabomu kutoka kwa helikopta na kisha baadaye wakashambulia kutoka ardhini," Bw Ping, ambaye hakuwa katika makao makuu hayo wakati huo, alisema awali.

Ameomba usaidizi kutoka kwa jamii ya kimataifa kulinda raia.



Wafuasi wa Bw Ping walikabiliana na polisi

Wafuasi wa Jean Ping

Wanajeshi waliitwa kukabiliana na waandamanaji

Matokeo ya uchaguzi yalitangazwa Jumatano alasiri na kumpatia Bw Bongo ushindi kwa 49.8% ya kura, akifuatwa na Bw Ping aliyepata 48.2 % ya kura, kura zilizowatenganisha zikiwa 5,594.

Bw Ping alisema uchaguzi huo ulijaa udanganyifu na "hakuna ajuaye" hasa nani alishinda.

Waandamanaji waliingia barabarani muda mfupi baada ya tangazo kutolewa. Walichoma moto majengo ya bunge na kukabiliana na polisi wa kuzima fujo.

Upande wa Bw Ping unasema takwimu kutoka ngome za rais huyo zinaonyesha asilimia 99 ya wapiga kura walijitokeza. Ameomba takwimu za wapiga kura kutoka kila kituo zitolewe wazi.

Marekani na Umoja wa Ulaya wametoa wito kura hizo ziwekwe wazi huku katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon naye akihimiza utulivu.

Bw Bongo aliingia madarakani mwaka 2009, baada ya kifo cha babake aliyechukua madaraka 1967.

Kabla ya kuingia kwenye siasa, Bw Ping alikuwa mwanadiplomasia ambaye alihudumu kama mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika.

Chanzo: BBC Swahili

Tuesday, August 30, 2016

UN: Viongozi wa Sudan Kusini wawajibike


Filippo Gand


Afisa wa ngazi ya juu wa shirika la Umoja wa Mataifa la huuma kwa wakimbizi, Filippo Grandi, amewatolea wito viongozi wa Sudan Kusini kumaliza mateso ya watu wao.

Bw Grandi alikua akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukutana na wakimbizi Kutoka Sudan Kusini wanaoishi kambini magharibi mwa Uganda. 

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanakadiria kuwa zaidi ya watu 80,000 wamewasili nchini Uganda tangu kuibuka kwa mapigano ya hivi karibuni nchini humo.
Alisema: " Viongozi wa taifa lile changa wanapaswa kuwajibika."

Vikosi vya wanajeshi watiifu wa viongozi wanaohasimiana kisiasa walikabiliana kisiasa katika mji mkuu, Juba, mwezi uliopita, suala linalozorotesha mchakato wa amani uliolenga kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

Chanzo: BBC Swahili

Tuesday, March 1, 2016

Rais Mstaafu wa awamu ya nne Mhe. Jakaya Kikwete akubali kuwa balozi wa chanjo Afrika

RAIS mstaafu Jakaya Kikwete amekubali uteuzi wa kuwa Balozi wa Heshima wa kuhamasisha masuala ya afya na kuwataka Wakuu wa Nchi za Afrika kuweka kipaumbele katika upatikanaji wa huduma za afya katika jamii.


Kikwete aliyasema hayo mjini Addis Ababa nchini Ethiopia juzi, wakati akitoa salamu zake baada ya kukubali kuwa Balozi wa Heshima wa ‘Africa United’ kupitia Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na Gavi.

United Africa ni mpango uliobuniwa kusaidia uhamasishaji wa masuala ya afya ukiongozwa na Gavi, CAF, Umoja wa Afrika, Benki ya Dunia na CDC Foundation na wameamua kutumia michezo kama nyenzo mojawapo ya kufanya kampeni ya kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa masuala ya afya yanayolikabili bara la Afrika.

Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Jopo la watu mashuhuri la kumshauri Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa juu ya namna bora ya kuendeleza na kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu hususani katika afya ya uzazi ya mama na mtoto, alisema upatikanaji wa chanjo utasaidia kuokoa vifo vingi vya watoto Afrika.

Uteuzi huo umekuja huku Rais huyo mstaafu akiteuliwa pia kuwa Mjumbe Maalumu wa AU nchini Libya.

Saturday, February 27, 2016

Shambulio la al-Shabab lawauwa watu 9



Polisi katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu wanasema kuwa wanamgambo wa al-Shabab wamewaua takriban watu 9 wakati wa shambulizi kwenye hoteli moja iliyo karibu na ikulu ya rais.

Ripoti zinasema kwa mshambuliaji wa kujitolea muhanga aliendesha gari katika lango la hoteli hiyo kabla ya watu waliokuwa na silaha kuingia ambapo ufyatulianaji wa risasi ulianza na walinzi wa hoteli.

Kundi la wanamgambo la Al Shabaab linesema kuwa liliendesha shambulizi hilo.

Al Shabab walikuwa wikidhibiti sehemu nyingi za mji wa Mogadishu kabla ya kuondoka lakini wanaendesha mashambulizi ya mara kwa mara.

Chanzo: BBC Swahili