Adverts

Tuesday, October 4, 2016

Wananchi Walioua Watafiti Wakimbia Kijiji Wakihofia kukamatwa na Jeshi la Polisi........Miili Ya Marehemu Yaagwa Jijini Arusha

Baada  ya baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Iringa Mvumi katika  Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma kuwaua watafiti wa Kituo cha Udongo na Maendeleo cha Selian Arusha, wakazi wa kijiji hicho wamehama makazi yao wakihofia kukamatwa na Jeshi la Polisi.

Waandishi wa habari waliofika kijijini hapo jana na walishuhudia hali ya utulivu kijijini hapo tofauti na ilivyozoeleka.

Pamoja na wananchi hao kukimbia makazi yao, taarifa zinasema viongozi wote wa Serikali ya Kijiji hicho  wamekamatwa na polisi wakiwamo Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji, Albert Chimanga na Diwani wa Kata ya Iringa Mvumi, Robert Chikole.

Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho aliyejitambulisha kwa jina la Michael Kagisi, alisema kitendo cha wananchi kukimbia kijiji hicho kimesababisha shughuli nyingi za  jamii kusimama   na maduka kufungwa.

Kwa mujibu wa Kagisi, hata wananchi   waliobaki kijijini hapo wakisema    hawakushiriki mauaji hayo, ikifika jioni wanakwenda porini kulala.

“Sehemu kubwa ya watu wameyakimbia makazi yao kwa sababu wanaogopa kukamatwa na polisi, yaani hata shule hazina wanafunzi kwa sababu wengi wamekimbia na wazazi wao.

“Yaani waliouawa waliuawa kwa makosa kwa sababu  kabla ya kuwapiga, walijitetea na kujitambulisha, lakini wananchi hawakutaka kuwasikiliza…   baada ya kuwaua, waliwawekea majani na kuwachoma moto ili wafe haraka,” alisema Kagisi.

Akifafanua, mwananchi huyo alisema siku ya tukio ulikuwapo mkutano kijijini hapo na mwenyekiti wa kijiji alipata taarifa kwamba katika eneo la kutengeneza chumvi, kuna gari ambalo walilitilia shaka kwamba huenda ni majambazi.

“Siku hiyo tulikuwa kwenye mkutano na baadaye tulimuona mwenyekiti akiwaita baadhi ya vijana na kuwaagiza waende eneo la tukio.

“Wale vijana walikwenda huko  walipiga simu kijijini kuwaeleza wananchi, kwamba kuna gari la watu ambao hawaeleweki.

“Taarifa hizo ziliposambaa, wananchi walihamasishana na kuelekea eneo la tukio.

“Walipofika tu, walianza kuwapiga, lakini wale watafiti walijieleza kwamba wao siyo majambazi, huku wakiwaomba wananchi wawapeleke katika ofisi zao za kijiji, lakini wananchi walikataa na kuendelea kuwapiga hadi walipowaua,” alisema.

Naye  Mchungaji wa Kanisa la Biblia kijijini hapo, Donald Nyambuya, alisema kwa sasa maisha kijijini hapo ni ya shida kwa sababu huduma nyingi za  jamii zimefungwa baada ya watu kukimbia makazi yao.

Mwinjilisti wa Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA), Jacob Foda, alisema kitendo cha watu kukimbia makazi yao  kimeathiri huduma ya  roho kwa kuwa huwa na kawaida kuwatembelea waumini wake.

Wakati huohuo, simanzi na majonzi, jana, vilitawala wakati wa kuaga miili ya Watafiti wa Kituo cha Utafiti wa Udongo na Maendeleo cha Selian mjini hapa.

Watafiti hao waliuawa juzi na wananchi wa Kijiji cha Iringa Mvumi, wilayani Chamwino, Mkoa wa Dodoma kwa kukatwakatwa mapanga na kuchomwa moto.

Miili hiyo iliwasili mjini hapa jana asubuhi kwa gari ikitokea Dodoma na kuingizwa kwenye eneo la wazi la kituo hicho kilichopo pembeni mwa Uwanja mdogo wa Ndege wa Arusha kwa ajili ya wafanyakazi kutoa heshima za mwisho.

Shughuli ya kuaga miili hiyo ilifanyika asubuhi kwa wafanyakazi, jamaa na marafiki kutoa heshima za mwisho bila majeneza kufunguliwa kwa kuwa imeharibika.

Baadaye  ilipelekwa katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru kwa ajili ya kufanyiwa maandalizi ya kusafirishwa.

Waliouawa katika tukio hilo  walitambuliwa kuwa ni Jaffari Mafuru aliyesafirishwa jana kwenda Mara kwa mazishi, Theresia Ngume, aliyetarajiwa kuzikwa jana mjini Arusha na dereva wa gari walilokuwamo,       STJ 9570 aina ya Toyota Hilux, mali ya Kituo cha Utafiti cha Selian, Nikas Magazine, aliyesafirishwa kwenda Ifakara, Morogoro kwa mazishi.

Watafiti hao  waliuawa wakiwa katika kazi ya mradi unaoandaa taarifa za hali ya udogo kwa nchi nzima.

Akizungumza baada ya kutoa heshima za mwisho, Mkurugenzi wa Kituo hicho, Januari Mafuru ambaye ni baba mzazi wa marehemu Jaffari, alisema tukio hilo limemuumiza sana.

Alisema kituo hicho kimekuwa kikiendesha mradi huo kwa lengo la kuwasilisha taarifa hizo kwa wakulima wadogo na wataalamu wa kilimo  ziweze kuwasaidia wananchi katika kilimo na hatimaye kuongeza mazao.

“Mradi huu umemaliza utafiti katika Mikoa ya Kanda ya Kaskazini ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara. Baada ya hapo kazi nyingine ilikuwa imeanza Kanda ya Kati Dodoma na Singida.

“Wiki iliyopita, tuliandaa watafiti wanane na magari yao manne kwa ajili ya kwenda mkoani Dodoma kukusanya udongo kwa ajili ya kuuleta hapa kwenye maabara za Seliani kufanyiwa utafiti kisha kutoa matokeo yatakayowarudia wakulima,” alisema Mafuru.

Akizungumzia kuwasili kwa watafiti hao katika Kijiji cha Iringa Mvumi, wilayani Chamwino yalikotokea mauaji hayo, Mafuru alisema timu zote zilikuwa na barua za utambulisho pamoja na vifaa vya kazi.

“Timu iliyokuwa Chamwino katika Kijiji cha Iringa Mvumi, iliwakuta wanawake wakiendelea na shughuli za kukusanya chumvi  na watafiti waliwasilimia na kujitambulisha wametokea wapi.

“Taarifa tulizonazo ni kwamba, baada ya kusalimia, watafiti waliacha gari pembeni na kutembelea maeneo   kuchagua udogo.

“Huku nyuma kundi la wale wanawake lilitoa taarifa kwa viongozi wao kuwa wamevamiwa na wanyonya damu, ndipo walipotokea watu wakiwa na mashoka na mapanga na   kuwashambulia kabla ya kuwachoma moto,” alisema.

Mtafiti Mwandamizi wa Kituo cha Selian, Dk. Lameck Makoye, alilaani mauaji hayo na kusema hajawahi kuona wala kusikia watafiti wakivamiwa   wanapokuwa   vijijini.

“Naamini Serikali imeona, binafsi sijawahi kuona tukio la aina hii kwa sababu  watafiti wale walikuwa na vielelezo vyote vinavyowatambulisha.

“Hata mradi waliokwenda kufanya ulikuwa ni kwa faida ya wananchi wa Kijiji cha Iringa Mvumi kwa vile umelenga maeneo ya nchi nzima.

“Sisi Kituo cha Utafiti cha Selian ndiyo tunaoleta maendeleo ya mkulima kwa nchi nzima kwa kufanya utafiti wa udongo unaomwezesha mkulima alime vipi na atumie mbolea kwa kiwango gani na ya aina gani,” alisema Dk. Makoye.

Mume wa marehemu Theresia, Jonas Mjema, akizungumza kwa huzuni kuhusu  kuondokewa na mkewe, alisema kabla ya tukio la mkewe kuchomwa moto, alizungumza naye asubuhi kujua anaendeleaje.

“Niliwasiliana naye asubuhi Jumamosi tukatakiana kazi njema, ilipofika jioni nilimtafuta lakini simu yake haikupatikana.

“Nilijipa matumaini labda mawasiliano hayakuwa mazuri kwa vile shughuli zao ni za porini.

“Ilipofika Jumapili, nilipigiwa simu na shemeji yangu akinipa taarifa za tukio la kuchomwa moto mke wangu,” alisema Mjema aliyeachwa na watoto wawili.

Aliyetoa taarifa za maiti kufufuka ikiwa mochwari Singida ashikiliwa na Polisi

Jeshi la polisi mkoa wa Singida, linamshikilia askari mgambo mwajiriwa hospitali ya mkoa, MG 7822 Emmanuel Daghau (42) kwa tuhuma ya kutoa taarifa za uongo juu ya maiti kufufuka ikiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya mkoa.

Imedaiwa kuwa uongo huo ulizua mtafaruku mkubwa kwa ndugu na jamaa wa merehemu Rahel Erasto (28), aliyekuwa mkazi wa Minga manispaa ya Singida.

Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Singida, SSP Mayala Towo, alisema tukio hilo limetokea Septemba, 30 mwaka huu, majira ya alasiri huko katika hospitali ya mkoa mjini hapa.

Akifafanua, kaimu kamanda huyo alisema kuwa Septemba, 29 mwaka huu Rahel (marehemu) alifikishwa katika hospitali hiyo ya mkoa, kwa ajili ya kupata huduma za kujifungua salama.

“Kutokana na sababu za kitabibu Rahel, alishindwa kujifungua kwa njia ya kawaida na hivyo ililazimika kufanyiwa upasuaji ambapo mtoto wa kiume alitolewa akiwa hai, Lakini mama kwa bahati mbaya alifariki dunia usiku saa saba Septemba, 30. Mimba hiyo ilikuwa ya kwanza kwa marehemu Rahel,” alisema kaimu kamanda huyo.

Akifafanua zaidi, alisema kuwa baada ya Rahel kufariki dunia, mwili wake ulipelekwa mochwari ambapo kesho yake, ndugu walijikusanya eneo hilo wakijadiliana namna kuuchukua mwili kwa ajili ya kwenda kuzika.

Alisema kuwa wakati ndugu wakiendelea kuzungumzia masuala ya mazishi, alijitokeza mlinzi Daghau na kuwaeleza kuwa ndugu yao huyo, alifariki kutokana na uzembe na kwamba usiku akiwa kwenye doria za kawaida, alisikia marehemu akipiga chafya na aliposogelea dirishani, alimwona akiwa amefufuka.

Towo alisema kuwa awali mgambo huyo baada ya kuhojiwa na Polisi, alikiri kumwona marehemu huyo akiwa amefufuka na alisikia akipiga chafya. Alikiri kwa maandishi na kuweka saini yake.

Alisema lakini baada ya Emmanuel kubaini kuwa baadhi ya ndugu wa marehemu na watoa huduma za afya hospitali ya mkoa kudai kuwa Rahel amefariki dunia kutokana na matatizo ya kawaida ya uzazi na wala hakufa na kufufuka, alipohojiwa mara ya pili, alikana maelezo yake ya awali aliyotoa kwa Polisi.

Wifi wa marehemu Rahel, Mary Mpaki, alikiri kuwa alimsikia mlinzi Emmanuel wakati akiwatangazia waombolezaji kuwa marehemu amefariki dunia kutoka na uzembe wa madaktari, na kwamba alipelekwa chumba cha kuhifadhia maiti akiwa hai.

“Kama ndugu wa marehemu ambao baada ya kufanyiwa upasuaji kuna ndugu ambao walitaka kulala wodini lakini hawakuruhusiwa.Tuliposikia maneno ya mlinzi huyo, tuliamini kwa asilimia mia moja maneno yake kwamba Rahel alipelekwa mochwari akiwa bado yu hai,” alisema kwa masikitiko.

Mary alisema baada ya taarifa ya mlinzi huyo, walienda moja kwa moja kituo cha Polisi kutoa taarifa hizo za kusikitisha.

Ndugu wa marehemu ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema taarifa iliyotolewa na mlinzi kuwa Rahel alifufuka na kupiga chafya, zitakuwa ni za ukweli kwa sababu Ni mtu mwenye akili, hawezi kudanganya jambo hilo.

“Tunasikia kwamba mlinzi kala matapishi yake kwa kitendo cha kukanusha taarifa alizotoa awali kituo cha Polisi. Kama amefanya hivyo, itakuwa kuna shinikizo amepata hivyo anatafuta njia ya kujiokoa,” alisema.

Kaimu mganga mkuu wa mkoa, Dk.Ramadhani Kabala, alikiri kuwepo kwa taarifa hizo na kudai kwa sasa mwili wa marehemu unaendelea kufanyiwa uchunguzi, ili kutambua kama kweli Rahel alifufuka na kupiga chafya akiwa ndani ya chumba cha kuhifadhia maiti.

“Ingawa si rahisi binadamu kufufuka baada ya kufariki dunia, lakini hatuwezi kuzipuuza taarifa hizi za mlinzi. Ipo timu inaongozwa na daktari bingwa kutoka wiraza ya mambo ya ndani, Dk.Ahmed Makata inaendelea na uchunguzi wa kina. Kwa hiyo baada ya kumalizika kwa uchunguzi, tutawaita waandishi wa habari kuwaeleza ukweli ili muweze kuitaarifu jamii,” alisema Dk.Kabala.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Singida, Mhandisi Mathew Mtigumwe, alikiri kupokea taarifa hiyo ya aina yake, na kwamba zipo timu mbili zinaendelea na kuchunguzi ili ukweli uweze kubainika.

Na Nathaniel Limu, Singida

UPDATED!: List Ya Vyuo Vilivyotoa Selection Ya Majina Ya Wanafunzi Waliochaguliwa Vyuo Vikuu Mbalimbali 2016/2017


Kuona Majina Ya Wanafunzi Waliochaguliwa Chuo Kikuu 2016/2017,
 
 ==>Chuo Kikuu Arusha    <<bonyeza Hapa>>

==>Chuo Cha Mipango Dodoma   <<bonyeza Hapa>>


==> Sokoine University- SUA   <<Bofya Hapa>>

==>Chuo Kikuu Suza-zanzbar  <<bonyeza Hapa>>

==>Chuo Kikuu Saut-mbeya      <<bonyeza Hapa>>


==>Chuo Kikuu Saut-arusha     <<bonyeza Hapa>>
 
==>Chuo Cha MUM-Morogoro(2nd Round)   <<bonyeza Hapa>>

==>Chuo Cha Ushirika-moshi MUCCOBS(MoCU)   <<bonyeza Hapa>>

==>Chuo Cha Maji-ubungo    <<bonyeza Hapa>>

==>Chuo Cha Tumaini- Dar  << bonyeza Hapa>>

==>Chuo Kikuu Ardhi    <<bonyeza Hapa>>

==>Chuo Kikuu Sekomu     <<bonyeza Hapa>>

==>Chuo Cha Mweka-moshi      <<bonyeza Hapa>>

 ==> 
Chuo Kikuu St. John's Dodoma    <<Bonyeza  Hapa>>

==> Chuo cha Tax Management- ITA  <<Bonyeza Hapa>>

==> Chuo Kikuu Huria -OUT  <<Bonyeza Hapa>>
 
==> TEKU     <<Bonyeza Hapa>>
 
 ==>Chuo Kikuu Ruaha    <<Bonyeza Hapa>>
 
==> Chuo Kikuu Iringa    << Bonyeza Hapa>>
 
==> Chuo kikuu Bugando  <<Bonyeza Hapa>>
 
==>Chuo  Kikuu Cha Mwalimu Nyerere   <<bonyeza Hapa>> 

==>Chuo  Kikuu Cha  Udsm,duce Na Muce   <<bonyeza Hapa>> 

==>Chuo  Kikuu Cha  Tumaini Makumira    <<Bonyeza Hapa>>   

==>Chuo  Kikuu Cha Udom  <<bonyeza Hapa>>

 ==>Chuo  Kikuu Cha Ifm <<bonyeza Hapa>>

==>Chuo Kikuu Marian << Bonyeza Hapa>>

 ==>Chuo Kikuu Cbe        << Bonyeza Hapa>>

==>Tumaini-mbeya     << Bonyeza Hapa>> & <<hapa>>

 ==>Chuo Kikuu Mum         << Bonyeza Hapa>>

==>Chuo Mum(Diploma) <<Bonyeza Hapa>>

 ==>Chuo- Stella Maris   << Bonyeza Hapa>>

 ==>Chuo- Kampala-kiu  << Bonyeza Hapa>>

Monday, October 3, 2016

Rais Magufuli Akutana Na Makamu Wa Rais Wa Jamhuri Ya Cuba, Ikulu Jijini Dar Leo

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 03 Oktoba, 2016 amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Cuba Mhe. Salvador Antonio Valdes Mesa ambapo viongozi hao wamekubaliana kuimarisha na kuongeza uhusiano na ushirikiano kati ya nchi hizi mbili kwa manufaa ya wananchi wake.

Katika Mazungumzo hayo Rais Magufuli amesema anatambua uhusiano na ushirikiano mzuri na wa kihistoria uliopo kati ya Tanzania na Cuba na kwamba Serikali yake imejipanga kuhakikisha uhusiano huu unaelekezwa katika maeneo yenye manufaa ya kiuchumi na ustawi wa jamii.

Rais Magufuli amemuomba Makamu huyo wa Rais wa Cuba kuwashawishi wawekezaji wa kutoka nchini mwake kuja hapa nchini kujenga viwanda vya kutengeneza dawa za binadamu ili kurahisisha upatikanaji wa dawa na kupunguza gharama.

Pia, Rais Magufuli amemuomba Makamu wa Rais wa Cuba Mhe. Salvador Antonio Valdes Mesa kuwashawishi wafanyabiashara wa Cuba kuja kuwekeza katika uzalishaji wa sukari na amewahakikishia kuwa wakiwa tayari Serikali ya Tanzania ipo tayari kuwapa ardhi kwa ajili ya kuendesha uzalishaji huo.

"Mhe. Salvador Antonio Valdes Mesa najua kuwa nchi yenu ina utaalamu wa kutosha katika uzalishaji wa sukari, uzalishaji wa dawa za binadamu na masuala mengine mengi yanayohusu matumizi ya teknolojia katika shughuli mbalimbali za uzalishaji, nakuomba uwaambie wafanyabiashara wa Cuba kuwa tunawakaribisha waje Tanzania kuwekeza na Serikali itawapa ushirikiano wa kutosha" amesema Rais Magufuli.

Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Cuba Mhe. Salvador Antonio Valdes Mesa amempongeza Rais Magufuli kwa juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali yake katika kuinua uchumi wa Tanzania na amemhakikishia kuwa Cuba ipo tayari kushirikiana na Tanzania kwa kutumia utaalamu na uzoefu wake.

Amesema kwa kuanzia Cuba italeta wataalamu kwa ajili ya kuangalia namna itakavyotekeleza ombi la kujenga viwanda vya kutengeneza dawa za binadamu na pia atazungumza na Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Cuba na kuwashawishi kuja hapa nchini kuwekeza katika uzalishaji wa sukari.

"Mhe. Rais Magufuli natambua kuwa uhusiano wetu na Tanzania na Afrika ni wa kihistoria, sisi Cuba tumepiga hatua kubwa katika maendeleo ya uchumi na teknolojia, nimekuja kukuhakikishia kuwa tutauendeleza uhusiano huu ili ulete manufaa kwenu na kwa wananchi wa Cuba" amesema Mhe. Mesa.
 

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
03 Oktoba, 2016

Rais MagufuliJP amteua Prof. Lawrence Mujungu Museru kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 03 Oktoba, 2016 amemteua Prof. Lawrence Mujungu Museru kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, Ikulu Jijini Dar es Salaam imeeleza kuwa uteuzi wa Prof. Lawrence Mujungu Museru umeanza jana tarehe 02 Oktoba, 2016.

Kabla ya Uteuzi huo Prof. Lawrence Mujungu Museru alikuwa akikaimu nafasi hiyo.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam

03 Oktoba, 2016

Sunday, October 2, 2016

Unyama Unyama: Watafiti Watatu toka Chuo cha Selian Wauawa na Wananchi Kwa Kuchomwa Moto Wakidhaniwa ni Wanyonya Damu

Yowe ya kuvamiwa na wanyonya damu , iliyopigwa na wanawake waliokuwa wakichimba chumvi katika Kijiji cha Iringa-Mvumi wilayani Chamwino, Mkoa wa Dodoma ndiyo iliyosababisha kuuawa kwa watafiti wa Chuo cha Utafiti wa Udongo na Maendeleo ya Ardhi cha Selian mkoani Arusha.

Watafiti hao waliuawa juzi kwa kukatwa katwa mapanga na minde, kisha kuchomwa moto. Gari la Serikali aina ya Toyota Hillux, pia lilichomwa moto.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba wanawashikilia watu kadhaa akiwamo mwenyekiti wa kijiji.

Alisema mwenyekiti wa kitongoji alipigiwa simu na mmoja wa wanawake waliokuwa eneo la tukio kwamba kuna wanyonya damu wamevamia kijiji.

Mambosasa alisema kwa kuwa mwenyekiti huyo alikuwa mbali, alimpigia simu mwenyekiti wa kijiji aende eneo la tukio kujua kilichotokea. Alisema mwenyekiti wa kijiji alipofika hakuamini maelezo ya watafiti hao na kuanza kuwashambulia.

Mambosasa alisema mtu mwingine alikwenda kijijini na kumueleza mchungaji wa kanisa kuhusu kijiji kuvamiwa na nyonya damu, naye akatagaza kwenye kipaza sauti kwamba kijiji kimevamia na watu hao.

Alisema wanakijiji walijitokeza kwenda eneo la tukio na kuwashambulia watafiti hao hadi kufa.

Mkuu wa Mkoa, Jordan Rugimbana alisema baada ya kutembelea eneo la tukio, ameamua kuwasimamisha kazi kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya Chamwino na ofisa utumishi wa wilaya hiyo kwa madai ya kutosambaza barua za kuwatambulisha watafiti hao katika maeneo waliyokwenda kufanya kazi.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Simon Kawea alisema taarifa alizozipata kutoka kwa diwani wa kata ya Iringa-Mvumi, watafiti hao walipofika katika eneo la Makamwa walikutana na watu na kuwauliza kilipo kijiji cha Iringa-Mvumi.

Kawea alisema watafiti hao walipofika eneo walilotaka kufanya utafiti walipigiwa yowe kwamba ni wanyonya damu.

Alisema baada ya kelele zile wanakijiji waliokuwa katika mkutano walisikia na kutoka na mapanga na silaha za jadi kisha kuwavamia watafiti hao na kuwashambulia kwa silaha hizo.

“Hata walipoonyesha vielelezo wao si wezi bali ni watafiti waliopewa kibali na halmashauri ya Chamwino na vielelezo vingine, wanakijiji walikataa na kuendelea kuwapiga,” alisema.

Alisema watendaji wa kijiji hicho na diwani wa kata hiyo, Robert Chikole waliwasihi wanakijiji kuwaacha watafiti hao lakini walizidiwa nguvu na wananchi.

Aliongeza: “Hata polisi walifika muda mfupi, walikuta wameumizwa vibaya wakarusha risasi juu lakini walizidiwa nguvu na kukaa pembeni. Kwa kweli wamekufa katika tukio la kinyama,” alisema.

Alisema watafiti hao walikwenda katika ofisi za Wilaya ya Chamwino na kupata kibali kabla ya kwenda kijijini hapo kwa ajili ya kufanya utafiti wa udongo.

Alisema diwani, mtendaji na mwenyekiti wa kijiji wanashikiliwa na polisi kuhusiana na tukio hilo.

Habari kutoka kijijini hapo zinasema wanakijiji wamekimbia makazi yao kutokana na msako wa polisi kwenye eneo hilo.

Majonzi yatawala Arusha
Mauaji ya hayo yameibua simanzi katika taasisi ya Selian na familia zao, ikiwamo ya mkurugenzi wa taasisi hiyo, Dk January Mfuru ambaye mtoto wake pia ameuawa.

Mtoto huyo, Faraji Mafuru amehitimu Chuo cha Mipango Dodoma hivi karibuni na alikuwa katika mazoezi kwa vitendo.

Mratibu wa utafiti katika kituo hicho, Dk Charles Lyamchai alisema tukio hilo limetokea wakati timu ya watafiti wa kituo hicho ikiwa mkoani Dodoma kutekeleza mradi wa kukusanya sampuli za udongo kwa ajili ya kuziingiza kwenye kanzidata ya Taifa.

“Hawa walikuwa kwenye mradi maalumu ambao umeanza mwaka 2014 na wapo wengine watafiti ambao wamesambaa kwenda mkoani Dodoma kwa kazi hii,” alisema.

Aliwataja wengine waliouawa kuwa ni dereva Nicas Magazine na Mtafiti wa maabara ya udongo, Teddy Lumanga.

“Wapo watumishi 10 huko kutoka hapa kituoni, waliokwenda kutekeleza mradi wa kutambua kiwango cha rutuba kwenye udongo nchini ambao tumeshaukamilisha kwenye wilaya zote za mikoa ya Kanda ya Kaskazini na Katavi na wilaya ya Kondoa, hili ni jambo la kushtua sana,” alisema.

Alisema watafiti hao walikuwa katika wiki ya pili na hawakuwa wamepata matatizo yeyote tangu wafike Dodoma, baada ya tukio hilo kiongozi wa msafara aliwasiliana na kituo.

Dk Lyamchai alisema kabla ya  kwenda huwa wanatoa taarifa kwa kuandika barua kwenye wilaya husika, pia maeneo ya vijijini huwa wanaambatana na mabwana shamba.

“Watafiti wetu hawana mahusiano yoyote na masuala ya damu, walikuwa kwenye kazi zao na walitoa taarifa hadi ofisi ya kata ila hatujui ni kwa nini tukio hili limejitokeza,” alisema.

Mtafiti mwandamizi wa kituo hicho, Dk Lameck Makoye alisema hawajawahi kukutana na changamoto kubwa kama hiyo hasa maeneo ambayo huwa na historia ya wenyeji wasiopenda wageni.

Alisema Dk Mafuru na watafiti wengine waliondoka jana kwendas Dodoma kuungana na watafiti wengine kutoka Kituo cha Hombolo na Makutupola kwenda eneo la tukio.

Selian ni miongoni mwa vituo maarufu katika Ukanda wa Afrika ya Mashariki na Kati kwa kufanya tafiti za mazao katika maeneo yenye ukame nchini.

ACT-Wazalendo waitisha mkutano wa kidemokrasia Kupigania Upatikanaji wa Katiba Mpya


Chama cha ACT- Wazalendo kimepanga kuwasha moto mjadala wa Katiba mpya katika mkutano wake kidemokrasia kilioitisha jijini Dar es Salaam Oktoba 8. 
Mkutano huo unalenga kufufua mchakato wa Katiba Mpya kwa kuzingatia michakato ya katiba za nchi nyingine za Afrika, alisema Katibu wa itikadi na uenezi wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu alipozungumza na waandishi jijini Dar es Salaam  jana. 
Alisema katika kupata uzoefu, ACT Wazalendo imemualika Adabu Namwamba, ambaye ni kiongozi wa Chama cha Labour cha Kenya kilichofanikiwa kubadilisha katiba yake baada ya mchakato mrefu. 
 Aliwataja wageni wengine kuwa ni mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania, Deus Kibamba ambaye naye atatoa mada kuhusu suala hilo. 
Mchakato wa kuandika Katiba mpya nchini umekwama katika hatua ya kupiga Kura ya Maoni baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kushindwa kukamilisha uandikishaji wapigakura kwa muda uliotakiwa. 
Mchakato huo uligubikwa na vikwazo kadhaa, ikiwa ni pamoja na vyama vinne vya upinzani na baadhi ya wajumbe kususia kwa maelezo kuwa Bunge liliacha Rasimu ya Katiba iliyokuwa na maoni ya wananchi na kuingiza sera za CCM. 
Katika mkutano huo, kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe atawasilisha mada kuhusu hali ya nchi kwa mtazamo wa chama hicho. 
“Kiongozi wetu atawasilisha uchambuzi mpana wa kina zaidi kuhusu hali ya nchi yetu kiuchumi, kisiasa na kijamii tangu Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani,” alisema. 
Pia, mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Anna Mghwira, ambaye aligombea urais mwaka jana, ataeleza uzoefu wake katika uchaguzi, wakati mshauri wa chama hicho, Profesa Kitila Mkumbo atachambua mwelekeo wa chama hadi mwaka 2020. 
“Chama kinatoa wito kwa wananchi wanaotaka kushiriki katika mkutano huo kuwasiliana na ofisi ili kujiandikisha,” alisema.