Mkurugenzi
wa Elimu na huduma kwa mlipa kodi wa TRA, Bw. Richard Kayombo amesema
mwenendo wa ukusanyaji mapato ya Serikali kwa sasa ni wa kuridhisha
katika kufikia lengo la kukusanya kiasi cha shilingi trioni 15.1 kwa
mwaka fedha wa 2016/2017.
Mamlaka
ya Mapato nchini (TRA) imekusanya Mapato ya shilingi trilioni 1.37 kwa
Mwezi September kati ya lengo la kukusanya shilingi trilioni 1.4 mwezi
huo
Kuhusu
zoezi la uboreshaji wa taarifa ya namba za utambulisho wa mlipa kodi
linaloendelea jijini Dar es Salaam, Bw. Richard Kayombo amesema mpaka
sasa TRA imetoa vyeti vipya vya TIN kwa watu 15, 467 na zimebaki siku
tisa kukamilisha zoezi hilo.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu
(Sera na Bunge), Bw. Uledi Mussa afuatilie malipo ya kiwanja kilichouzwa
na CDA kwa sh. milioni 240 lakini fedha iliyoingia ofisini ni sh.
milioni 6 tu.
“Katibu
Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, ninataka ufuatilie mauzo ya kiwanja namba
26 block AA eneo la Kikuyu East ambacho kimeuzwa kwa sh. milioni 240
lakini fedha iliyoingia CDA ni sh. milioni 6 tu. Nataka kujua nani
ameingiza milioni 6 na nani kachukua hizo sh. milioni 234,” alisema.
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo jana mchana Alhamisi, Oktoba 6, 2016 wakati
akizungumza na watumishi na viongozi wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao
Makuu Dodoma (CDA) kwenye ukumbi wa Hazina ndogo mjini Dodoma.
Bila
kutoa ufafanuzi zaidi, Waziri Mkuu alisema eneo hilo lilipaswa kuwa na
kituo cha mafuta na akataka apatiwe taarifa mapema iwezekanavyo.
Pia
alimwagiza Katibu Mkuu huyo afuatilie mkataba wa upangishaji wa jengo
la CDA ambalo wamepangishwa taasisi ya Tunakopesha Limited kwa madai
kuwa mhusika alipewa bure na sasa anataka kulipangisha tena ili apate
cha juu.
Waziri
Mkuu aliwaonya watumishi hao pamoja na viongozi wao waache tabia ya
kushirikiana na madalali kuuza viwanja na akawataka wachape kazi
wakijielekeza na kasi ya Serikali ya kuhamia Dodoma.
“Tabia
ya watumishi kushirikiana na madalali kuuza ardhi sasa basi. Hata
hivyo, nimefarijika kukuta mmeanza kuweka mfumo wa kielektoniki katika
baadhi ya huduma. Ni lazima mauzo ya viwanja sasa hivi yafanyike kwa
njia ya kieletroniki, madalali hawana nafasi,” alisisitiza.
Aliutaka
uongozi wa CDA uongeze kasi ya upimaji viwanja kwa sababu mahitaji ni
makubwa lakini akaonya kuwa wakati zoezi hilo likifanyika, wananchi
walionunua viwanja na bado hawajamalizia kuvilipia, wasinyang’anywe kwa
kigezo cha kutaka kuwauzia wengine.
“Mimi
nataka idadi ya viwanja vilivyopimwa iongezeke. Lakini pia msitumie
fursa hii kuwanyang’anya watu wenye umiliki halali eti kwa sababu
Serikali inataka idadi ya viwanja vilivyopimwa iongezeke,” alisema.
“Kama
mtu amepewa offer au hati yake asinyang’anywe hata kama amelipia nusu
asinyang’anywe. Ahimizwe kumalizia hilo deni na ninyi kazi yenu ni
kupima viwanja vingine,” alisisitiza.
“Natambua
mnayo benki ya viwanja, lakini inabidi muongeze idadi ya viwanja vingi
zaidi. Tumeita wawekezaji waje kujenga nyumba za kuishi watumishi,
mahoteli na viwanda na maeneo yote haya inabidi yatengwe rasmi,” alisema.
Alisema
jumla ya viwanja 70,000 vimepimwa tangu CDA ianzishwe mwaka 1973.
Amesema kama wataendelea na kasi hiyo wakati mahitaji yameongezeka,
itawachukua zaidi ya miaka 40 kukamilisha mahitaji ya viwanja 100,000
ambavyo vinatarajiwa kuanza kupimwa hivi karibuni.
Mapema,
akitoa taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mkuu wa CDA, Eng.
Paskasi Muragili alisema usanifu wa upimaji viwanja 20,000 umekamilika
na kwamba wana lengo la kupima viwanja vingine 100,000 ifikapo Juni
2017.
Waziri
Mkuu alitembelea Ofisi ya CDA na kukagua mfumo wa utunzaji mafaili wa
zamani pamoja na uhamishaji wa taarifa za wenye viwanja kwenye mfumo wa
kompyuta. Pia alikagua mifumo ya uuzaji viwanja kwa njia ya mtandao
ambayo hata hivyo bado haijakamilika.
Wakati
huo huo, Waziri Mkuu alipokea mchango wa zaidi ya sh. milioni moja
kutoka kwa Mkuu wa Wilaya wa Kongwa, Bw. Deogratius Ndejembi zikiwa ni
kwa ajili ya wakazi wa mkoa wa Kagera walioathirika kwa tetemeko la
ardhi lilitokea Septemba 10, mwaka huu.
Pia
Waziri Mkuu alipokea mchango mwingine wa zaidi ya sh. milioni tano
kutoka kwa makundi mbalimbali ya wafanyabiasha wa Manispaa ya Dodoma
wakiwemo wamiliki wa hoteli, nyumba za kulala wageni, waendesha bodaboda
na madereva wa daladala.
Akipokea
msaada huo, Waziri Mkuu aliwashukuru wafanyabiashara hao na
kuwahakikishia kwamba fedha hizo zitapelekwa mkoani Kagera na kuwafikia
walengwa kama ilivyokusudiwa.
Kiongozi Mkuu wa Chama Cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ameisifia nguvu
ya vyama vya siasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwa
kile walichokifanya hasa katika uchaguzi wa mwaka jana.
Akizungumza
jana katika mahojiano maalum na kituo cha runinga cha Clouds TV, Zitto
alisema kuwa chama chake hakiwezi kubeza nguvu kubwa iliyooneshwa na
umoja huo na kwamba uliweka historia katika chaguzi zote zilizowahi
kufanyika nchini.
“Ukawa umeweka historia Kubwa zaidi katika
chaguzi za nchi yetu japo kuwa kuna madhaifu ila hatuwezi kupuuza nguvu
ile,” alisema Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini.
Hata
hivyo, pamoja na kusifu nguvu ya muungano huo wa hivyo vya siasa ambavyo
ni Chadema, Chama Cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na NLD, Zitto
alisisitiza kuwa chama chake hakitajiunga na umoja huo kutokana na
maazimio na miiko waliyoiweka katika Azimio la Tabora la chama chake.
“Hatukuweza kujiunga na Ukawa kwasababu tuliweka kanuni zetu wazi tulizozitangaza katika azimio la Tabora,” Zitto anakaririwa.
Katika
hatua nyingine, Zitto alizungumzia mgogoro wa uenyekiti wa CUF
unaoendelea ndani ya chama hicho na kutoa rai kwa vyama vingine vya
siasa kutowafarakanisha.
Alisema kuwa CUF inapaswa kuachiwa suala
hilo walimalize wenyewe katika vikao vyao vya ndani ya chama na sio
vinginevyo.
Aliongeza kuwa kutokana na mgogoro unaoendelea ndani ya CUF,
hivi sasa ajenda yao kubwa [kupinga kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi
mkuu wa Oktoba]imewekwa kando bali sasa wanatafuta uhalali wa kiongozi
wa chama hicho.
“Rai yangu tusichochee kabisa mgogoro huu bali ni
tuwe kama madaraja ya kufanikisha mgogoro huu kumalizimika kwa amani,”
alisema.
Hata hivyo, mapema wiki hii Baraza Kuu la Uongozi wa CUF
lilifungua shauri mahakamani kuhusu mgogoro wa uongozi ndani ya chama
hicho, wakimshataki Msajili vya Vyama vya Siasa nchini pamoja na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Katika shauri hilo, wanapinga uamuzi wa
Msajili kuandika barua ya kumtambua Profesa Ibrahim Lipumba kuwa
Mwenyekiti halali wa chama hicho huku wakidai kuwa alijiuzulu na taarifa
za kujiuzulu kwake waliziwasilisha kwa Msajili.
Baraza hilo
limedai katika shauri hilo kuwa katiba na sheria ya vyama vya siasa
haimpi mamlaka Msajili kuingilia maamuzi ya ndani ya vyama vya siasa.
Shauri hilo bado halijaanza kusikilizwa.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli amewataka watu
wote nchini wanaohodhi mashamba makubwa na kutoyaendeleza wafanye hivyo
ndani ya mwezi mmoja kabla hayawanyang’aya mashamba hayo kwa mujibu wa
sheria na mamlaka aliyonayo.
Akizungumza jana na wananchi mkoani Pwani wakati wa zoezi la kuzindua kiwanda cha kusindika matunda, Rais Dkt. Magufuli alitumia fursa hiyo kuwataka wawekezaji wanaotaka kuja nchini kuwekeza wafanye hivyo kwa kuwa ardhi ipo ya kutosha.
“Nataka
watu wote wanaotaka kuja nchini kuwekeza waje, kwa kuwa ardhi ya
kutosha tunayo na nawataka watu wote waliohodhi ardhi hata kama walikuwa
viongozi huko nyuma nataka wayalime ndani ya mwezi mmoja na kama
wasipofanya hivyo nitabatilisha hati zao za umiliki na kuwapa watu
wengine ambao wapo tayari kuendeleza ardhi hiyo" Alisema Rais Dkt. John Magufuli.
Aidha Rais Magufuli alisema
baadhi ya wafanyabiashara wa sukari nchini wamekuwa siyo waaminifu kwa
kuagiza sukari kwa ajili ya matumizi ya viwandani kutoka nje ya nchi
sukari ambayo ikifika nchini huiweka kwenye mifuko na kuiuza kwa
matumizi ya kawaida ya nyumbani jambo linaloweza kuathiri afya za
watumiaji.
“Tatizo
la sukari liliingia baada ya kuanza kuifuatilia sukari ili sukari
inayopakiwa kwa matumizi ya binadamu iwe hivyo ndipo wafanyabiashara
wakaanza kuficha sukari, ndiyo maana ninataka wawekezaji waje hapa
kuwekeza katika kilimo cha sukari ili sukari izalishwe hapa nchini” Alisema Rais Dkt. Magufuli.
Pamoja na hayo Rais Magufuli alikemea
tabia ya watu kuficha pesa na wengine kuzigeuza katika mfumo wa dolla
na kuzificha chini ya ardhi na kusisitiza wanaofanya hivyo mwisho wake
watakuta pesa hizo zimeharibika huku akiwataka wazitumie kuwekeza katika
viwanda.
Walimu
wanne wa Chuo Kikuu cha Elimu Dar es Salaam (Duce) na cha Kumbukumbu ya
Mwalimu Nyerere waliohusika kumpiga vibaya mwanafunzi wa Shule ya
Sekondari Mbeya wamefukuzwa chuo huku Jeshi la Polisi mkoani Mbeya
likiwashikilia kwa mahojiano walimu wengine watano wa shule hiyo
kutokana na tukio hilo.
Aidha,
serikali imemvua madaraka Mkuu wa shule hiyo, Magreth Haule kwa
kutochukua hatua baada ya kitendo hicho kufanyika shuleni hapo Septemba
28, mwaka huu.
Hatua
hizo zimechukuliwa baada ya jana katika mitandao ya kijamii kusambaa
kipande cha video kikionesha walimu zaidi ya watatu wakiwa eneo la ofisi
wakimshambulia kwa kumpiga makofi, mateke na fimbo sehemu mbalimbali za
mwili hasa kichwani mwanafunzi Sebastian Chinguku.
Waziri
wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce
Ndalichako ametangaza kuwafukuza chuo walimu wanafunzi hao walioshiriki
kitendo cha kumpiga mwanafunzi huyo wa kidato cha tatu wa Shule ya kutwa
ya Sekondari ya Mbeya.
Walimu
hao ni Frank Msigwa (anayedaiwa kumpiga zaidi mwanafunzi huyo kwa
makofi kichwani), John Deo na Sante Gwamaka wote wa Duce na Evans Sanga
wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
Akizungumza
na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana, Profesa Ndalichako
alisema kitendo hicho ni cha kikatili, jinai na kuwa walimu hao
wanafunzi hawafai kuendelea na taaluma hiyo ya ualimu na kuwa hatua
zaidi za kisheria zinaendelea kuchukuliwa dhidi yao.
Profesa
Ndalichako alisema kwa mujibu wa taratibu za vyuo vikuu kitendo
kilichofanywa na walimu wanafunzi hao ni kosa la jinai na kuwa hakiwezi
kufumbiwa macho.
Alitoa
onyo kali kwa wanafunzi wanaokwenda kwenye mafunzo kwa vitendo na
kwenda kinyume cha taaluma yao kuwa wanapoteza sifa hivyo amewataka
kuzingatia maadili ya fani na taaluma wanazosomea.
Mkoani
Mbeya, Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Dhahiri Kidavashari alisema
wanawashikilia walimu wa shule hiyo watano kwa mahojiano kuhusu tukio
hilo. Hata hivyo, alisema si kwamba walimu hao wanaohojiwa ndio
waliohusika na tukio hilo bali wameanza na wale waliopo ili kupata
taarifa zaidi.
“Hatuwezi
kusema sasa hivi kama wale walimu ndio walioonekana katika kipande cha
video kinachosambaa mitandaoni kwa kuwa hili ni suala la mahojiano,
tunaamini hawa tulionao wanaweza wakatupa mwanga,” alisema.
Akieleza
sababu ya adhabu hiyo, Kamanda alisema katika mahojiano ya awali
imebainika kuwa mwalimu wa Kiingereza alitoa kazi, lakini baadhi ya
wanafunzi hawakufanya baadaye mwalimu huyo aliwapa adhabu ya kupiga
magoti, lakini mwanafunzi huyo alionekana kupinga kwa kueleza ana tatizo
la goti hatoweza kufanya adhabu hiyo na mwalimu aliamua kumpeleka
ofisini na kumpiga kwa kumchangia.
“Mwalimu
aliwaadhibu wanafunzi darasani na alipotaka kumuadhibu mwanafunzi huyo
mbele ya darasa, alionesha kupinga kupigwa mbele ya wanafunzi wenzake
ndipo alipoamua kumpeleka ofisini na kutokea tukio linalosambaa,” aliongeza Kidavashari.
Katika
taarifa yake, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba,
alisema Septemba 28 mwaka huu, mwanafunzi Chinguku wa kidato cha tatu wa
Shule ya Sekondari Mbeya, mkazi wa Uyole, alipigwa na walimu watatu.
“Nimeelekeza vyombo vya dola Dar es Salaam wawatafute chuoni kwao hao walimu kuhusiana na shambulio hilo kwa mwanafunzi huyo,” ilisema Mwigulu.
Naye
Waziri katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(Tamisemi), George Simbachawene ameagiza mamlaka za nidhamu kumvua
madaraka Mkuu wa Shule hiyo, Haule kwa kushindwa kuchukua hatua na kutoa
taarifa mara baada ya tukio hilo kufanywa na walimu hao shuleni hapo.
"Kwa
kuwa waliotenda kosa hili wametoweka tangu Septemba 29, 2016 na
hawajulikani walipo, nimesikitishwa kwa kitendo cha mwalimu mkuu wa
shule hiyo, Magreth Haule kutochukua hatua. Hii inaonesha kulikuwa na
dalili za kutaka kulificha tukio hili baya.
“Na
kwa sababu hiyo, pamoja na kwamba wanaendelea kuhojiwa na Polisi,
naagiza mamlaka yake ya nidhamu kumvua madaraka mkuu huyo wa shule," alisema Simbachawene katika taarifa yake kwa umma jana.
Katika
hatua nyingine, Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba
amelaani kitendo kilichofanywa na walimu hao na kukieleza kuwa ni cha
mwituni na cha kinyama kwa kuwa hakuna adhabu kama hiyo katika utumishi
wa ualimu.
"Nami
nimeona hiyo video katika mitandao ya kijamii, kuna sheria za adhabu za
viboko lakini si hii walioifanya hao walimu vijana maana walikuwa
wakipiga makofi, ngumi, mateke, ngwara. Hizi hazipo kwenye ualimu,
lazima wafuate sheria zinazosimamia utumishi wa walimu," alisema Mukoba.
Alishauri
vyuo vya ualimu viweke mkazo katika kufundisha walimu vijana namna ya
kuwa zaidi ya walimu, kuwa na uvumilivu, subira na kuzingatia sheria.
Wafunzwe kisaikolojia kukubali kuwa hawaishii kuwa walimu bali wanaingia
kwenye kundi la malezi.
Alisema
kwa tukio hilo, ni lazima sheria ichukue mkondo wake ili iwe fundisho
kwa wengine wenye tabia hizo hasa walimu vijana kwa kuwa kitaaluma ni
tukio la kinyama lisilokubalika.
“Hata kama mwanafunzi ana makosa, amevuta bangi, huwezi kumuadhibu vile, maana pale hujui nani kavuta bangi nani mzima,” alisema Mukoba.
Awali,
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla alisema serikali inalifuatilia kwa
karibu tukio la kupigwa kama mwizi mwanafunzi huyo wa shule hiyo ya
jijini Mbeya na kusema tayari baadhi ya walimu akiwemo mkuu wa shule,
wanashikiliwa na Polisi.
Makalla
alibainisha hayo jana kwenye Maadhimisho ya Siku ya Fimbo Nyeupe
Duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani Mbeya na kusisitiza kuwa walimu
waliohusika na tukio la kumpiga mwanafunzi wao kama mwizi wanasakwa na
lazima watapatikana.
Alisema
Septemba 26, mwaka huu, mwalimu aliyekuwa katika mafunzo kwa vitendo
katika shule ya Sekondari ya Mbeya Day aliyemtaja kwa jina la Frank
Msigwa alitoa kazi kwa wanafunzi darasani na Septemba 28 alipokuwa
akisahihisha kazi zilizofanyika alibaini baadhi ya wanafunzi
hawakufanya.
Makalla
alifafanua kuwa miongoni mwa wanafunzi aliobaini hawakufanya kazi yake
ni pamoja na Chinguku na ndipo aliwatoa nje ya darasa na kuwapa adhabu
ya kupiga 'push up' lakini mwanafunzi huyo akagoma akidai kuwa na
matatizo ya kiafya katika mbavu zake.
Alisema
baada ya kugomea adhabu hiyo mwalimu aliwaamuru wapige magoti lakini
pia mwanafunzi huyo aligoma akisema ana matatizo ya goti katika moja ya
miguu yake ndipo mwalimu alilazimika kutoa adhabu ya kuwachapa viboko
viwili kila mmoja na aliwapiga wote isipokuwa Chunguku ambaye kama
alivyofanya kwenye adhabu za kwanza hii pia alikataa.
Alisema
baada ya hapo mwalimu huyo alilazimika kwenda kuwaita wenzake wawili
ambao nao walikuwa kwenye mafunzo ya ualimu kwa vitendo shuleni hapo na
wakambeba mwanafunzi huyo hadi ofisini kwao ambako huko ndiko walianza
kumchapa kwa kumchangia kama inavyooneshwa kwenye kipande cha video
kilichosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.
Kwa
mujibu wa Makalla, walimu waliotenda kitendo hicho walitoroka na
hawajulikani walipo. Alisema serikali inaendelea kuwasaka huku walimu
wengine wakihojiwa Polisi.
Jeshi
la Polisi visiwani Zanzibar, limesema litamchukulia hatua za kinidhamu
ofisa wake mwenyewe cheo cha Sajenti ambaye alionekana hivi karibuni
akipokea rushwa kutoka kwa raia wa kigeni.
Hatua
hiyo, imekuja baada ya picha za video kusambaa katika mitandao ya
kijamii, zinazomwonyesha askari huyo akipokea fedha ambazo hadi sasa
hazijajulikana kiwango chake kutoka kwa raia huyo wa kigeni, ambaye
alikuwa na kosa la kutofunga mkanda.
Katika
video hiyo, raia huyo anaokana kutoa fedha na kumkabidhi askari huyo
huku akiahidi kumsaidia ili asikamatwe mbele ya safari.
Tukio
hilo lilitokea eneo la Mkokotoni Mkoa wa Kaskazini Unguja, ingawa
askari huyo alitaja eneo la Mahonda akionyesha nia ovu ya kutenda kosa
hilo bila kujijua kama anachukuliwa video.
Kamishna
wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Hamdani Omar Makame alisema jeshi hilo
linampongeza raia huyo wa kigeni kwa kutoa taarifa hiyo.
“Jeshi
la polisi linachukua nafasi hii kulaani kosa hili, licha ya kua ni kosa
la jinai linalifedhehesha jeshi na kulitia doa kutokana na dhamana
kubwa lililokabidhiwa,” alisema.
Alisema kwa mujibu wa taratibu za jeshi hilo, tayari limeanza uchunguzi mara moja na kwamba litachukua hatua zinazostahili.
Kutokana
na hali hiyo, Kamishina Hamdani amewataka wamiliki wa makampuni ya simu
za mikononi kufufua mfumo wa upigaji simu kutumia namba za dharura
ambazo ni 111 na 112 ili kuwarahisishia wananchi kutoa taarifa.